Sessions Management

Parliament Proceedings

Contribution onSittingSitting date
Makaridio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa Mwaka wa Fedha 20100/2012 42Aug 9, 2011
Displaying 1-5 of 54 result(s).
Hon. Dr. Cyril August Chami Contribution
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia taarifa iliyowasilishwa leo hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Viwanda na Biashara
ambayo ilichambua Bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara?


Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu sasa likubali kupokea, kujadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka 2011/2012.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete - Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuchaguliwa tena kuiongoza nchi kwa kipindi cha pili cha miaka mitano. Hii inadhihirisha imani kubwa walionayo wananchi kwa Mheshimiwa Rais na Chama cha Mapinduzi kwa sera zake nzuri za kukuza uchumi na kuongeza
kipato cha wananchi. Aidha, napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Tisa wa Afrika wa Uwekezaji (9th Africa Investment Forum 2011, "Accelerating East African Investment and Accessing a Market of a Billion People") uliofanyika tarehe 17 hadi 19 Aprili, 2011 jijini Dar es Salaam. Mkutano huo ulikuwa jukwaa muhimu la kutangaza fursa za uwekezaji, kuimarisha biashara Barani Afrika hususan Tanzania na kujenga ubia mpya katika shughuli za kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru pia Mheshimiwa Rais kwa ziara yake aliyoifanya Wizarani kwangu tarehe 1 Aprili, 2011. Nachukua fursa hii kumhakikishia Mheshimiwa Rais kuwa tutaendelea kuzingatia miongozo na maelekezo aliyoyatoa katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia kutumia fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal kwa kuchaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha miaka mitano. Aidha, nampongeza kwa kuhamasisha uhifadhi wa mazingira yanayozingatia maendeleo endelevu katika Sekta ya Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Kwa namna ya pekee nawapongeza Mheshimiwa Seif Sharif Hamad kwa kuteuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Mheshimiwa Balozi Seif Ali Idd kwa kuteuliwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Nawatakia mafanikio mema katika kutekeleza
shughuli za kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nimpongeze Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda - Mbunge wa Katavi (CCM), kwa kuchaguliwa bila kupingwa kuwa Mbunge na hatimaye kuteuliwa tena na kuthibitishwa na Bunge kwa kura nyingi kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Spika kwa kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Njombe Kusini (CCM) na pia kwa kuwa mwanamke wa kwanza Tanzania kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vilevile, nampongeza Mheshimiwa Job Yustino Ndugai - Mbunge wa Kongwa (CCM), kwa kuchaguliwa kuwa Naibu Spika na wewe Mwenyekiti na wenyeviti wenzako wawili wa Bunge hili kwa kuaminiwa na Bunge letu na kupewa nyadhifa mlizonazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Mawaziri wenzangu wote, pamoja na Naibu Mawaziri, kwanza kwa kuchaguliwa kuwa Wabunge na pili kwa kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushika nyadhifa hizo. Aidha, napenda kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa imani aliyonayo kwetu kwa kututeua mimi na pia Naibu Waziri, Mheshimiwa Lazaro S. Nyalandu - Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM) kuongoza na kusimamia majukumu ya Wizara ya Viwanda
na Biashara.

Mwisho, lakini siyo kwa umuhimu, napenda niwapongeze Waheshimiwa Wabunge wote
kwa kuchaguliwa au kuteuliwa kuingia katika Bunge hili Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia niwashukuru kipekee kabisa wapigakura wa Jimbo langu la Moshi Vijijini kwa kunichagua kwa mara nyingine kuwa Mbunge katika Bunge lako Tukufu. Binafsi, nawashukuru kwa ushirikiano walionipa katika kipindi chote nikiwa mwakilishi wao hapa Bungeni. Nawaahidi kuendelea kuwapa ushirikiano wa dhati kwa kipindi hiki katika kuleta maendeleo na ustawi wa Jimbo letu. Aidha, namshukuru mke wangu, watoto, ndugu zangu na Watanzania kwa ujumla kwa upendo na ushirikiano ambao wameendelea kunipa na hivyo kuniwezesha kutekeleza majukumu yangu inavyopaswa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa shukurani zangu za dhati kwa Kamati ya Bunge ya Viwanda na Biashara ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Mheshimiwa Mahmoud Hassan Mgimwa - Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kaskazini (CCM) akisaidiwa na Makamu wake, Mheshimiwa Mhandisi
Stella M. Manyanya - Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), kwa ushauri wao wenye ubunifu na maelekezo wakati wa kujadili muhtasari wa makadirio ya matumizi ya Wizara hii. Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba hoja na michango ya Kamati imezingatiwa katika hotuba ninayoiwasilisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kukushukuru Mheshimiwa Spika, Naibu Spika, Wenyeviti wa Kamati za Bunge, Katibu wa Bunge na Watendaji wote wa Bunge pamoja na Bunge lako Tukufu kwa ushirikiano tunaoupata katika kuwasilisha Miswada mbalimbali ya Sheria na mapendekezo ya Bajeti ya Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, napenda kuwahakikishia kuwa mchango na ushauri wenu utazingatiwa ili kuhakikisha kuwa malengo tuliyojiwekea yanafikiwa kwa manufaa na ustawi wa nchi yetu na jamii ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee, napenda kuwapongeza na kuwashukuru Mawaziri walionitangulia kuwasilisha hoja zao, hususan Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda - Mbunge wa Jimbo la Katavi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hotuba yake fasaha na inayoonyesha mafanikio ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne. Pia, napenda kumpongeza Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Mustafa Haidi Mkulo - Mbunge wa Jimbo la Kilosa (CCM) kwa hotuba yake ambayo imetoa mwelekeo wa uchumi wetu ikiwa ni pamoja na malengo ya Bajeti ya Serikali. Bajeti hiyo imelenga kukuza uchumi na kupunguza umasikini kwa kuzingatia utekelezaji wa MKUKUTA II, Kilimo Kwanza na Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa
Miaka Mitano (2011/2012 - 2015/2016) wa Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutumia fursa hii kuzishukuru Wizara na Taasisi za Serikali na wadau wote, hususan Asasi za sekta binafsi zikiwemo Baraza la Kilimo Tanzania, Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania, Chama cha Wadau wa Ngozi na Mazao yake, Chama cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo Tanzania, Baraza la Taifa la Biashara, Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania, Chama cha Wafanyabiashara Wanawake na Vikundi vya Biashara Ndogo, kwa michango yao katika kuendeleza Sekta ya Viwanda, Biashara, Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo na Masoko ambazo Wizara yangu inazisimamia. Aidha, ninawashukuru wananchi kwa ushirikiano waliotupa katika kipindi chote kilichopita. Ni matumaini yangu kuwa wataendeleza ushirikiano ili kuchangia maendeleo ya Sekta na Uchumi wa nchi yetu.


Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee napenda kuwashukuru viongozi wenzangu wa Wizara ya Viwanda na Biashara ambao ni Naibu Waziri - Mheshimiwa Lazaro S. Nyalandu, Katibu Mkuu - Bibi Joyce K. G. Mapunjo, Naibu Katibu Mkuu - Dkt. Shaaban R. Mwinjaka na Wakuu wa Idara na Taasisi zilizo chini ya Wizara. Aidha, nawashukuru wataalamu na wafanyakazi wote wa Wizara na Taasisi zake kwa kujituma katika kutekeleza majukumu yao. Vilevile, ninawashukuru wale wote tulioshirikiana nao katika maandalizi ya hotuba hii ninayoiwasilisha leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kumshukuru Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali na wachapaji wengine kwa kuchapisha machapisho mbalimbali ya Wizara yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010, ukurasa wa 47 - 53 hususan Ibara ya 49, 50, 51, 52, 53 na 54 yamewekwa malengo ya maendeleo endelevu ya Sekta ya Viwanda, Biashara na Masoko kwa kipindi cha mwaka 2010 - 2015. Napenda nichukue fursa hii kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Wizara umezingatia utekelezaji wa maelekezo ya Ilani. Mafanikio yaliyopatikana hadi sasa ni kama
ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika uwekezaji, Wizara kupitia Mamlaka ya Maeneo Huru ya Uzalishaji kwa Mauzo Nje (EPZA), Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na Mamlaka ya Serikali za Mitaa imeendelea kutenga maeneo maalumu ya uwekezaji katika Mikoa yote nchini. Maeneo haya yatawekewa miundombinu ya msingi ili kuvutia sekta binafsi kujenga viwanda na kufanya biashara katika maeneo hayo.

Hatua hiyo itapunguza changamoto ya upatikanaji wa ardhi kwa wawekezaji wanaotaka
kuanzisha viwanda nchini. Aidha, kupitia sheria za Maeneo Maalumu ya Uzalishaji kwa Mauzo Nje (EPZ) na Maeneo Maalumu ya Uwekezaji (SEZ), Serikali imebainisha vivutio mbalimbali ikiwa ni pamoja na nafuu za kodi ili kuhamasisha ushiriki wa sekta binafsi katika uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara pia inaandaa utaratibu wa kuanzisha Kituo Kimoja cha Huduma za Uwekezaji (One Stop Services Centre) katika eneo maalumu la uwekezaji la Benjamin William Mkapa, kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji wa huduma zote muhimu zinazohusika na uwekezaji wa viwanda. Wizara inaendelea kushirikiana na taasisi zinazohusika na utoaji wa mikopo hususan Benki ya Raslimali Tanzania (TIB) ili kurahisisha upatikanaji wa mitaji ya kuwekeza katika viwanda na biashara. Wizara kupitia SIDO na TanTrade imeendelea kutoa mafunzo kwa wajasiriamali mbalimbali kuhusiana na uzalishaji wa bidhaa zenye ubora ili kuweza kuhimili ushindani katika soko la ndani na nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuinua uwezo na kuimarisha ujuzi unaohitajika viwandani, Wizara kwa kushirikiana na Serikali ya Japan, Benki ya Dunia na Chuo Kikuu cha GRIPS - Tokyo ilitoa mafunzo yajulikanayo kwa jina la KAIZEN yenye lengo la kuongeza tija, ufanisi, usimamizi wa shughuli za viwanda na kuongeza ubora wa bidhaa. Mafunzo hayo yalitolewa kwa wajasiriamali 113 wenye viwanda vya nguo na mavazi waliopo katika Mkoa wa Dar es Salaam. Programu hiyo ilikuwa ya majaribio (pilot).

Matokeo ya programu hiyo ambayo ndiyo iliyoiinua Sekta ya Viwanda kwa nchi za Japan, Taiwan, Korea, Malaysia, Singapore, China, nchi za Ulaya na Amerika ya Kaskazini yamepata mwitikio mkubwa. Wizara imekamilisha Mkakati wa KAIZEN utakaohusisha sekta ndogo zote za viwanda (sub sectors). Serikali ya Japan itafadhili programu hiyo kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania ili kujenga na kuimarisha stadi kwa ajili ya shughuli za viwanda kupitia Programu ya KAIZEN.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha upatikanaji wa wataalamu wa ngozi (leather technologists), Wizara kwa kushirikiana na Chuo cha Teknolojia cha Dar es Salaam (DIT) inaendelea na ufufuaji na uendelezaji wa Chuo cha Teknolojia ya Ngozi cha Mwanza (TILT). Jitihada hizo zimewezesha kuanza mafunzo ya muda mfupi ya utengenezaji wa bidhaa za ngozi kuanzia mwezi Julai, 2011 na baadaye mafunzo ya muda mrefu katika fani ya leather technologists baada ya ukarabati wa majengo kukamilika. Vilevile, Tanzania Gatsby Foundation (TGF) wanashirikiana na College of Engineering and Technology (CoET) Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ili kuanzisha mafunzo ya wataalamu wa nguo (textile technologists).

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kujenga mifumo imara ya viwanda, biashara na masoko yenye kuendeleza na kukuza mauzo nje, Wizara imeendelea kuimarisha mifumo ya EPZ na SEZ kwa kuipa nguvu ya kisheria EPZA kusimamia Mfumo wa SEZ. Kwa kutumia Mfumo wa SEZ, wawekezaji katika sekta mbalimbali za uchumi wanaotaka kuuza bidhaa katika masoko ya nje na ya ndani wataweza kuwekeza kupitia mfumo huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kupitia programu za EPZ na SEZ, Wizara imetenga maeneo mbalimbali nchini hususan yale ya mipakani kwa lengo la kutumia fursa za biashara za mipakani. Maeneo hayo yapo katika Mikoa ya Arusha, Kagera, Kigoma, Kilimanjaro, Iringa, Lindi, Manyara, Mara, Mbeya, Morogoro, Mtwara, Mwanza, Pwani, Ruvuma, Singida, Shinyanga na Tanga. Maeneo haya yatatumika kama vitovu vya kujenga viwanda vya kuongeza thamani mazao na kuuza nchi jirani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuimarisha Kifedha Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) ili kiwe Chombo Madhubuti cha Kuchochea Mapinduzi ya Viwanda Nchini kwa Kutoa Mikopo ya Muda Mrefu na Riba Nafuu kwa Wawekezaji Wakubwa, wa Kati na Wadogo Nchini
Kote

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imeandaa programu za kusaidia upatikanaji na udhamini wa mikopo ya kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya kusindika mazao ya kilimo na mifugo ambapo andiko la programu mbili za kushirikiana na TIB na SIDO limekamilika. Programu ya mikopo
kupitia TIB inaitwa Industrial Development Support Loan (IDSL) ambayo inalenga Serikali kutoa ruzuku ya asilimia tano ya riba inayotozwa na TIB. Programu ya pili ni ya kupitia SIDO inayoitwa Industrial Credit Guarantee Initiative (ICGI) ambapo SIDO itatakiwa kutoa dhamana ya mikopo midogo itakayotolewa na NMB kwa wajasiriamali. Utekelezaji wa programu hizi unategemea upatikanaji wa fedha za Kilimo Kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuwekeza katika Mradi wa Makaa ya Mawe ya Mchuchuma, Chuma cha Liganga na Viwanda vya Kemikali na Mbolea katika Kanda za Maendeleo kikiwemo Kiwanda cha Mbolea aina ya Urea Mkoani Mtwara na kuwezesha Kiwanda
cha Minjingu kuzalisha mbolea bora ya NPK na MPR ili kufikia lengo lililowekwa

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na juhudi za muda mrefu zilizofanywa na Wizara kupitia NDC za kuvutia wawekezaji katika miradi ya makaa ya mawe ya Mchuchuma na Chuma cha Liganga, mwekezaji katika miradi hii alipatikana mwezi Januari 2011, ambaye ni Kampuni ya Sichuan Hongda Corporation Limited ya China. Majadiliano ya awali yalifanyika mwezi Januari, 2011 na majadiliano ya mkataba wa ubia yanaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Makaa ya Mawe wa Mchuchuma unahusisha uzalishaji wa umeme wa Megawati 600 ambao utatumika katika uchenjuaji na uyeyushaji wa madini ya chuma na chuma ghafi na bakaa kuingizwa kwenye gridi ya Taifa. Kwa kuanzia na chuma ghafi tani milioni moja kwa mwaka kitazalishwa ambacho kitatumika kuzalisha bidhaa mbalimbali za chuma (iron and steel products) nchini. Katika uzalishaji huo, yatapatikana pia madini adimu ya Vanadium na Titanium ambayo yana thamani kubwa zaidi kuliko chuma chenyewe. Aidha, utekelezaji wa miradi hiyo ambayo itakwenda sambamba na uhakiki wa makaa ya mawe, uchorongaji na upembuzi yakinifu kwa mradi wa chuma unatarajiwa kuanza mwaka 2011/2012. Mwekezaji huyo atawekeza kiasi cha Dola za Kimarekani bilioni tatu kwa ajili ya kutekeleza miradi ya chuma na makaa ya mawe kwa mfumo unganishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mrefu Serikali imekuwa na juhudi za kuanzisha kiwanda cha mbolea kwa kutumia gesi asili Mkoani Mtwara. Nafurahi kulieleza Bunge lako Tukufu kuwa juhudi hizo zimepata mafanikio ambapo mwezi Februari, 2011 mwendelezaji wa mradi wa gesi asili ya Mnazi Bay, Kampuni ya Wentworth Resources Limited (WRL) ambayo imenunua hisa za Artumas Energy (T) Ltd ameonyesha nia ya kuwekeza katika uzalishaji wa mbolea.

WRL inaendelea na uandaaji wa upembuzi yakinifu na uchimbaji wa visima zaidi vya gesi ili kupata malighafi ya kutosha ya kuzalisha mbolea aina ya Urea na kemikali ya Methanol kwa matumizi ya viwanda. Kwa upande mwingine, Kampuni ya Minjingu Mines and Fertilizer Ltd. (MMFL) inayozalisha mbolea aina ya Minjingu Rock Phosphate (MRP), imefanya upanuzi wa Kiwanda ambao umeongeza uwezo wa uzalishaji kutoka tani 75,000 kwa mwaka hadi tani 100,000 za MRP. Aidha, mbolea itakayozalishwa sasa itakuwa aina ya NPK ambayo ina ubora zaidi kuliko ya MRP baada ya kiwanda kuongeza naitrojeni katika idadi ya malighafi zake za uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu suala la kuimarisha uzalishaji mali viwandani kwa kuvifufua na kuviendeleza kwa teknolojia ya kisasa viwanda vyote ambavyo viliuzwa huko nyuma kisha kutelekezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ufuatiliaji na tathmini ya mwaka 2007/2008 wa viwanda vilivyobinafsishwa ulibainisha kuwepo mafanikio kwa baadhi ya viwanda na mashirika yaliyobinafsishwa ambapo mashirika 42 kati ya 74 yalitekeleza mikataba kama ilivyokubalika na kuwekeza zaidi ya kiwango cha mikataba.

Aidha, viwanda na makampuni 15 yaliwekeza chini ya kiwango kilichokubalika katika mikataba ya ubinafsishaji, na hivyo utendaji ni wa kulegalega. Mengi ya hayo ni yale yaliyobinafsishwa kupitia utaratibu wa kuwauzia wafanyakazi na menejimenti (Employee Management Buy-Out-MEBO). Aidha, ilibainika kwamba viwanda 17 wawekezaji wameshindwa kuvifufua na hivyo vimefungwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya viwanda vinavyoendelea na uzalishaji saba
vilivyobadilisha biashara ya awali kutokana na sababu mbalimbali zikiwepo ushindani katika soko la bidhaa zilizokuwa zinazalishwa awali. Viwanda hivi vinaendelea vizuri na vinazalisha bidhaa bora tofauti na za awali. Aidha, mashirika na viwanda 17 vilivyofungwa ni kutokana na kuwekeza kwa kiwango ambacho hakikidhi mahitaji na hivyo bidhaa zilizozalishwa zikashindwa kuhimili ushindani.

Tathmini hiyo ilibainisha pia kuwa baadhi ya viwanda vimeongeza uzalishaji na hata kukuza mchango katika pato la Taifa ikiwa ni pamoja na kuongeza ajira na kutumia teknolojia ya kisasa. Mifano ya baadhi ya viwanda vinavyofanya vizuri ni pamoja na Tanzania Breweries Ltd, Tanzania Cigarette Company Ltd, Tanzania Portland Cement Company Ltd, Tanga Cement Company Ltd, Mbeya Cement Company Ltd, Tanzania Distillers Company Ltd, 21st Century Textiles Mills Ltd, ALAF, East African Cable (T) Ltd, Nampack Tanzania Ltd, Dar Brew (T) Ltd., TANELEC Ltd, Tanzania Pharmaceutical Industries Ltd, Tanzania Steel Pipes na NAMERA Group (Sunguratex).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia kuwa muda umepita tangu uperembaji wa kwanza ulipofanyika na kutokana na sababu kwamba taarifa iliandaliwa na kutoa mapendekezo ya jumla ya hatua za kuchukuliwa kwa wale ambao hawajafufua viwanda na mashirika waliyouziwa, mwezi Juni, 2011 Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Consolidated Holdings Corporation (CHC) iliunda kikosi kazi kwa lengo la kufanya uchambuzi wa kina zaidi na kutoa mapendekezo yanayotekelezeka kwa kuzingatia masharti yaliyomo kwenye mikataba ya mauzo,
hasa kwa kuzingatia kwamba viwanda hivi vinafufuliwa na kufanya kazi kama ilivyokusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu kuboresha vivutio kwa ajili ya uwekezaji kwenye viwanda vitakavyotumia malighafi mbalimbali zilizopo nchini vikiwemo Viwanda vya nguo, ngozi, usindikaji matunda, mbogamboga na usanifu wa madini ya vito.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jitihada za kukuza uwekezaji kwenye viwanda vya kuongeza thamani katika mazao, Wizara imeendelea kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Fedha ili kutoa vivutio mbalimbali kwa wawekezaji. Vivutio hivyo ni pamoja na misamaha mbalimbali ya kodi kwa wawekezaji wanaozalisha bidhaa na kuuza nje kupitia mfumo wa EPZ; kuandaa maeneo na kuyawekea miundombinu ya msingi kama maji, umeme, barabara kama ilivyofanyika katika eneo la Uwekezaji la Benjamin Wiliam Mkapa na kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kupunguza muda wa kusajili makampuni yanayowekeza katika maeneo ya EPZ, muda wa kutoa leseni na muda wa kufungua na kufunga biashara katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ipo katika hatua za awali za kuwezesha upatikanaji wa mikopo maalumu kwa wajasiriamali katika usindikaji wa mazao ya kilimo kwa kutumia programu za Industrial Development Support Loans (IDLS) kupitia Benki ya Raslimali Tanzania (TIB) na Industrial Credit Guarantee Initiative (ICGI) kupitia SIDO. Hatua nyingine ni pamoja na kuandaa na kuwasilisha mapendekezo ya sekta mbalimbali katika vikao vya kujadili marekebisho ya mfumo wa kodi ili kuwa na ushindani wa haki kati ya bidhaa za viwanda vya ndani na zile zinazoagizwa kutoka nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia Mamlaka ya EPZ imeendelea kubainisha maeneo ya uwekezaji ya EPZ na SEZ na kuhamasisha uwekezaji ndani ya maeneo hayo. Kwa ujumla, mpaka sasa viwanda 44 vinavyozalisha bidhaa chini ya EPZ vimeanzishwa. Viwanda hivi vimewekeza jumla ya mtaji wa Dola za Kimarekani milioni 650 na vimetoa ajira 13,000 za moja kwa moja. Aidha, ujenzi wa miundombinu katika eneo maalumu la uwekezaji la Benjamin William Mkapa Special Economic Zones (BWM-SEZ) umekamilika ambapo viwanja 14 katika eneo hilo vimetolewa kwa wawekezaji. Mbali na maeneo ya awali ya Millenium Business Park (Dar es Salaam), Hifadhi EPZ (Dar es Salaam) na Kisongo EPZ (Arusha), maeneo mapya yaliyoanzishwa na sekta binafsi ni Global Industrial Park Mkuranga (Pwani), Rusumo Falls SEZ (Kagera) na inayoendelea kujengwa ya Kamal EPZ Industrial Park, Bagamoyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kampuni ya Kamal Group inaendeleza eneo la EPZ lenye ukubwa wa ekari 300 ambapo ujenzi wa miundombinu ya msingi umekamilika kwa asilimia 80. Tayari Makampuni manne yameshaanza kujenga viwanda katika eneo la Kamal EPZ Industrial Park. Kati ya viwanda hivyo, ni kiwanda kikubwa cha kuzalisha chuma kitakachogharimu kiasi cha
dola za Kimarekani milioni 222. Kiwanda hiki kitakuwa miongoni mwa viwanda vikubwa na vya kisasa vya uzalishaji wa chuma katika Afrika ambapo kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 700,000 kwa mwaka na kuajiri zaidi ya wafanyakazi 5,000 wa moja kwa moja. Uzalishaji unatarajiwa kuanza katikati ya mwaka 2012.

Vingine ni Kiwanda cha Kusindika mazao ya kilimo cha Kamal Agro Ltd kinachotarajiwa kuanza uzalishaji Desemba, 2011; kiwanda cha kusafisha mafuta machafu cha Kamal Refinery Ltd kitakachoanza uzalishaji mwezi Novemba, 2011; Kiwanda cha kuzalisha gesi ya Acetylene ya kutumika viwandani cha Kamal Acetylene Ltd ambacho kilianza uzalishaji mwishoni mwa mwezi Juni, 2011 na Kiwanda cha kuzalisha mbegu bora kwa kutumia bioteknolojia ya Kamal Seeds Ltd. Aidha, Makampuni mbalimbali makubwa kama S. S. Controls Ltd., Lotus Packaging Ltd., Accumen Holding Ltd., U.K Cable Ltd.; Lotus Battery Ltd. na Lotus Appliances Ltd. yamethibitisha nia ya kuwekeza katika eneo la Kamal Industrial Estate EPZ.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Sekta binafsi kupitia Chama cha Wadau wa Ngozi Tanzania (Leather Association of Tanzania - LAT) imeendelea kutekeleza Mkakati Unganishi wa Kufufua na Kuendeleza Sekta na Viwanda vya bidhaa za ngozi nchini. Mkakati huo unaotekelezwa kwa kutumia fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Mifugo (Livestock Development Fund), una lengo la kukuza uwezo wa viwanda vya ndani ili kusindika ngozi zote hapa nchini badala ya kuuza nje zikiwa ghafi. Kwa sasa vipo viwanda nane vya kusindika ngozi vyenye uwezo wa kusindika futi mraba milioni 73.9. Hata hivyo, uzalishaji halisi ni futi za mraba 34.3 sawa na asilimia 46.41 ya uwezo wa viwanda hivyo. Pamoja na uwezo mdogo wa uzalishaji, thamani ya mauzo ya ngozi zilizosindikwa na kuuzwa nje ya nchi yameongezeka kutoka Shilingi bilioni 6.8 mwaka 2009 hadi Shilingi bilioni 8.4 mwaka 2010 sawa na ongezeko la asilimia 23.5.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla Sekta Ndogo ya Ngozi inaendelea kuimarika, kwani tumeanza kuona bidhaa za ngozi sokoni na hata ajira kuongezeka kutoka wafanyakazi 520 mwaka 2009 hadi 1,150 mwaka 2010. Mafanikio mengine yaliyopatikana kutokana na utekelezaji wa mkakati huo ni pamoja na kufanyika kwa mafunzo ya usindikaji wa ngozi na utengenezaji wa bidhaa za ngozi kwa Mikoa 15 ya Tanzania Bara. Mikoa hiyo ni Arusha, Kagera, Kilimanjaro, Iringa, Manyara, Mara, Mbeya, Morogoro, Mwanza, Pwani, Ruvuma, Singida, Shinyanga, Tabora na Tanga. Hadi sasa, jumla ya washiriki 500 wamepata mafunzo hayo na wanaendelea na
utengenezaji wa bidhaa za ngozi na usindikaji wa ngozi vijijini kwa kutumia njia za asili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafurahi kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba Wizara ilikipatia Kituo cha SIDO Dodoma mashine 25 za uzalishaji wa bidhaa za ngozi. Mashine hizo zinatumika kutoa mafunzo ya utengenezaji wa bidhaa za ngozi kwa wajasiriamali ili hatimaye waweze kuanzisha viwanda vyao vidogo vidogo, ili kujiajiri na kutoa ajira kwa wengine. Kituo hiki nilikizindua tarehe 18 Juni, 2011 na wakati huo wa uzinduzi, wajasiriamali 17 walikuwa wanaendelea na mafunzo. Kituo hiki kimeshatoa mafunzo kwa wajasiriamali 74 ambao wameanzisha viwanda vidogo saba kwa kujiunga kwenye vikundi vya uzalishaji, viwili tayari vimeandikishwa na vitano viko katika mchakato wa uandikishwaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kwa kushirikiana na wadau imeendelea na zoezi la kuandaa taarifa kuhusu fursa za uwekezaji katika miradi mbalimbali ya maendeleo ya viwanda hapa nchini. Uandaaji na uainishaji wa fursa za uwekezaji na miradi ulipewa kipaumbele katika Kanda za Maendeleo za Mtwara, Kati na Kaskazini. Aidha, Wizara inatekeleza Mkakati Unganishi wa Maendeleo ya Viwanda na Mpango Kabambe unaolenga kuziendeleza sekta ndogo za viwanda kwa kuainisha sekta za kipaumbele. Sekta hizo ni pamoja na usindikaji wa mazao ya kilimo na mifugo yatakayozalishwa katika kanda hizo kwa ajili ya malighafi za viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukanda wa Kaskazini, sekta za kipaumbele ni za kuzalisha nguo, nyama, ngozi na bidhaa za ngozi, maziwa na bidhaa zake, matunda na mbogamboga. Katika Ukanda wa Kati, kipaumbele ni uzalishaji wa mafuta ya kula, ngozi na bidhaa zake, nguo, saruji na vifaa vingine vya ujenzi vikiwemo nondo na mabati. Katika Ukanda wa Mtwara, kipaumbele ni viwanda vya korosho, chuma na bidhaa za chuma, saruji, mbolea, na kemikali
ambazo zinatokana na gesi asili. Wizara kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), Balozi za Tanzania na wadau wengine itaendelea kuzitangaza fursa hizo kwa lengo la kupata wawekezaji wa ndani na wa nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imeendelea kusimamia na kuratibu utekelezaji wa Programu ya Muunganisho wa Ujasiriamali Vijijini (MUVI) yenye lengo la kuongeza ufanisi wa mlolongo wa thamani wa bidhaa za mazao ya alizeti, mihogo, mifugo, matunda na nyanya ili kuimarisha kipato cha mzalishaji na hatimaye kupunguza umaskini. Katika mwaka 2010/2011, Mikoa sita iliyoainishwa katika programu hii ilichagua Wilaya zitakazokuwa katika mpango huo. Wilaya hizo ni Iringa Vijijini, Kilolo na Njombe kwa Mkoa wa Iringa; Simanjiro, Hanang na Babati kwa Mkoa wa Manyara; Sengerema kwa Mkoa wa Mwanza, Bagamoyo, Rufiji na Mkuranga kwa Mkoa wa Pwani; Songea Vijijini, Namtumbo na Mbinga kwa Mkoa wa Ruvuma; Kwimba na Ukerewe kwa Mkoa wa Mwanza na Muheza, Korogwe, Kilindi na Handeni kwa Mkoa wa Tanga.

Baadhi ya shughuli nyingine zilizotekelezwa katika Wilaya hizo ni pamoja na kuhamasisha uanzishwaji na uimarishaji wa vyama/vikundi vya wazalishaji na wakulima, kuimarisha mifumo ya usambazaji wa mbegu bora na pembejeo, kuwaelimisha wakulima dhana ya kilimo cha biashara, kuanzisha majukwaa ya kuratibu shughuli za sekta za mazao yaliyochaguliwa, na kuanzisha na kuendeleza mifumo unganishi ya masoko (market linkages).

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jitihada za kuongeza mchango wa Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo kwenye Pato la Taifa, Wizara imeendelea kusimamia utekelezaji wa programu mbalimbali zikiwemo Muunganisho Ujasiriamali Vijijini (MUVI) na Mkakati wa Wilaya Moja Bidhaa Moja (ODOP). Programu hizo zinalenga kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo pamoja na usindikaji wake kwa lengo la kukuza uzalishaji na kujenga uchumi imara ambao hatimaye utaweza kuchangia katika Pato la Taifa kutoka asilimia 33 ya sasa na kufikia asilimia 40 mwaka 2015.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, jumla ya teknolojia mpya 312 zimetafutwa kutoka ndani na nje ya nchi kwa ajili ya matumizi ya miradi ya uzalishaji. Aidha, SIDO kupitia vituo vyake vya uendelezaji wa teknolojia vilivyopo Mbeya, Arusha, Kilimanjaro, Lindi na Kigoma iliwezesha utengenezaji wa mashine mpya za aina mbalimbali 506 na vipuri 1,622 na usambazaji kwa watumiaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kutoa elimu na kuwajengea uwezo wakulima wa kusindika mazao kabla ya kuyauza kama vile usindikaji wa asali, utengenezaji wa mvinyo, utengenezaji wa juisi pamoja na ufungashaji wa bidhaa kwa kutumia teknolojia ya TBS.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kwa kushirikiana na SIDO imekuwa ikitoa mafunzo mbalimbali kwa Wajasiriamali ili kuwaimarisha katika kuendesha na kuendeleza shughuli za biashara na miradi ya uzalishaji. Mafunzo yaliyotolewa ni pamoja na ufugaji na utengenezaji wa mizinga ya nyuki, usindikaji na ufungashaji wa asali ambapo wafugaji wa nyuki wapatao 566 walipata mafunzo hayo. Aidha, wasindikaji 20 wa zao la alizeti kutoka Mji wa Makambako Mkoani Iringa walibainishwa na kuunganishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS). Vile vile, jumla ya wajasiriamali 15,722 kupitia kozi 564 wamepata mafunzo yaliyowawezesha kupata maarifa na stadi za kuimarisha shughuli zao za uzalishaji mali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kusaidia kukuza na kuboresha bidhaa za wajasirimali wadogo, Wizara kwa kushirikiana na SIDO imeweza kuwaunganisha Wajasiriamali wadogo na makampuni makubwa na za kati ambapo wajasiriamali 58 waliunganishwa na makampuni ya Nyanza Mine Tobacco Authority; Prume Timber Ltd; Intermec Engineering; Wilddersun Safaris Ltd; Lake Victoria Sardins; Misanga Mini Supermarket; SAUT University; Katapala Engineering Safari Co. Ltd; Mohamed Enterprises; Lavena na U-Tum Supermarkets katika Mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Morogoro, Mwanza, Rukwa na Tabora. Hatua hii imewasaidia wajasiriamali wadogo kuzalisha bidhaa zenye ubora na kuweza kupata masoko kwenye makampuni hayo makubwa na ya kati.

Mheshimiwa Mwenyekiti,Wizara imefanya jitihada mbalimbali katika kuijengea uwezo SIDO,
licha ya kuwa na bajeti ndogo mwaka hadi mwaka. Katika mwaka 2010/2011, Serikali imeweza kupeleka baadhi ya maofisa wa SIDO katika mafunzo na semina mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kitaalamu wa kuwahudumia wajasiriamali wadogo kwa ufanisi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, Wizara imeweza kukamilisha mapitio ya majukumu, kazi na Sheria Na. 28/1973 iliyoanzisha SIDO ili kuboresha utendaji wa Shirika. Hatua inayofuata ni Serikali kuridhia mapendekezo yaliyotolewa na Mtaalamu Mwelekezi na ushauri mbalimbali uliotolewa na wadau wa Sekta hiyo. Aidha, Serikali imeendelea kuongeza mtaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Wajasiriamali Wadogo (NEDF) ili kuhudumia wajasiriamali wengi zaidi. Mfuko huo ulianzishwa na Serikali mwaka 1994 kwa mtaji wa shilingi milioni 800. Serikali imekuwa ikichangia fedha za Mfuko kiasi cha shilingi milioni 500 kila mwaka kutoka mwaka 2006/2007 hadi 2010/2011. Kiwango cha juu cha ukopeshwaji kilikuwa Sh. 500,000/= ambacho kilirekebishwa mwaka 2008 hadi kufikia shilingi milioni 2.5 kwa shughuli za uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka 2010/2011, Wizara kupitia SIDO imekamilisha ujenzi wa jengo la kongano (industrial clusters) ya usindikaji wa vyakula Kemondo Mkoani Kagera na kukarabati majengo ya kongano Kigoma kwa bidhaa zitokanazo na zao la mchikichi. Aidha, Wizara inaendelea kushirikiana na wadau wengine wakiwemo Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na sekta binafsi katika kutenga na kuendeleza maeneo kwa ajili ya wenye viwanda vidogo na biashara ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhamasisha matumizi ya fursa za masoko ya ndani, kikanda na kimataifa zikiwemo fursa za masoko ya AGOA, EBA, China, Japan, Canada na India ili
kukuza biashara ya nje kwa kiwango kikubwa

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka 2010/2011 Wizara imeendelea kuhamasisha jumuiya ya wafanyabiashara kuhusu fursa za masoko zilizopo ndani ya nchi, kikanda na kimataifa kwa kutoa taarifa hizo kupitia taasisi zinazowawakilisha wafanyabiashara, kuwaunganisha kutoka nje katika mikutano ya ana kwa ana na kupitia warsha mbalimbali za kikanda. Aidha, mauzo ya bidhaa kwenye masoko hayo ya upendeleo yamekuwa yakiongezeka. Kwa mfano, mauzo katika soko la China yaliongezeka kutoka shilingi bilioni 491.9 mwaka 2009/2010 hadi shilingi bilioni 908.3 mwaka 2010/2011 sawa na ongezeko la asilimia 84.7.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mauzo katika soko la India yaliongezeka kutoka shilingi bilioni 242.5 mwaka 2009 hadi shilingi bilioni 312.9 mwaka 2010 sawa na ongezeko la asilimia 29. Mauzo katika soko la Marekani kupitia mpango wa AGOA yaliongezeka kutoka Dola za Kimarekani milioni 1.8 mwaka 2009 hadi Dola za Kimarekani milioni 2.1 mwaka 2010 sawa na ongezeko la asilimia 16.7.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imeendelea kuwajengea uwezo wajasiriamali kwa kutoa mafunzo na mbinu mbalimbali za kuyafikia masoko ya nje yaliyotolewa kwa njia ya warsha na semina. Mafunzo hayo yamekuwa yakiendeshwa kwa vikundi kupitia Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na kupitia Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade). Mafunzo yaliyotolewa yalihusu biashara kwa ujumla na mauzo nje (Train for Trade and Export Readiness). Mafunzo hayo yalifanyika katika Mikoa ya Arusha na Dar es Salaam na kushirikisha jumla ya wajasiriamali 55. Lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha wajasiriamali kujua masharti na mahitaji ya soko hususan viwango vya ubora wa kimataifa ili kuziwezesha bidhaa husika kumudu ushindani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyokwishasema hapo juu, majadiliano ya Ubia wa Uchumi (Economic Partnership Agreement -EPA) kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Ulaya (EU) yameendelea tangu pande hizi mbili zilipotiliana saini ya awali (initialing) Mkataba wa Mpito wa EPA (Framework for Economic Partnership Agreement-FEPA) tarehe 27 Novemba, 2007 mjini Kampala- Uganda. Kuanzia mwezi Juni, 2010 kasi ya majadiliano ilipungua kutokana na tofauti zilizojitokeza kwa pande zote mbili na hasa Jumuiya ya Ulaya pale iliposhindwa kukubaliana na matakwa ya msingi ya EAC hasa suala la Ushirikiano wa Kiuchumi na
Maendeleo.

Nchi wanachama wa EAC wanataka Jumuiya ya Ulaya kuongeza misaada ya kifedha zaidi ya zile zinazotolewa chini ya Mfuko wa Maendeleo ya Jumuiya hiyo (EDF) ili kuzisaidia nchi za EAC kutatua changamoto za uzalishaji duni, miundombinu na vikwazo vingine visivyo vya kiushuru ili kunufaika na fursa za masoko zilizotolewa na Jumuiya ya Ulaya jambo ambalo EU hawakubaliani nalo.

Aidha, EU imeweka masharti kwa nchi za EAC baada ya kusainiwa kwa mkataba wa EPA. Masharti hayo ni pamoja na kuzuia kuongeza kodi kwa bidhaa zitakazouzwa katika soko la EU na kutoa upendeleo sawa kwa EU pale nchi za EAC zitakapoingia makubaliano na nchi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi na kuzipa fursa zaidi ya zile ilizotoa kwa EU. Nchi za EU wanataka nchi za EAC kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ya kuongeza kodi kwenye bidhaa watoe taarifa kwa EU kupitia Baraza la EPA litakaloundwa na ambalo litakuwa linakutana mara moja kila baada ya miaka miwili.

Kutoza kodi baadhi ya bidhaa na hasa bidhaa ghafi kunalenga kushawishi uongezaji thamani bidhaa na hivyo kukuza viwanda vya ndani na hatimaye kuongeza ajira na kupunguza umaskini. Masharti hayo yanazinyima nchi za EAC kuwa na uhuru (policy space) wa kuamua mambo yao yenye kuleta maendeleo. Tofauti hizi zilisababisha kusitishwa kusainiwa kwa mkataba wa mpito wa EPA-FEPA. Majadiliano ya EPA yataendelea ili kuondoa tofauti zilizojitokeza kwa lengo la kukamilika ifikapo mwezi Desemba, 2011 ili kuwezesha kusainiwa kwa mkataba kamili wa EPA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jumuiya ya Afrika Mashariki imeingia katika hatua ya tatu ambayo ni ya Soko la Pamoja kati ya hatua tano za mtangamano ambazo ni Eneo Huru la Biashara, Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja, Umoja wa Sarafu na Shirikisho la Kisiasa. Itifaki ya Soko la Pamoja ilisainiwa rasmi na Wakuu wa nchi za Jumuiya tarehe 29 Novemba, 2009 na utekelezaji wake ulianza rasmi tarehe 1 Julai, 2010.

Hatua ya Soko la Pamoja inategemewa kuongeza zaidi fursa za masoko ya biashara ya huduma, soko la mitaji, uhuru wa watu kuingia nchi wanachama na kuanzisha shughuli za kiuchumi na uhuru wa kufanya kazi popote katika nchi wanachama. Kwa kutambua fursa
zitokanazo na Soko la Pamoja, Wizara kwa kushirikiana na asasi zinazowawakilisha
wafanyabiashara kama TCCIA, CTI, TPSF, VIBINDO na TAFOPA imeendelea kuwahamasisha wafanyabiashara kuzichangamkia fursa hizo kwa lengo la kuongeza kipato na hatimaye kuchangia katika ukuaji wa uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika juhudi za kupunguza gharama za kufanya biashara katika Jumuiya za EAC na SADC, nchi wanachama zimefanya utafiti wa Vikwazo vya Biashara Visivyo vya Kiushuru (Non Tarrif Barriers - NTBs) katika kila nchi. Kutokana na matokeo ya utafiti, ili kuondoa vikwazo Wizara kwa kushirikiana na wadau imeunda Kamati ya Kitaifa itakayofanya kazi ya kuainisha, kufuatilia na kutoa taarifa ya vikwazo vilivyopo na vinavyojitokeza na kupendekeza njia ya kuvitatua.

Vilevile, nchi wanachama wa Jumuiya hizi zimeunda Kamati ya Kikanda ambayo inajumuisha Waratibu wa Kamati za Kitaifa (National Focal and Enquiry Points) ambayo inaratibu hali ya Vikwazo Visivyo vya Kiushuru katika nchi wanachama na kupendekeza hatua za kuviondoa. Wajumbe wa Kamati hizo vilevile wamepatiwa mafunzo ya namna ya kupashana habari kwa njia ya mtandao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kwa kushirikiana na wadau ilifanya utafiti wa kina kuhusu maeneo yanayoongeza gharama za kufanya biashara nchini. Baada ya utafiti, mpango
maalumu (road map) unaoeleza vikwazo vilivyopo na njia ya kuvitatua uliandaliwa.

Aidha, kila mdau anayehusika na utekelezaji wa mapendekezo ya kuboresha mazingira
ya kufanya biashara nchini alishirikishwa na kupewa taarifa kwa utekelezaji. Maeneo ambayo yanafanyiwa kazi ni pamoja na kupunguza muda wa kusajili kampuni, majina ya biashara, kupata leseni za biashara, kupunguza vizuizi vya barabarani (road blocks), kurahisisha utoaji wa mizigo bandarini, kurahisisha taratibu za kuvuka mipakani na kupunguza muda wa kupata vibali vya kuendesha shughuli za uwekezaji kama vile vibali vya ujenzi (building permit). Maeneo ya kipaumbele ambayo yamefanyiwa kazi ili kupunguza gharama za kufanya biashara pamoja na kurahisisha taratibu za kupata leseni za biashara katika Mamlaka ya Halmashauri kwa kutenganisha mahitaji ya mipango miji na afya kwenye maombi ya leseni za biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Maafisa Afya na Mipango Miji watatekeleza majukumu yao ya usimamizi wa afya na mipango miji bila kufungamanishwa na maombi ya leseni za biashara kama ilivyokuwa hapo awali. Maeneo mengine yaliyofanyiwa kazi ni pamoja na kuwezesha kupatikana kwa baadhi ya huduma za usajili wa makampuni na majina ya biashara katika mtandao wa kumpyuta (tovuti ya BRELA- www.brela-tz.org).

Aidha, tovuti hii ina taarifa zote za huduma ikiwa ni pamoja na fomu zote zinazohitajika katika kupata huduma zitolewazo na BRELA) na kuanza kutolewa kwa huduma za udhibiti kwa pamoja katika bandari na vituo vya mipakani (one stop centre) kwa kuzifanya taasisi za udhibiti kama vile TBS, TFDA, Wakala wa Vipimo, Wakaguzi wa mimea na mifugo zitafanya kazi kwa pamoja na kuwa na ofisi katika jengo moja zitaanza kutolewa. Idadi ya vizuizi vya barabarani vimepunguzwa na kubakiza vile vinavyohusu mizani za barabarani, usalama na vituo vya TRA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia TanTrade ina mpango wa kuanzisha vituo vya biashara vya kanda kwa kuanzia na mikoa ya Arusha, Mbeya na Mwanza. TanTrade tayari imefanikiwa kupata jengo la kupanga NSSF, Mwanza kwa ajili ya kituo cha biashara Kanda ya Ziwa na taratibu zinafanyika ili kupata fedha za kulipia kodi ya pango na kupata kibali cha kuajiri watumishi kwa ajili ya ofisi hiyo mpya. Kwa vituo vingine, taratibu zitaendelea kufanyika kadri uwezo utakavyoruhusu.

Wizara kwa kushirikiana na TanTrade ilihamasisha wajasiriamali kushiriki katika Maonesho ya Kimataifa ya Dar es Salaam na Maonesho ya Kisekta. Pia, iliwahamasisha na kuwawezesha kushiriki Maonesho ya Nairobi International Trade Fair, African Commodity Exhibition (ACE) Yiwu, China, Maonesho ya Kimataifa ya Msumbiji, Maonesho ya Kimataifa ya Malawi na Maonesho ya EXPO 2010 yaliyofanyika Shanghai, China. Aidha, katika maonyesho ya mwaka huu nchi 17 zilishiriki pamoja na makampuni ya nje 364, wakati mwaka 2010 makampuni ya nje yaliyoshiriki ni 216, hili likiwa ni ongezeko la washiriki 148. Washiriki wa ndani walikuwa 1100 ukilinganisha na washiriki 995 mwaka 2010. Nafurahi kuliarifu Bunge lako kuwa Maonesho yamefikia viwango vya juu vya ubora
kimataifa kwa kutunukiwa cheti safi kutoka Shirikisho la Maonesho ya Biashara Duniani (UFI).

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imeendelea na utafiti wa masoko kwa kufuatilia mienendo ya bei ya mazao makuu ya chakula na biashara kwa lengo la kupanua wigo wa mahitaji na kuwapatia wazalishaji bei nzuri zaidi. Bei ya mkulima kwa mazao makuu ya biashara yakiwemo kahawa aina ya arabika, chai, pamba, mkonge na korosho iliongezeka kwa viwango tofauti.

Aidha, bei ya mlaji kwa mazao makuu ya chakula hususan mahindi, mchele, ngano, ulezi na mtama ilipungua na bei za maharage, uwele na sukari ziliongezeka katika msimu wa mwaka 2010/2011 ikilinganishwa na bei za msimu wa mwaka 2009/2010. Kutokana na ongezeko kubwa la bei ya sukari, Serikali iliingilia kati kwa kutoa bei elekezi na maelekezo maalumu kwa wazalishaji na wasambazaji wa sukari nchini kusambaza na kuhakikisha kuwa bei ya mlaji haizidi kiasi cha Sh.1,700/= kwa kilo. Serikali pia ilipunguza kiwango cha ushuru wa kuagiza sukari toka nje ya nchi ili kupunguza makali ya bei ya sukari nchini. Hata hivyo, ufanisi haukuwa kwa asilimia 100 kwa sababu ya wafanyabiashara wa rejareja(retailers) wenye tamaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika imefanya utafiti kuwezesha kupata soko kwa tumbaku ya Tanzania nchini China na Uturuki. Wafanyabiashara kutoka nchini China wameonyesha nia ya kununua tumbaku hiyo. Wizara inafanya pia juhudi za kuwezesha tumbaku ya Tanzania kuingizwa katika orodha ya bidhaa
zinazoruhusiwa kuuzwa nchini China bila ushuru na ukomo (duty free quota free) kupitia Mkataba
Maalumu wa Upendeleo (Special Preferential Tariff Agreement)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika uanzisha programu ya kuwa na utambulisho wa kitaifa kwa bidhaa Wizara kwa kushirikiana na Shirika la Utafiti wa Viwanda (TIRDO) na Sekta Binafsi kwa kuhusisha kikamilifu vyama vya wenye viwanda na wafanyabiashara nchini kutoka Tanzania Bara na Visiwani TPSF, CTI, TCCIA, ZNCCA, TAHA, TWCC, Tea Association of Tanzania, Cashewnuts Processors Association, na kadhalika, imewezesha upatikanaji wa huduma ya usajili wa kutumia nembo za mistari (bar codes) na huduma nyingine zinazotolewa na Kampuni ya Kimataifa ya GS1 yenye Makao Makuu huko Brussels, Ubelgiji. Majukumu yaliyofanywa ni pamoja na kufanya upembuzi yakinifu kuhusu utayari wa Tanzania kama nchi kuingia katika mfumo huo, kutoa mafunzo kwa wadau, kuitisha Mkutano wa Kitaifa wa Wadau na kuwezesha kuanzishwa kwa chombo kitakachosimamia na kuratibu utoaji wa bar codes hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafurahi kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa Tanzania
imekubalika kuwa kati ya nchi zitakazotoa nembo za utambuzi wa bidhaa (bar codes) kwenye kikao cha GS1 General Assembly 2011, kilichofanyika tarehe 14 - 19 Mei, Paris, Ufaransa na kuifanya Tanzania kuwa mwanachama wa GS1. Haya ni mafanikio makubwa kwa nchi yetu, kwani wenye viwanda na wafanyabiashara wetu hasa wajasiriamali watapata huduma hii hapa nchini kwa bei nafuu badala ya kufuatilia huduma hii nchini Kenya na Afrika ya Kusini. Hii itasaidia sana kukuza mauzo ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na huduma hii ya nembo ya utambuzi (bar codes), tumewezesha uanzishwaji wa chombo kitakachosaidia huduma ya vifungashio (packaging) hapa nchini Tanzania Institute of Packaging. Huduma hii ilizinduliwa hapa nchini tarehe 3 Agosti, 2011 ambapo Rais wa World Packaging Authority alishiriki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma hizi mbili, bar codes na packaging ni muhimu sana katika maendeleo ya viwanda, biashara na masoko. Serikali haifanyi bishara lakini inalo jukumu la kuiwezesha sekta binafsi ili iweze kutoa bidhaa bora na hivyo kushindana katika masoko ndani na nje ya nchi. Kwa misingi hiyo, Wizara itaendelea kushirikiana na sekta binafsi kwa kupitia vyama vya wenye viwanda na wafanyabishara (TPSF, ZNCCIA, CTI, TCCIA, TAHA, ACT na TWCC) kuhakikisha kuwa huduma hizi mbili zinakidhi malengo yaliyotarajiwa na kuwanufaisha wadau wote na kuhakikisha huduma zote muhimu katika kuendeleza Viwanda na Biashara zinapatikana hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kwa kushirikiana na Wizara za Sekta ya Kilimo, sekta binafsi, Washirika wa Maendeleo, Asasi zisizo za Kiserikali na Taasisi za Elimu ya Juu imekamilisha Mkakati wa Masoko ya Mazao na Bidhaa za Kilimo ili kuwezesha utekelezaji wa Sera ya Masoko ya Mazao na Bidhaa za Kilimo. Waraka wa Baraza la Mawaziri kutoa taarifa ya utekelezaji umeandaliwa. Katika kurahisisha utekelezaji wa Mkakati huo, Wizara imetafsiri Sera ya Masoko ya Mazao ya kilimo kwa lugha ya Kiswahili na uandishi wa mkakati katika lugha rahisi (popular version) umeanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuendeleza Miundombinu ya Masoko ya Mikoa na kuanzisha masoko katika vituo vya mipakani ili kukuza biashara ya ndani na kikanda Wizara kwa kupitia Mradi wa Uwekezaji Katika Sekta ya Kilimo (DASIP) imefanya makubaliano ya kujenga masoko sita katika mikoa ya Kagera, Kigoma, Mara na Shinyanga. Masoko hayo yatajengwa katika mipaka ya Manyovu, Mtukula, Murongo, Kabanga na Sirari na pia Bandari Kavu ya Isaka Wilayani Kahama. DASIP inakamilisha mpango wa kumpata mshauri mwelekezi wa kuandaa michoro na gharama za ujenzi. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Programu ya Market Infrastructure, Value Addition and Rural Financing (MIVRF) itajenga masoko manne ya mipakani na maghala kwa ajili ya matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za mazao ghalani. Programu hiyo itaanza kutekelezwa mwanzoni mwa mwaka wa fedha 2011/2012. Aidha, Wizara kupitia Mipango ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo ya Wilaya (DADPs) na Mradi wa DASIP inaendelea na ujenzi wa masoko ya mazao ya kilimo katika Halmashauri mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kufanikisha ujenzi wa masoko ya kimataifa katika miji
midogo ya Segera na Makambako, Wizara iliingia mkataba na Chuo Kikuu cha Ardhi kama Mshauri Mwelekezi kuandaa Mpango Kamambe (Master Plan) ya masoko hayo. Mshauri Mwelekezi huyo amekamilisha rasimu ya Mpango huo. Uchambuzi wa awali wa Mpango huo umefanywa na Wizara na maoni yamewasilishwa kwa Mshauri Mwelekezi ili ukamilishwe. Aidha, changamoto zilizojitokeza za upatikanaji wa eneo la kutosha huko Makambako zimepatiwa ufumbuzi kwa kushirikiana na Uongozi wa Mkoa wa Iringa. Ujenzi wa masoko hayo utategemea upatikanaji wa fedha/wawekezaji. Wizara itaendelea na juhudi za kutafuta fedha kutoka kwa wawekezaji au kupitia miradi ya maendeleo hususan ile inayolenga kufanikisha azma ya Kilimo Kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imeendelea kuratibu uanzishwaji wa Vituo vya Pamoja vya Mipakani (One Stop Boarder Posts) ili kurahisisha ufanyaji biashara na nchi jirani kwa kupunguza muda unaotumika kukamilisha taratibu za watu na mizigo kuvuka mpakani, pia kuwawezesha wafanyabisahara wetu kutumia vizuri fursa tulizonazo katika mipaka yetu. Katika kufanikisha zoezi hilo, utafiti wa mahitaji ya ujenzi wa Kituo (needs assessment) upande wa Tanzania (kwa Kituo cha Tunduma) umekamilika kwa kushirikiana na Trade Mark E.A. Hatua hizo ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano kati ya Serikali yetu na Serikali ya Zambia ya kujenga Kituo cha Pamoja katika mpaka wa Tunduma/Nakonde. Aidha, utafiti kama huo umefanyika kuwezesha ujenzi wa Kituo cha Pamoja cha Mpakani mwa Tanzania na Burundi eneo la Kabanga/Kobero na majadiliano kati ya pande hizo mbili yanaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imetembelea maeneo ya mipaka kwenye vituo vya Kabanga, Kasumulu, Mtukula, Namanga, Rusumo na Tunduma ili kutathmini urahisi wa kufanya biashara na nchi jirani na pia kuhamasisha uanzishwaji wa mfumo wa utendaji kazi wa pamoja (One Stop Centre) kwa Taasisi za Umma zinazosimamia Sheria za Biashara Mipakani. Taasisi mbalimbali hususan Mamlaka ya Mapato, Wakala wa Vipimo, Shirika la Viwango Tanzania, Mamlaka ya Chakula na Madawa na Wakaguzi wa Mazao ya Kilimo na Mifugo watawezeshwa kufanya kazi kwa pamoja ili kuondoa usumbufu kwa wafanyabiashara kuwatafuta katika maeneo mbalimbali. Lengo ni kurahisisha ufanyaji biashara kwa kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za biashara kwa kupunguza muda wa kukagua na kuidhinisha bidhaa kupita mipakani.

Aidha, Kamati za ufuatiliaji kazi pamoja mipakani (Joint Border Committee - JBC) zimekwishaundwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania imepewa jukumu la kuongoza Kamati hizo katika kila mpaka. Katika utekelezaji wa mfumo wa utendaji kazi wa pamoja, Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, na Taasisi za TBS, TFDA, TRA na WMA zimekwishapewa Ofisi ya Pamoja katika Mamlaka ya Bandari Tanzania ili kurahisisha utaratibu wa uingizaji na utoaji wa mizigo nchini kupitia Bandari ya Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hatua hizo, Wizara pia imetembelea masoko ya mipakani ya Kasanga, Kasesya, Kasumulu, Kipili, Kirando na Tunduma na kutoa elimu kwa wajasiriamali kuhusu umuhimu wa kurasimisha biashara na mbinu za kufanya biashara kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa. Aidha, wataalamu walisaidia wajasiriamali kuanzisha vikundi na kuvisajili, ambapo jumla ya vikundi 40 vilisajiliwa BRELA kutoka katika maeneo hayo. Vilevile, Wizara kwa kushirikiana na SIDO iliendesha warsha ya urasimishaji biashara pamoja na taratibu nyingine za ufanyaji biashara kwa wajasiriamali katika kanda ya Kaskazini mjini Moshi mwezi Mei, 2011, ambapo wajasiriamali 21 walisajili majina ya biashara. Mafunzo haya yataendelezwa katika kanda zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza Mkakati wa Kukuza Mauzo Nje na Mpango Unganishi wa Biashara, rasimu ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Biashara (Trade Sector Development Programme - TSDP) imewasilishwa kwa Washirika wa Maendeleo (Development Patners-DPs) ambao wanatarajiwa kuchangia fedha kwenye mfuko (Mult-donor Basket Fund) utakaotumika katika utekelezaji wa Programu hiyo. Hadi sasa nchi ya Sweden kupitia Shirika lake la Maendeleo ya Kimataifa (Sida) imeonesha nia ya kuchangia kwenye Mfuko wa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu ya kwanza ya utekelezaji wa TSDP itaanza kwa:-

(a) Kutekeleza miradi inayolenga kuimarisha uwezo wa Serikali kusimamia na
kufuatilia utekelezaji wa programu;

(b) Kuwezesha utekelezaji wa mkakati na mpango kazi wa kitaifa wa kuendeleza
biashara ya maua, matunda na mbogamboga kupitia Mkakati wa Kuendeleza Mazao ya Maua,
Matunda na Mboga (National Horticultural Development Strategy);

(c) Kuboresha huduma katika sekta ya utalii kwa kuainisha na kupanga madaraja ya
mahoteli ya kitalii (Classification and Grading of Accomodation Establishments) kwa kufuata mfumo wa kimataifa katika Mikoa ya Arusha na Manyara kwa upande wa Tanzania Bara na
Zanzibar; na

(d) Kurazinisha sheria, kanuni na taratibu za usimamizi wa viwango vya mazao ya
chakula na mifugo (Sanitary and Phytosanitary-SPS-standards) vinavyolenga kulinda afya za binadamu, wanyama na mimea na kujenga uelewa wa wauzaji wa bidhaa nje ya nchi kuhusu hakimiliki (Intellectual Property Rights-IPRs).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na juhudi mbalimbali za Serikali ikiwa ni pamoja na kuhamasisha ununuzi wa bidhaa za ndani kwa kupitia kauli mbiu ya 'Nunua Bidhaa za Tanzania Jenga Tanzania', Wizara imetayarisha Waraka wa kuvikuza, kuviendeleza na kuvilinda viwanda vya ndani ambapo kauli mbiu hiyo inasisitizwa ili kufikia lengo la kuendeleza sekta ya viwanda nchini.

Kauli mbiu hiyo inakwenda sambamba na uboreshaji na ufungashaji wa bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali hapa nchini. Ili kutimiza azma hiyo, Wizara kupitia Shirika la Viwango Tanzania limetoa mafunzo ya ubora wa bidhaa na ufungashaji bora kwa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati (SMEs) 292 katika Mikoa ya Iringa, Manyara, Mtwara, Singida na Tanga. Sampuli za bidhaa 359 zilipimwa katika maabara za TBS. Aidha, wajasiriamali 55 walipewa leseni za kutumia alama ya ubora ya 'TBS' kwa bidhaa za maji, unga wa mahindi, mvinyo, mafuta ya alizeti, mikate, jibini, nyama, achari, asali, sabuni ya maji, sabuni za kuogea, siagi, jamu, juisi na chaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuboresha na Kupanua Wigo wa Biashara Mtandao Katika Ngazi ya Wilaya, Mkoa hadi Taifa,Wizara imeandaa Mfumo wa Usajili wa Shughuli za Biashara (software) kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA). Mafunzo ya matumizi ya mfumo huo yalitolewa kwa Maafisa Biashara na Wataalamu wa mifumo wa Halmashauri za Majiji, Miji, Manispaa na Wilaya 24.

Aidha, Kompyuta 24 pamoja na vifaa vyake (accessories), zilinunuliwa na kusambazwa katika Halmashauri hizo. Uteuzi wa Wasajili (Registrar) katika Halmashauri za Wilaya unafanyika kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI. Aidha, Wizara imefanya Mkutano na Wakurugenzi Watendaji wa Wilaya 24 kuhusu Sheria ya Business Activities Registration Act - BARA ili kurahisisha usimamizi wa utekelezaji wa Sheria hiyo. Pamoja na juhudi hizo za Wizara, BRELA imeweka huduma mbalimbali katika tovuti yake www.brela-tz.org ikiwa ni pamoja na taarifa zote za huduma zitolewazo na BRELA pamoja na fomu zote zinazohitajika katika kupata huduma zinazotolewa na BRELA .

Mheshimiwa Mwenyekiti, BRELA imekamilisha rasimu ya makubaliano kati yake na TCCIA kushirikiana katika kutoa huduma saidizi kwa wateja hadi katika ngazi ya Wilaya kwa kuwa tayari wana mfumo wa kiteknolojia unaowasiliana katika Wilaya 95. BRELA imeanza kutembelea baadhi ya vituo vya TCCIA kwa lengo la kujionea hali halisi ya zana za kufanyia kazi, na pia kutoa elimu kwa wafanyabiashara na wajasiriamali ili wafahamu uwepo wa huduma hizo katika Ofisi za TCCIA zilizo karibu nao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuboresha mazingira ya biashara nchini, Wizara imetenganisha utaratibu wa kupitisha fomu za maombi ya leseni za biashara kwa Maafisa Mipango Miji na Maafisa Afya ili kuwarahisishia wafanyabiashara kujipatia leseni za biashara na hivyo kuongeza wigo wa kurasimisha biashara. Hatua hizo zimechukuliwa katika kipindi hiki cha
mpito ambapo Wizara inaendelea na maandalizi ya kuanza utekelezaji wa Sheria ya Usajili wa Shughuli za Biashara (BARA). Utekelezaji wa Sheria hiyo unategemewa kuanza mara baada ya kukamilisha maandalizi katika Wilaya zote nchini. Maandalizi hayo yamepangwa kukamilishwa katika robo ya kwanza ya mwaka 2011/2012.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2010/2011, Wizara imeendelea kuhamasisha wazalishaji kutumia njia mbalimbali za mawasiliano zikiwemo simu za kiganjani ili kupata taarifa za masoko katika maeneo wanayoishi. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji kupitia kwa Wakusanya Taarifa za Masoko walioko katika Halmashauri na Mikoa, tumeendelea kusambaza taarifa za masoko na hivyo kuwezesha kuwepo kwa njia mbalimbali za mawasiliano hususan magazeti, mtandao wa kompyuta (internet), redio na luninga.

Wizara imetoa mafunzo kwa wakusanya taarifa za mifugo na mazao ya kilimo kuhusiana na ukusanyaji, usambazaji na jinsi ya kupata taarifa za masoko kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu (SMS) ili nao wawaelimishe wadau katika maeneo yao. Sambamba na jitihada hizo tayari makampuni ya simu za mkononi yakiwemo Vodacom na Airtel yameanzisha huduma hiyo na hivyo kufanya upatikanaji wa taarifa hizo kuwa rahisi zaidi. Aidha, majadiliano yamefanyika kati ya wadau na makampuni ya simu za kiganjani na kuweka mikakati ya ushirikiano katika kukusanya na kusambaza taarifa za masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imekamilisha taratibu za kuanzishwa kwa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) na Mamlaka hiyo imeanza kutekeleza majukumu yake. Kurugenzi ya kushughulikia Maendeleo ya Biashara ya Ndani imeundwa na tayari imetembelea Mikoa saba na Wilaya 44 ili kubainisha bidhaa zinazozalishwa, bei, ubora, mfumo wa biashara uliopo na changamoto za biashara ya ndani na kuanza kuandaa Mkakati wa Kuboresha Soko la Ndani. Mamlaka pia, imefungua Ofisi yake huko Zanzibar. Uzinduzi rasmi wa Mamlaka hiyo ulifanyika tarehe 01 Julai, 2011.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuendeleza utekelezaji wa Mfumo wa Stakabadhi za Mazao Ghalani, Wizara kupitia Bodi ya Leseni za Maghala Tanzania imetoa Leseni kwa maghala 27 yenye daraja "A", "B" na "C" kwa ajili ya kutumia Mfumo wa Stakabadhi za Maghala kufikia msimu wa 2010/2011.

Maghala yaliyopewa leseni hizo yana ujazo wa kuanzia tani 200 hadi 60,000. Maghala hayo yapo katika maeneo mbalimbali yanayotekeleza mfumo kwa mazao ya alizeti, kahawa, korosho, mahindi, mpunga, pamba na ufuta. Aidha, kiasi cha tani 120,062 za korosho ziliuzwa kupitia mfumo huo kwa msimu wa 2010/2011 ikilinganishwa na tani 61,000 msimu wa 2007/2008. Kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Maghala, wakulima wameweza kujipatia mikopo kutoka NMB,
CRDB Bank na Kilimanjaro Cooperative Bank (KCB) kama ifuatavyo:-

Shilingi bilioni 20.66 zilitolewa na NMB msimu wa mwaka 2009/2010 na kuongezeka hadi Shilingi bilioni 42.9 msimu wa mwaka 2010/2011; CRDB Bank walitoa mikopo ya kiasi cha Shilingi billioni 45.92 mwaka 2009/2010 na kuongezeka hadi Shilingi bilioni 66.17 msimu wa mwaka 2010/2011. KCB msimu wa mwaka 2009/2010 ilitoa mikopo ya kiasi cha Shilingi bilioni 2.96 na msimu wa mwaka 2010/2011 imetoa Shilingi bilioni 2.16. Vilevile, uboreshaji wa miche ya mikorosho umeendelea kuleta tija katika uzalishaji wa zao la korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuendeleza Mfumo wa Stakabadhi za Mazao Ghalani, Wizara kupitia Mradi wa District Agriculutural Investment Project imefanya tathmini ya maghala 74 yaliyojengwa katika maeneo ya mradi huo kwa mikoa ya Kagera, Mwanza na Shinyanga na hatua inayofuata ni kuanzisha matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi kwa zao la mpunga na pamba kwa Mikoa ya Mwanza na Shinyanga pamoja na zao la kahawa kwa Mkoa wa Kagera.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuendeleza Miundombinu ya Masoko ya Mikoa na Kuanzisha Masoko Mpakani kama vile Karagwe, Kigoma, Holili, Horohoro, Namanga, Sumbawanga, Taveta na Tarakea, Wizara inaratibu uanzishwaji wa Vituo vya Pamoja vya Mpakani ili kurahisisha biashara na nchi jirani kwa kupunguza muda unaotumika kukamilisha taratibu za
kuvuka mpaka. Katika kufanikisha zoezi hilo, yafuatayo yamefanyika. Makubaliano ya ushirikiano wa kujenga Kituo cha Pamoja katika Mpaka wa Tunduma/Nakonde yamefikiwa kati ya Tanzania na Zambia. Vilevile, utafiti wa mahitaji (needs assessment) ya ujenzi wa Kituo cha Pamoja Tunduma umefanyika kwa kushirikiana na Trade Mark EA kupitia DFID. Aidha, hatua za kufanya utafiti kama huo katika kituo cha mpakani cha Kabanga zimeanza. Wizara ina mpango wa kufanya utafiti kama huo katika vituo vya mipakani vya Daraja la Umoja (Tanzania na Msumbiji), Holili (Tanzania na Kenya) na Kasumulo (Tanzania na Malawi).

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kushirikiana na Sekta Binafsi katika kubuni na kutekeleza mikakati ya masoko ya ndani, kikanda na Kitaifa, Wizara kwa kushirikiana na sekta binafsi imeanzisha Jukwaa la Wadau wa Masoko ya Mazao ya Kilimo (Agricultural Marketing Forum) kwa lengo la kuwakutanisha wadau wa kuendeleza masoko ya mazao ya kilimo. Mkutano wa Pili wa Wadau ulifanyika na kuainisha maeneo yatakayoshughulikiwa na Jukwaa hilo ikiwa ni pamoja na
uendeshaji wake. Wizara imeziwezesha na kufanya kazi kwa karibu na taasisi zifuatazo:

Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA), Tanzania Horticulture Association (TAHA), Horticultural Development Council of Tanzania (HODECT), Agricultural Council of Tanzania (ACT), Rural Livelihood Development Company (RLDC), Tanzania Agricultural Market Development Trust (TAGMARK), Bodi za Mazao na Vyama vya Ushirika. Mafanikio ya ushirikiano huo ni pamoja na kuandaliwa kwa Mkakati wa Kuendeleza Mazao ya Bustani (Horticulture Development Strategy), kuwashirikisha katika maandalizi ya Mkakati wa Masoko ya Mazao, Maandalizi ya Mkakati wa Mfumo Mpana na Unganishi wa Taarifa za Masoko na kufanya mapitio ya utekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo kwa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuimarisha udhibiti wa bidhaa duni (substandard) toka nje ya nchi, Wizara kupitia Shirika la Viwango Tanzania imeendelea kuongeza mtandao wake kwa kufungua ofisi nyingine moja ya kukagua ubora wa bidhaa zinazoingia Tanzania kupitia mpaka wa Namanga. Uanzishaji wa ofisi hiyo unafanya jumla ya ofisi za TBS kufikia tano ambazo ni Horohoro, Bandari ya Tanga, Sirari, Holili na Namanga. Kwa sasa, tathmini inafanyika kwa ajili ya kufungua Ofisi katika mipaka ya Mtambaswala, Mtukula, Rusumo na Tunduma. Aidha, Shirika liliendelea kutekeleza mfumo wa udhibiti wa ubora wa bidhaa zinazoingizwa nchini kutoka nje (batch certification). Hadi Juni, 2011, Shirika lilikwishatoa vyeti 2,123 vya ubora wa bidhaa zilizotoka nje ukilinganisha na lengo la vyeti 2,200 sawa na asilimia 97.

Katika kutekeleza mfumo huo Shirika hushirikiana kwa karibu sana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Vilevile, TBS inatarajia kuanzisha utaratibu wa kupima ubora wa bidhaa zote mahali zinakotoka kabla ya kuingiza nchini (Preshipment Verification of Conformity to Standards - PVoC).

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuwalinda wajasiriamali, Wizara kupitia Tume ya Ushindani imeendelea kufanya ukaguzi wa bidhaa bandia katika Bandari ya Dar es Salaam na Bandari Kavu (Inland Container Depots). Vilevile, Tume imeendelea kufanya ukaguzi katika maghala na maduka mbalimbali katika Mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Mbeya, Morogoro, Musoma, Mwanza, na Singida. Katika ukaguzi huo, Tume ya Ushindani ilifanikiwa kukamata na kuteketeza bidhaa zenye thamani ya Shilingi milioni 824.7 kwa kipindi cha 2010/2011. Bidhaa zilizokamatwa na kuteketezwa ni pamoja na vipuri vya magari, betri (dry cell), betri za pikipiki, vifaa vya umeme, vifaa vya muziki, redio, runinga, jenereta za umeme na kalamu. Aidha, kupitia Baraza la Ushindani, Wizara imeendelea kupokea na kuamua rufani kutokana na maamuzi ya Tume na ya Mamlaka za Udhibiti kwa wale ambao hawakuridhika na maamuzi hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utekelezaji wa mipango ya Sekta kwa mwaka 2010/2011, Wizara imeendelea na utekelezaji wa mikakati mbalimbali inayolenga kukuza, kuendeleza na kulinda viwanda vya ndani ambapo kumekuwa na mafanikio ya kuridhisha yanayoweza kupimwa kwa vigezo vya ukuaji wa Sekta ya Viwanda na mchango wake katika pato la Taifa, kuongezeka kwa uzalishaji wa bidhaa viwandani na kuongezeka kwa ajira na mauzo ya bidhaa za viwandani. Katika kipindi cha mwaka 2010, ukuaji wa Sekta ya Viwanda uliendelea kuwa chanya ambapo ulifikia asilimia 7.9.

Ukuaji huo umepungua kidogo kwa asilimia 0.1 kutoka asilimia 8.0 mwaka 2009 hali
iliyochangiwa kwa kiasi kikubwa na tatizo la mdororo wa uchumi ulioikumba dunia mwaka 2008 na kufikia kilele mwaka 2009. Aidha, mchango wa Sekta ya Viwanda katika pato la Taifa nao uliongezeka kutoka asilimia 8.6 mwaka 2009 na kufikia asilimia 9.0 mwaka 2010. Ongezeko hilo limetokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa baadhi ya bidhaa za viwandani. Hata hivyo, kasi ya ukuaji na mchango wa Sekta ya Viwanda kwa pato la Taifa haukuongezeka kama ilivyotarajiwa, kutokana na athari za mgao wa umeme ambao ulisababisha kupanda kwa gharama za uzalishaji na hivyo baadhi ya viwanda kusimamisha au kupunguza uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda ambavyo uzalishaji uliongezeka katika kipindi cha mwaka 2010 ni pamoja na uzalishaji wa unga wa ngano ulioongezeka kutoka tani 368,885 mwaka 2009 na kufikia tani 388,905 mwaka 2010, ambalo ni ongezeko la asilimia 5.4. Uzalishaji wa konyagi uliongezeka kutoka lita 10,201,000 mwaka 2009 hadi kufikia lita 12,972,843 mwaka 2010 sawa na ongezeko la asilimia 27.2, pombe ya kibuku uliongezeka kutoka lita 16,141,000 mwaka 2009 hadi kufikia lita 20,753,530 mwaka 2010 sawa na ongezeko la asilimia 28.6, uzalishaji wa bia uliongezeka kutoka hektolita milioni 2.84 mwaka 2009 hadi kufikia hektolita milioni 5.15 mwaka 2010 sawa na ongezeko la asilimia 81.3.

Aidha, uzalishaji wa mabati uliongezeka kutoka tani 50,664 mwaka 2009 na kufikia tani 66,231 mwaka 2010 sawa na ongezeko la asilimia 30.7, uzalishaji wa betri uliongezeka kutoka betri milioni 78 mwaka 2009 hadi kufikia betri milioni 93 mwaka 2010 sawa na ongezeko la asilimia 19.2 ambapo uzalishaji wa sigara uliongezeka kutoka sigara bilioni 5,831 mwaka 2009 hadi bilioni 6,170 mwaka 2010 sawa na ongezeko la asilimia 5.8. Vilevile, uzalishaji wa chuma uliongezeka kutoka tani 34,793 mwaka 2009 hadi tani 43,882 mwaka 2010 sawa na ongezeko la asilimia 26.1.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalishaji wa saruji uliongezeka kutoka tani 1,940,845 mwaka 2009 hadi tani 2,312,055 mwaka 2010, sawa na ongezeko la asilimia 19.1. Uzalishaji huo uliongezeka kwa kiasi kikubwa kutokana na upanuzi wa viwanda vyote vitatu vya saruji nchini na kuongezeka kwa mahitaji ya saruji katika Sekta ya Ujenzi. Kiwanda cha Tanzania Portland Cement Co. Ltd kimeongeza uwezo wa uzalishaji kutoka tani 700,000 hadi 1,400,000; Tanga Cement Co. Ltd kutoka tani 500,000 hadi 1,200,000; na Mbeya Cement Co. Ltd kutoka tani 250,000 hadi 350,000. Kwa ujumla, hadi kufikia mwaka 2010 uwezo wa uzalishaji (installed capacity) wa saruji kwa viwanda vyote vitatu uliongezeka kwa asilimia 102.8.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka 2010, Sekta ya Nguo na Mavazi imeendelea kuimarika kutokana na matumizi ya teknolojia ya kisasa pamoja na uongezaji wa mitaji kwa Viwanda kama vile Polytex (21st Century), Sunguratex (NAMERA Group), Mwatex, NIDA, Kiwanda cha A - Z (Arusha) cha kuzalisha vyandarua na Mazava Fabrics Production Ltd. (Morogoro) cha kuzalisha mavazi yanayouzwa zaidi Soko la AGOA. Kwa ujumla Sekta ya Nguo na Mavazi imekuwa na ongezeko la uzalishaji kufikia mita za mraba 120,000,000 mwaka 2010 ikilinganishwa na mita za mraba 91,501,000 zilizozalishwa mwaka 2009. Ongezeko hilo ni sawa na
asilimia 31.1

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba hali ya sekta ya Viwanda vya Kusindika Ngozi na bidhaa za ngozi inaendelea kuimarika, tathmini iliyofanyika inaonyesha kwamba uwezo uliosimikwa (installed capacity) wa viwanda vyote nane vya usindikaji ngozi nchini ni futi za mraba milioni 73.9 wakati uwezo halisi uliotumika (capacity utilization) kwa mwaka 2010 ni futi za mraba milioni 39.7 ikilinganishwa na futi za mraba milioni 37.3 mwaka 2009. Kushuka huko kulitokana na changamoto mbalimbali zilizoikumba Sekta ya Viwanda vya ngozi ikiwepo ya mdororo wa uchumi ulioikumba dunia.

Aidha, kwa upande wa ngozi zilizosindikwa kwa kiwango cha wet-blue mauzo yake nje ya nchi yalipungua kutoka tani 5,831 mwaka 2009 hadi tani 5,504 mwaka 2010 (sawa na upungufu wa asilimia 5.6). Hata hivyo, thamani ya mauzo ya ngozi hizo zilizosindikwa yaliongezeka kutoka Shilingi bilioni 6.8 mwaka 2009 hadi Shilingi bilioni 8.4 mwaka 2010 (sawa na ongezeko la asilimia 23.5). Ongezeko hili lilisababishwa na kupanda kwa bei za ngozi zilizosindikwa katika soko la nje mwaka 2010. Aidha, baadhi ya viwanda vimeanza kusindika ngozi hadi kiwango cha kati (crust
leather) na cha mwisho (finished leather) kwa ajili ya kutengeneza bidhaa za ngozi hapa nchini.

Viwanda vya bidhaa za ngozi navyo vimeendelea kuimarika kutokana na juhudi mbalimbali
zinazochukuliwa ikiwemo mafunzo ya usindikaji na utengenezaji wa bidhaa za ngozi kwa vikundi vya wajasiriamali nchini. Ajira kwenye Sekta ya Ngozi imeongezeka kutoka wafanyakazi 520 mwaka 2009 hadi wafanyakazi 1,150 mwaka 2010.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkutano wa kuhamasisha uwekezaji wa viwanda ndani ya nchi kwa kuwashirikisha wawekezaji na wajasiriamali wa Kitanzania ulifanyika mwezi Machi, 2011, ambapo baadhi ya Watanzania wameonesha nia ya kuanzisha viwanda. Mfano, Kampuni ya Yuko's General Supplies Ltd (Kiluvya, Kibaha) inatarajia kuanzisha kiwanda cha kutengeneza viatu, Kampuni ya Covenant Investment Agency inatarajia kuanzisha kiwanda cha kusindika ngozi Dar es salaam, Kampuni ya Tanmbuzi Co. Ltd inatarajia kuanzisha Kiwanda cha Usindikaji wa ngozi Mkoani Kilimanjaro na Afro Star (T) Ltd inatarajia kuanzisha pia kiwanda cha usindikaji wa ngozi. Wizara itafuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi hiyo ili kuhakikisha inakamilika na kuwezesha usindikaji wa ngozi zote zinazokusanywa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inakamilisha Programu Maalumu ya Uanzishwaji na Uendelezaji wa Maeneo Maalumu ya viwanda kama mpango mmojawapo wa kuhamasisha na kuchochea uwekezaji wa viwanda vya usindikaji na utengenezaji wa bidhaa za ngozi nchini. Maeneo hayo yatajulikana kama Vijiji vya Viwanda kwa ajili ya kuwavutia wawekezaji wa viwanda vidogo na vikubwa. Programu hii kwa mapana yake ina
mikakati mitatu ambayo ni:
(i) Mkakati wa Kuanzisha na Kuendeleza Vijiji vya Viwanda kama maeneo maalumu kwa ajili ya kuhamasisha na kuchochea uwekezaji wa viwanda vya bidhaa za ngozi na
usindikaji wa ngozi nchini;

(ii) Mkakati wa Kuendelea Kuimarisha na kujenga Uwezo wa Kisekta na wa kiushindani
katika soko; na

(iii) Mkakati wa Kuwezesha Sekta Kuyafikia na Kuyakuza Masoko ya Bidhaa za Ngozi zinazotengenezwa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalishaji katika kiwanda cha General Tyre (EA) Ltd (GTEA)

ulisimama mwezi Septemba, 2007 kutokana na ukosefu wa fedha za uendeshaji. Serikali imeendelea kufanya majadiliano na mbia mwenza, kampuni ya Continental AG tangu mwishoni mwa mwaka 2008 na hadi sasa majadiliano hayo hayajahitimishwa kutokana na masharti magumu yaliyowekwa na mbia mwenza.

Masharti hayo ni pamoja na kuitaka GTEA kuuza matairi yatakayozalishwa nchini Tanzania katika nchi za Uganda na Burundi pekee; Continental AG kutowekeza ndani ya GTEA kwa vile siyo shughuli ya msingi ya Continental AG na deni la Continental AG la USD milioni 3.321 linalodaiwa GTEA kulipwa kabla ya kufikia muafaka wa kutumia alama yake ya biashara ya General. Kutokana na msimamo wa Continental AG, na kwa kuzingatia umuhimu wa kiwanda hiki katika uchumi wa Taifa, Serikali imekusudia kukabidhi kiwanda hiki NDC ili iweze kutafuta mwekezaji mahiri ili kiwanda kifufuliwe kwa kutumia malighafi ya mpira unaozalishwa hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia NDC imeendelea kuweka msukumo katika kuhamasisha uwekezaji ambapo wawekezaji wameendelea kujitokeza kwa miradi mbalimbali chini ya NDC. Miradi hiyo ni pamoja na makaa ya mawe ya Mchuchuma, Chuma cha Liganga na mradi wa magadi (soda ash) wa Ziwa Natron; na miradi mingine ikiwemo uanzishaji wa kiwanda cha mbolea Mtwara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa kuzalisha chuma ghafi (sponge iron) unaofahamika kwa jina la "Kasi Mpya" utatumia madini ya chuma ya Maganga Matitu (sehemu ya Liganga) na makaa ya mawe ya Katewaka (karibu na Mchuchuma) katika Wilaya ya Ludewa.

Mradi huo unatarajiwa kuzalisha chuma ghafi tani 330,000 kwa mwaka ambacho
kitatumika kuzalisha chuma cha pua (steel billet) tani 250,000 kwa mwaka na umeme (captive power) wa MW 25. Mradi huo unatekelezwa na Kampuni ya Maganga Matitu Resources Development Limited (MMRDL) ambayo ni kampuni ya ubia kati ya NDC kwa niaba ya Serikali ambayo inamiliki hisa asilimia 25 na mwekezaji, Kampuni ya MM Steel Resources Public Limited Company inayomiliki hisa asilimia 75. Kwa sasa Kampuni hiyo inakamilisha uchorongaji ili kubaini ubora na uwingi wa chuma na makaa ya mawe katika eneo la mradi na zoezi linatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba 2011. Ujenzi wa mgodi wa chuma, mgodi wa makaa ya mawe na kiwanda cha kuzalisha sponge iron unatarajiwa kuanza mwaka 2012.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Viwanda na Biashara imepewa jukumu la kutekeleza nguzo namba saba ya azma ya Kilimo Kwanza ambapo Sekta ya Viwanda inapaswa kuwa kichocheo cha kuleta Mapinduzi ya Kijani hapa nchini.

Malengo makuu ya nguzo hiyo ni kuendeleza viwanda vya usindikaji ili kuongeza thamani mazao ya kilimo na mifugo na kuhakikisha upatikanaji wa zana na pembejeo za kilimo. Ili kutekeleza azma hiyo, katika mwaka 2010, Wizara iliendelea kuhamasisha uanzishaji wa viwanda vinavyohusika na usindikaji na utengenezaji wa pembejeo na zana za kilimo. Aidha, kupitia Mamlaka ya EPZ viwanda vinane vya kusindika mazao na kutengeneza vifungashio vya mazao vimepewa leseni wakati viwanda 20 vya usindikaji mazao na vitano vya kutengeneza pembejeo na zana za kilimo vilionyesha nia ya kuwekeza kupitia TIC katika mwaka 2010. Kwa ujumla wawekezaji 168 walionyesha nia ya kuwekeza katika uanzishaji viwanda ambapo 18 vipo chini ya EPZA na 150 chini ya TIC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kwa kushirikiana na wadau imeandaa Mkakati Unganishi wa kuendeleza Sekta ya Viwanda na inakamilisha Mpango Kamambe wa kutekeleza Mkakati huo. Mpango Kamambe huo umebainisha programu na miradi mbalimbali itakayotekelezwa ikiwa ni pamoja na ujenzi wa uwezo wa Wizara, uimarishaji wa miundombinu, uendelezaji wa sekta za kipaumbele hususan usindikaji wa mazao, uendelezaji wa sekta binafsi, uhaulishaji wa teknolojia, upatikanaji wa mitaji na uimarishaji wa masoko. Utekelezaji wa Mkakati huo unakwenda sambamba na juhudi za kuanzisha viwanda vya kipaumbele vya mbolea na saruji katika mwambao wa pwani ya Mtwara, uendelezaji wa SEZ katika pwani ya Bagamoyo na uendelezaji wa miradi ya Mchuchuma na Liganga ili kujenga viwanda vya msingi kwa maendeleo ya Sekta ya Viwanda na sekta nyingine za uzalishaji.

Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Tanzania Gatsby Trust (TGT) inaandaa mkakati wa sekta ndogo ya nguo na mavazi kama moja ya sekta za kipaumbele. Lengo ni kuhakikisha viwanda vya ndani vya nguo vinasindika angalau asilimia 70 ya pamba inayozalishwa hapa nchini kutoka asilimia 30 ya sasa. Azma ya Wizara ni kuhakikisha nguo zinazalishwa na mavazi kushonwa kwa ajili ya soko la ndani na la nje hususan soko la AGOA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na juhudi za muda mrefu zilizofanywa na Wizara kupitia NDC za kuvutia wawekezaji katika miradi ya makaa ya mawe ya Mchuchuma na chuma cha Liganga, mwekezaji katika miradi hii alipatikana mwezi Januari, 2011, ambaye ni Kampuni ya Sichuan Hongda Corporation Limited ya China na majadiliano ya mkataba wa ubia yanaendelea. Mradi wa makaa ya mawe wa Mchuchuma unahusisha uzalishaji wa umeme wa MW 600 kwa ajili ya uchenjuaji na uyeyushaji wa madini ya chuma na chuma ghafi na bakaa kuingizwa kwenye gridi ya Taifa. Tani milioni moja za chuma ghafi zitazalishwa kwa mwaka kiasi ambacho kitatumika kuzalisha bidhaa mbalimbali za chuma (iron and steel products) nchini. Katika uzalishaji huo, yatapatikana pia madini adimu ya Vanadium na Titanium ambayo yana thamani kubwa zaidi kuliko chuma chenyewe. Kwa mfano, kiasi cha mashapo kinachotoa tani moja ya chuma inayouzwa katika soko la dunia kwa Dola za Kimarekani 600, pia kinatoa madini hayo ya vanadium na titanium yenye thamani ya Dola za Kimarekani 882.

Utekelezaji wa miradi hii ambao utakwenda sambamba na uhakiki wa makaa ya mawe, uchorongaji na upembuzi yakinifu kwa mradi wa chuma unatarajiwa kuanza mwaka 2011/2012 baada ya majadiliano ya mkataba wa ubia kukamilishwa na mkataba kusainiwa. Mwekezaji huyo atawekeza kiasi cha Dola za Kimarekani bilioni tatu kwa ajili ya kutekeleza miradi ya chuma na
makaa ya mawe kwa mfumo unganishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa Magadi (Soda Ash) wa Ziwa Natron unatarajiwa kuzalisha tani 500,000 za Magadi kwa mwaka. NDC inaendelea kukamilisha tafiti za ziada za kisayansi kuhusu Kemia, Haidrolojia, Ekolojia na Hydrodyanamics ya Ziwa Natron, baada ya wadau kuonyesha wasiwasi juu ya utafiti wa athari za mradi katika mazingira na jamii ambao ulikwishakamilika. Aidha, utafiti kuhusu upatikanaji wa magadi katika eneo mbadala mbali na Ziwa huko Engaruka Wilayani Monduli, unaendelea. Utekelezaji wa mradi huo utahitaji uboreshaji wa miundombinu ya reli kati ya Tanga na Arusha, ujenzi wa reli mpya kati ya Arusha na Ziwa Natron (km 132) na upanuzi wa Bandari ya Tanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya Kange, Tanga na TAMCO, Kibaha yanafanyiwa Cadastral Survey ili kuonyesha mipaka ya viwanja, miundombinu, na kadhalika na hivyo kuvutia wawekezaji kwa ajili ya ujenzi wa viwanda mbalimbali. Kazi hiyo inatarajiwa kukamilika katikati ya mwezi Agosti, 2011 kwa upande wa eneo la Kange wakati kwa upande wa TAMCO zoezi lilikwishakamilishwa ambapo usanifu wa miundombinu hususan barabara na mfumo wa maji safi na taka vinatarajiwa kukamilika mwezi Septemba, 2011 ili kutoa nafasi kwa wawekezaji waliokwishawasilisha maombi yao NDC kujenga viwanda. Viwanda vinavyotarajiwa kuanzishwa ni vya magari, kuongeza thamani mazao ya kilimo na vya nguo. Vilevile, eneo la Kilimanjaro Machine Tools lililoko Wilaya ya Hai lilipata mwekezaji isipokuwa kutokana na mdororo wa uchumi kasi yake ya kuanza shughuli za uzalishaji ilipungua na bado hajaanza hadi sasa. Kutokana na kuchelewa huko, NDC tayari imekwishampa notisi ya kutengua mkataba ili kuachana naye na kuanza utaratibu wa kumpata mwekezaji mwingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia NDC inaendelea na mazungumzo na mwekezaji aliyebainishwa ili kuanzisha mradi wa kilimo cha mashamba makubwa ya mtama mtamu katika Wilaya ya Kisarawe, Mkoa wa Pwani kwa ajili ya kuzalisha malighafi ya kuzalisha ethanol na nishati kutokana na mabua ya mtama huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia NDC imeendelea kuibua na kunadi fursa za uwekezaji katika kanda za maendeleo za Mtwara na Kati, kwa mfano, uendelezaji wa uongezaji thamani mkaa wa mawe na madini ya chuma katika ukanda wa Mtwara na madini ya nickel katika ukanda wa Kati. NDC inajishughulisha pia na mikakati ya utekelezaji wa miradi mihimili katika ukanda wa Kati. Aidha, NDC imeendelea kunadi heavy capacity ferry na Bandari ya Mtwara kwa uendelezaji na upanuaji kwa ajili ya kuibua fursa nyingine katika ukanda wa maendeleo wa Mtwara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa kuzalisha umeme wa MW 50 hadi 300 kwa kutumia nguvu ya upepo huko Singida (Singida Wind Power Project-SWPP) unatekelezwa kwa ubia kati ya NDC na Kampuni ya Power Pool East Africa Ltd (PPEAL). Upembuzi yakinifu wa mradi umekamilika na Serikali imewasilisha maombi ya awali ya mkopo nafuu (preferential loan) katika Benki ya Exim ya China na mazungumzo yanaendelea. Mradi huu unategemewa kuanza kutekelezwa mwishoni mwa mwaka 2011.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia NDC iko katika hatua za mwisho za kupata kibali kutoka Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) cha kutekeleza mradi wa kusafisha dhahabu kwa njia ya kikemia baada ya kufanya utafiti wa athari ya mradi katika mazingira na jamii (ESIA). Aidha, tafiti za njia bora ya usafishaji wa dhahabu kwa kutumia kemikali uko katika hatua ya mwisho ya kukamilisha michoro ya mitambo ya kusafishia dhahabu hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, NDC imeingia ubia na Kampuni ya Pacific Corporation East Africa (PCEA) na kuunda Kampuni ya ubia ya TANCOAL Energy Ltd kwa ajili ya kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe ya Mbalawala na Mhukuru huko Mbinga. Kampuni hiyo inamilikiwa na NDC kwa asilimia 30 na PCEA kwa asilimia 70. Mradi huu unahusu uchimbaji wa makaa ya mawe kwa ajili ya matumizi ya viwandani na uzalishaji wa umeme kwa kuanzia na MW 400 kwa ajili ya kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa. Uzalishaji wa makaa ya mawe kwa ajili ya viwanda utaanza mwishoni mwaka 2011, ambapo ujenzi wa kituo na kuzalisha umeme utaanza mwaka 2014/2015.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia NDC pia inasimamia ujenzi wa kiwanda cha
kutengeneza dawa za kibaiolojia za kuua viluilui vya mbu wanaoeneza malaria kwa kutumia teknolojia kutoka Cuba. Kiwanda hicho kitakachozalisha lita milioni sita za dawa kwa mwaka kinajengwa katika eneo la Viwanda la TAMCO-Kibaha, Mkoani Pwani. Ujenzi wa Kiwanda husika hadi kukamilika utagharimu Dola za Kimarekani milioni 22.3, katika fedha za kigeni na Shilingi bilioni tano katika fedha za Kitanzania, ambapo asilimia 75 ya fedha za kigeni imeshalipwa. Maandalizi ya ujenzi wa kiwanda yamekamilika na ujenzi umeanza mwezi Juni, 2011 na utakamilika Julai, 2012.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uanzishwaji wa Viwanda vipya na uendelezaji wa Viwanda katika maeneo ya EPZ na SEZ kwa kiasi kikubwa vimechangia ongezeko la ajira katika Sekta ya Viwanda. Kwa mfano, katika maeneo ya EPZ ajira iliongezeka kutoka wafanyakazi 9,300 mwaka 2009 hadi wafanyakazi 13,000 mwaka 2010, sawa na ongezeko la asilimia 30. Kwa ujumla, idadi ya wafanyakazi walioajiriwa katika viwanda vikubwa na vya kati walikuwa 107,267 mwaka 2009 na kuongezeka hadi wafanyakazi 108,340 mwaka 2010. Katika ajira hizo, viwanda vilivyoongoza ni vya kusindika mazao ya chakula (44,365); ufumaji na ushonaji (11,988); na tumbaku na sigara (6,883).

Mheshimiwa Mwenyekiti, mamlaka ya EPZ imekamilisha zoezi la kubainisha maeneo ya EPZ na SEZ katika Mikoa. Mikoa iliyotoa maeneo ni Arusha hekta (1600); Iringa (hekta 200); Kagera (hekta 2600); Kigoma (hekta 3000); Kilimanjaro (hekta 463); Lindi (hekta 100); Manyara (hekta 530.87); Mara (hekta 1360); Mbeya (hekta 500); Mtwara (hekta 2600); Mwanza (hekta 3500); Morogoro (hekta 2000); Pwani (hekta 9081); Ruvuma (hekta 2033); Shinyanga (hekta 1040); Singida (hekta 2000) na Tanga (hekta 1363). Maeneo haya yataendelezwa kwa awamu na kwa kushirikisha sekta binafsi. Juhudi za kupata maeneo katika Mikoa ya Tabora, Dodoma na Rukwa zinaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mamlaka ya EPZ ipo katika hatua za mwisho za kuanzisha Kituo cha Utoaji Huduma (One Stop Services Centre) katika eneo la Benjamini William Mkapa Special Economic Zone. Tayari mawasiliano na taasisi, wadau zikiwemo TRA, NEMC na Uhamiaji yamefanyika ili kuipatia EPZA maofisa watakaotoa huduma katika kituo hicho. Aidha, majengo ya kituo hicho yamekamilika na tayari yamewekwa samani, na kuunganishwa na mfumo kasi wa mtandao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi Julai 2010 Baraza la Mawaziri lilitoa maamuzi ya kufanyia Sheria za EPZ na SEZ marekebisho ili kuiwezesha Mamlaka ya EPZ chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara kusimamia pia mfumo wa SEZ ambao hapo awali ulikuwa unasimamiwa na iliyokuwa Wizara ya Mipango na Ubinafsishaji. Urekebishaji wa Sheria hizo mbili ulipitishwa na Bunge lako Tukufu mwezi Aprili, 2011 na Kanuni za Sheria ya SEZ zinaandaliwa. Kukamilika kwa Kanuni za Sheria ya SEZ kutatoa fursa ya kuanza kutumika kwa mfumo wa SEZ na hivyo kuvutia wawekezaji wengi zaidi katika eneo la SEZ.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la SEZ la Bagamoyo lenye ukubwa wa hekta 9,081 litaendelezwa kwa mfumo wa satellite town na utakaohusisha pia uendelezaji wa Bandari ya Mbegani na ujenzi wa uwanja wa Ndege katika kijiji cha Zinga. Hatua zilizofikiwa katika
kuendeleza eneo hili ni kama ifuatavyo:

(a) Zoezi la uainishaji mipaka, upimaji na upigaji wa picha za anga tayari limekamilika;

(b) Eneo la Bagamoyo SEZ tayari limetangazwa katika government gazette kama eneo
maalum la mradi;

(c) Upembuzi yakinifu umekamilika;

(d) Uthamanishaji wa maeneo ya mashamba makubwa ya Pimbini, Kitopeni, Kidagoni na
Mareale umekamilika;

(e) Uthamanishaji wa maeneo mengine ya wananchi upo katika hatua za mwisho
(wataalamu wa Wizara ya Ardhi wanamalizia uthamanishaji wa sehemu iliyobaki); na

(f) Pamoja na juhudi za kutafuta Shilingi bilioni 53 za fidia ya eneo zima ambazo zimekuwa
zikiendelea, ufumbuzi bado haujapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kushirikiana na Benki ya Dunia, Mamlaka ya EPZ inaendelea
na taratibu za kuandaa Mpango Kamambe ya eneo zima. Baada ya kuandaliwa kwa Mpango Kamambe, wawekezaji binafsi na Mifuko ya Pensheni itahamasishwa kukodisha vitalu katika eneo hilo na kujenga miundombinu ya uzalishaji. Aidha, tayari makampuni manne (4) yameonesha nia ya kuendeleza miundombinu ya viwanda katika eneo hilo. Makampuni hayo ni Turkuaz Ltd kutoka Uturuki; Blue Rock Ltd kutoka Marekani; Kamal Group Ltd kutoka India na Industrial Park Ltd ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, Wizara kupitia Mamlaka ya EPZ imeendelea kuhamasisha wawekezaji wa kujenga miundombinu na viwanda vya uzalishaji katika maeneo ya EPZ.

Kutokana na uhamasishaji huu makampuni ya Kamal Group (Zinga, Bagamoyo), Global Industrial Park (Mkuranga, Pwani) na Rusumo Falls SEZ (Kagera) yamepewa leseni za kujenga miundombinu ya msingi katika maeneo mapya ya uwekezaji ambayo yameanza kuvutia viwanda vya uzalishaji.

Aidha, Kiwanda cha Mazava Fabrics and Production E.A Ltd kimeongeza uzalishaji wa nguo katika eneo la EPZ Msamvu Mkoani Morogoro. Kiwanda hiki kinatengeneza nguo za michezo aina ya Alleson, Puma, Adidas na kadhalika kwa ajili ya soko la AGOA na Ulaya na kimeajiri wafanyakazi 1,500. Idadi hii inatarajia kufikia wafanyakazi 2,500 ifikapo mwezi Septemba, 2011 na itaongezeka kufikia 5,000 ifikapo mwishoni mwa mwaka 2012.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyoelezwa hapo awali katika mwaka wa fedha 2010/2011 Mamlaka ya EPZ ilikamilisha ujenzi wa eneo maalumu la uwekezaji la Benjamin William Mkapa Special Economic Zone (BWM-SEZ). Jumla ya wawekezaji 14 wamepewa viwanja vya kujenga viwanda katika eneo hilo ambapo kwa sasa viwanja vyote vilivyotengwa vimetolewa kwa wawekezaji.

Wawekezaji waliojenga viwanda katika eneo hilo ni Tembo Agro Ltd (Oman); Harvest Africa Ltd (Tanzania); The Great Export Co. Ltd (Tanzania); Paperkraft International Ltd (Tanzania); Labotrix Group (T) Ltd (China); Quality Pulse Exporters Ltd (India); Steel One Ltd (Tanzania); Konectt Industries Ltd (India); Rising Electronics Ltd (Tanzania); DZ Card Africa Ltd (Thailand); Somani Agro Exports Ltd (Tanzania na Uingereza); Tube LTD (Tanzania na China); Kastan Industries Ltd (Korea na Marekani); Rehmat Beverages and Food (Tz) Ltd (Oman).

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kwa kupitia Mamlaka ya EPZ iliendelea na uhamasishaji wa uwekezaji katika Maeneo Maalumu ya uwekezaji ya EPZ na SEZ kwa kutumia njia mbalimbali kama vipeperushi, mabango, majarida, tovuti ya Mamlaka na matangazo kwenye vyombo mbalimbali vya habari (magazeti, luninga, radio n.k) na kwa njia ya kushiriki katika maonyesho na makongamano ya kibiashara yanayofanyika ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuvutia wawekezaji wengi.

Aidha, Mamlaka ya EPZ imekuwa inatoa mada kuhusu umuhimu na fursa zilizoko chini ya EPZ na SEZ kwa wajumbe wa Halmashauri na Mabaraza ya Madiwani katika Wilaya za Bagamoyo, Kigoma, Manyara na Meru kuchangamkia fursa hizo. Kutokana na uhamasishaji huu, idadi ya wawekezaji imeongezeka kutoka 18 mwaka 2008 hadi 44 mwaka huu ambapo mtaji umefikia Dola za Kimarekani milioni 650 na yameuza nje bidhaa zenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 350 na kutoa ajira za moja kwa moja 13,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo. Wizara imekuwa ikitekeleza mipango na mikakati mbalimbali ikiwa na lengo la kuindeleza Sekta. Katika utekelezaji huo, Wizara imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuongeza uwezo wa SIDO
katika uwezeshaji wa kitaalamu na mitaji, kuboresha huduma za ugani na ushauri.

Mheshijmiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha kuwa ushirikishwaji wa wananchi unakuwepo, Wizara kwa kushirikiana na Manispaa na Halmashauri mbalimbali imekuwa ikianisha na kutenga maeneo kwa ajili ya wajasiriamali wadogo na wa kati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuimarisha ajira na kuongeza kipato kwa wajasiriamali vijijini, Wizara kupitia SIDO iliendelea kupeleka miradi mbalimbali ya uzalishaji mali vijijini. Katika mwaka 2010/2011, miradi mipya 237 ilianzishwa na kufikia miradi 2,743 kutoka miradi 2,506 mwaka 2009 hili ni ongezeko la asilimia 9.5. Huduma za ugani na ushauri ziliongezeka kutoka wajasiriamali 47,356 mwaka 2009 hadi kufikia wajasiriamali 55,356 mwaka 2010/2011 sawa na ongezeko la asilimia 16.9.

Aidha, huduma za mafunzo mbalimbali za wajasiriamali na biashara ziliongezeka kutoka wajasiriamali 28,619 mwaka 2009 na kufikia wajasiriamali 38,583 mwaka 2010/2011, sawa na ongezeko la asilimia 34.8. Mafunzo mengine yalitolewa kwa wahunzi ambapo idadi iliongezeka kutoka 6,519 mwaka 2009 na kufikia wahunzi 7,039 mwaka 2010/2011, sawa na ongezeko la
asilimia 8.0.

Mheshimiwa Mwenyekiti, idadi ya wajasiriamali walioshiriki kwenye maonesho mbalimbali nje na ndani ya nchi iliendelea kuongezeka kwa asilimia 18.4 kutoka 8,254 mwaka 2009 na kufikia 9,772 mwaka 2010/2011. Aidha, washiriki kwenye maonesho hayo waliweza kuuza bidhaa zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 480. Upatikanaji wa mitaji pia uliongezeka, kufikia shilingi bilioni 5.026 mwaka 2010/2011.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imekuwa ikitekeleza programu na mikakati mbalimbali kwa lengo la kuiendeleza sekta hii. Hii ni pamoja na utekelezaji wa programu ya Muunganisho Ujasiriamali Vijijini (MUVI), mkakati wa Wilaya moja bidhaa moja (ODOP), programu ya usindikaji wa vyakula inayofadhiliwa na Serikali ya Korea ya Kusini na mikataba kati ya SIDO na Shirika la Viwanda Vidogo India ambao utekelezaji wake utajikita kwenye teknolojia ya habari pamoja na
uimarishaji wa viatamizi vya biashara na teknolojia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imefanya jitihada mbalimbali za kuongeza uwezo wa SIDO katika uwezeshaji wa kitaalamu na mitaji. Juhudi hizo ni pamoja na uanzishwaji wa Mfuko wa Kitaifa wa Kuwaendeleza Wajasiriamali Wadogo (NEDF) mwaka 1994. Toka mfuko ulipoanzishwa hadi kufikia mwezi Machi, 2011 Serikali ilikwishawekeza jumla ya shilingi bilioni 4.8.

Aidha, mfuko ulikuwa umepokea jumla ya maombi 145,435 yenye thamani ya shilingi bilioni 75 ambapo jumla ya maombi 51,019 yenye thamani ya shilingi bilioni 26 yaliidhinishwa na kuwezesha upatikanaji wa ajira 153,185. Kiasi hicho ni kikubwa kuliko fedha zilizokwishawekezwa
na Serikali kwa sababu mfuko huo unaendeshwa kwa mfumo wa mzunguko (revolving).

Katika mwaka 2010/2011, jumla ya wajasiriamali 5,976 walipewa mikopo ya thamani ya shillingi billioni 5.26 na mikopo hiyo iliwezesha kupata ajira za watu 6,458. Katika mikopo hiyo, asilimia 42 ilitolewa kwa wanawake ambao wengi wapo vijijini. Katika kipindi hicho marejesho yalikuwa ni asilimia 91.4. Kwa ujumla mfuko huu umesaidia kuboresha vipato kwa wananchi na
kuchochea ujasiriamali mijini na vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, Wizara imekamilisha zoezi la ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa za sekta ya viwanda vidogo na biashara ndogo. Taarifa kamili imekamilika na inatarajiwa kuzinduliwa mwezi Septemba, 2011 kwa ajili ya kutumiwa na wadau mbalimbali. Aidha, Serikali kupitia SIDO imeendelea kutoa huduma za ushauri na ugani ambapo jumla ya wajasiriamali 20,755 walipata huduma za ushauri katika maeneo mbalimbali yanayohusiana na uendelezaji wa biashara na shughuli za uzalishaji. Aidha, SIDO imeendelea kutoa huduma za ugani zikilenga maeneo mbalimbali ya kiufundi ambapo zilitolewa huduma katika viwanda vidogo 1,247 katika wilaya mbalimbali hapa nchini na kati ya hivyo 237 vilikuwa
viwanda vipya. Hili ni ongezeko la asilimia 19.

Mheshimiwa Mwenyekiti, SIDO imeweza kuhamasisha mafundi wadogo kuhudhuria
mafunzo ya usindikaji na utengenezaji wa bidhaa za ngozi na kuwezesha kozi 20 kuendeshwa katika mikoa 15 nchini. Kozi zilizoendeshwa ziliwashirikisha wajasiriamali 336 ambapo 117 sawa na asilimia 35 walikuwa wanawake. Mafunzo haya yamewezesha miradi 102 kuanzishwa ambapo 70
ni ya utengenezaji wa bidhaa za ngozi na 32 ya usindikaji ngozi.

Aidha, kozi 11 za usindikaji wa vyakula zimeendeshwa kwa wajasiriamali 198 katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Kilimanjaro, Mbeya, Pwani, Rukwa, Shinyanga, Mtwara na Mwanza. Pia, kozi moja ya wataalamu elekezi 21 imeendeshwa ili kuweza kutoa fursa kwa wasindikaji kupata mwongozo wa usindikaji kupitia wataalamu hawa. Aidha, mashine na vifaa vya usindikaji wa vyakula zilizopokelewa kutoka Korea Kusini zitawezesha vituo vya mafunzo ya usindikaji vyakula
vya Dar es Salaam na Morogoro kuwa na uwezo mzuri wa kutoa mafunzo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa uanzishwaji na uendelezaji wa viwanda vidogo umewezesha uanzishaji wa viwanda vipya 237 vijijini na kutengeneza ajira mpya 5,089 katika mwaka 2010/2011. Asilimia 86 ya viwanda vilivyopata huduma hiyo ni vya usindikaji wa vyakula vya aina mbalimbali. Aidha, majengo kumi yamekarabatiwa katika mikoa ya Arusha, Iringa, Kilimanjaro, Kigoma, Mbeya, Shinyanga na Tanga. Vilevile, wajasiriamali wabunifu 37 wamepata nafasi katika majengo yaliyoandaliwa chini ya mradi wa kiatamizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, jumla ya majengo 87 yenye nafasi ya kutosha miradi midogo 520 yamejengwa kwa ushirikiano na sekta binafsi. Uendelezaji huo umefanyika katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Kilimanjaro, Mara, Mbeya,
Morogoro, Mtwara, Mwanza, Rukwa, Ruvuma, Shinyanga, Tabora na Tanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhamasisha na kuwawezesha wajasiriamali wadogo kuweza kuyafikia masoko ya ndani na nje ya nchi, Serikali imekuwa ikiboresha vituo vyake vya kusambaza habari kwa ajili ya kuyajua masoko na sehemu muhimu za kufanyia biashara. Katika mwaka wa fedha wa 2010/2011, Wizara kupitia SIDO imeweza kufanya ukarabati wa majengo na manunuzi ya vifaa kwa ajili ya vituo vya habari 15 katika mikoa mbalimbali hapa nchini ili kurahisisha
upatikanaji wa habari za kimasoko na biashara za ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imeendelea kutoa vipaumbele vya pekee katika maonesho ya bidhaa mbalimbali zawa jasiriamali wadogo katika maonesho ya Kitaifa na Kimataifa ili kuweza kuwapa fursa ya kujifunza na kuuza bidhaa na huduma wanazozalisha. Katika mwaka 2010/2011, Wizara kupitia SIDO imewezesha kufanyika kwa maonesho matano ya kikanda ya bidhaa za wajasiriamali wadogo. Kanda hizo ni Kanda ya Mashariki, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Kati, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Kusini. Aidha, jumla ya wajasiriamali 1,214 walishiriki na kufanikiwa kuuza bidhaa zenye thamani ya shilingi milioni 480. Pia, SIDO
iliwezesha wajasiriamali 442 kushiriki katika maonesho ya Sabasaba na Nanenane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo furaha kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa katika mwaka 2010/2011, Serikali kupitia SIDO imeweza kutoa mafunzo ya ujuzi wa kutengeneza majiko sanifu ya kutumia mkaa kidogo na taka za randa za mbao kwa wajasiriamali 30 katika mikoa ya Iringa na Mtwara. Pia, SIDO imeweza kuandaa makongamano 40 ya uhamasishaji wa utengenezaji na utumiaji wa majiko sanifu, mitambo ya majiko yatumiayo kinyesi cha mifugo na taka za randa za mbao katika mikoa yote nchini. Vilevile, mafunzo ya kuongeza ujuzi katika eneo la uhunzi yalitolewa kwa wahunzi 520 yakilenga kuboresha ubora wa bidhaa zao na kuhimili ushindani wa
kibiashara ambapo mikoa ya Mtwara, Shinyanga na Iringa ilinufaika na mafunzo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, SIDO ilitoa mafunzo kwa wajasiriamali 15,722 kupitia kozi 564 zilizoendeshwa katika mikoa mbalimbali. Vilevile, SIDO ilitekeleza utaratibu wa kujenga uwezo wa wajasiriamali wadogo 10,976 kwa kushirikiana na TPSF kupitia programu ya Business Development Gateway (BDG) ambao walishiriki katika ushindanishaji wa mipango ya biashara na kufanya tathmini ya miradi iliyopitishwa. Hii inafanya wajasiriamali waliopata mafunzo
kati ya 2005/2006 na 2010/2011 kufikia 39,181.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2010/2011 thamani ya
mauzo ya bidhaa nje imeongezeka kutoka dola za Kimarekani milioni 3,294.7 mwaka wa fedha 2009/2010 hadi kufikia dola za Kimarekani milioni 4,296.8 kwa mwaka wa fedha 2010/2011. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 30.4. Mauzo ya Tanzania yameongezeka kutoka shilingi bilioni 3,753 mwaka fedha 2009/2010 hadi kufikia shilingi bilioni 5,191 mwaka 2010/2011 ikiwa ni ongezeko la
shilingi bilioni 1,438 sawa na asilimia 38.3.

Aidha, manunuzi ya bidhaa kutoka nje pia yameongezeka kutoka shilingi bilioni 8,447 mwaka fedha 2009/2010 na kufikia shilingi bilioni 11,119 mwaka 2010/2011 ikiwa ni ongezeko la shilingi bilioni 2,672 sawa na ongezeko la asilimia 31.6. Thamani ya mauzo ya bidhaa asilia (traditional commodities) iliongezeka hadi dola za Kimarekani milioni 559.0 mwaka 2010/2011 kutoka dola za Kimarekani milioni 479.6 mwaka 2009/2010 sawa na ongezeko la asilimia 16.5. Thamani ya mauzo ya bidhaa zisizo asilia (non-traditional products) iliongezeka hadi dola za Kimarekani milioni 3,177.3 mwaka 2010/2011 kutoka dola za Kimarekani milioni 2,376.1 mwaka
2009/2010 sawa na ongezeko la asilimia 33.7.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2010/2011 thamani ya mauzo ya bidhaa za viwandani iliongezeka kwa asilimia 90.3 hadi dola za Kimarekani milioni 963.9 kutoka dola za Kimarekani milioni 506.5 mwaka 2009/2010. Mauzo ya bidhaa za viwandani yalichangia asilimia 30.3 ya mauzo
yasiyo asilia kwa mwaka 2010/2011 ikilinganishwa na asilimia 21.3 mwaka 2009/2010.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla ongezeko la mauzo nje lilichangiwa na kuimarika kwa mazingira ya kufanya biashara ikiwa ni pamoja na mwamko uliotokana na uhamasishaji wa fursa za masoko na kupungua kwa mdororo wa uchumi duniani. Aidha, kupanuka kwa fursa za masoko mfano yale ya China na Jumuiya ya Afrika Mashariki yote kwa pamoja yamechangia ongezeko la biashara nchini katika kipindi cha mwaka 2010/2011 ambapo thamani ya mauzo ya Tanzania kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki iliongezeka kwa asilimia 70.6 kutoka dola za Kimarekani milioni 263.8 mwaka 2009/2010 hadi dola milioni 450.0 mwaka 2010/2011. Ongezeko
hilo lilichangiwa na mauzo zaidi nchini Kenya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, thamani ya mauzo kwa nchi ya Kenya iliongezeka kwa asilimia 67.6 kufikia dola za Kimarekani milioni 297.3 mwaka 2010/2011. Mauzo ya bidhaa kwa nchi ya Kenya yalichangia asilimia 66.1, Rwanda asilimia 12.2, Burundi asilimia 11.3 na Uganda ilichangia asilimia 10.4. Nafurahi kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa urari wa biashara ya bidhaa kati ya Tanzania na nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki ulikua na ziada ya dola za Kimarekani milioni 164.8 mwaka 2010/2011 ikilinganishwa na nakisi ya dola za Kimarekani milioni 46.7 mwaka 2009/2010. Hivyo, Watanzania tuondoe hofu ya kumezwa na Kenya na badala yake tuongeze bidii
ili badala ya kuwa soko la wenzetu, tuendelee kuwauzia bidhaa kwa wingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, thamani ya mauzo ya bidhaa kwenda nchi za Bara la Asia zikiwemo China, Japan, India, Hong Kong na Falme za Kiarabu iliongezeka kwa asilimia 29.0 hadi dola za Kimarekani milioni 1,200.2 kutoka dola 930.3 milioni mwaka 2009/2010. Kwa mara nyingine Waheshimiwa Wabunge niwahakikishie kuwa mauzo yetu ndani na nje ya nchi yatazidi
kuongezeka kwa kupata huduma za bar codes na packaging.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majadiliano ya Kimataifa ya Duru la Doha, Tanzania na nchi nyingine maskini duniani zimeendelea kutetea msimamo wa nchi maskini wa kutaka majadiliano yakamilike mapema iwezekanavyo na kuhakikisha kuwa maslahi yanayolenga maendeleo ya nchi maskini yanazingatiwa. Msimamo wa Tanzania na nchi nyingine maskini duniani ni kushinikiza kupunguzwa na hatimaye kuondolewa kwa ruzuku kubwa zinazotolewa na nchi tajiri kwa wakulima wao na kufanya bidhaa zetu zitokanazo na kilimo kutohimili ushindani katika masoko ya
nchi tajiri.

Aidha, shinikizo la kupatiwa misaada ya kifedha na kiufundi limeendelezwa na hatimaye kuwezesha walau kupata kiasi kidogo cha fedha. Mojawapo ni fedha zilizopatikana na kuwezesha kufanya mapitio ya Sheria ya Anti-Dumping inayolenga kudhibiti biashara ya ushindani usio wa haki. Aidha, Mfuko wa Maendeleo wa Jumuiya ya Ulaya (EDF) umefadhili zoezi la kuandaa Sera ya Taifa ya Haki Miliki ambapo imetoa mchango wa kiasi cha takriban shilingi milioni 130. Juhudi zinaendelea ili kushinikiza kuongezewa fedha zaidi na hasa kupitia mfuko wa Aid for Trade ili
kukabiliana na changamoto zikiwemo za uzalishaji duni na kuboresha miundombinu ya masoko.

Vilevile mafanikio mengine ni pamoja na Tanzania kupunguziwa madeni yake na hata kusamehewa katika maeneo mengine. Hata hivyo, pamoja na mafanikio haya madogo, bado nchi tajiri hazijaonesha waziwazi dhamira ya kukubaliana na misimamo inayolenga maslahi ya
kundi la nchi maskini duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara iliendelea kushiriki kikamilifu katika mchakato wa hatua ya pili ya mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo ni kuanzishwa kwa Itifaki ya Soko la Pamoja. Kama nilivyokwishaelezea awali, mazungumzo ya kuanzishwa kwa Itifaki ya Soko la Pamoja yalikamilika na utekelezaji wa Itifaki hiyo ulianza rasmi mwezi Julai, 2010. Hatua nyingine zilizoendelea ni ukamilishwaji wa viambatisho kwenye Itifaki ya Soko la Pamoja mwezi Februari, 2011. Viambatisho hivyo vilihusu sekta ndogo za ujenzi na masuala ya ufundi, afya na huduma za
jamii, michezo na utamaduni, huduma za utunzaji wa mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ambayo sasa ni eneo huru la biashara, Tanzania imeendelea kutekeleza Itifaki ya Biashara ya SADC kwa kuendelea kupunguza viwango vya ushuru wa bidhaa kwa lengo la kufikia asilimia sifuri ifikapo mwaka 2012 ili kuwezesha kuingia hatua ya pili ya Umoja wa Forodha na hili linafanyika kwa nchi zote wanachama wa SADC. Hatua ya eneo huru imechangia kuongezeka kwa biashara kati ya Tanzania na nchi wanachama za SADC.

Ninayo furaha tena kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa katika mwaka 2010/2011 thamani ya mauzo ya bidhaa za Tanzania kwa nchi za SADC iliongezeka kwa asilimia 67.0 kutoka dola za Kimarekani milioni 374.2 mwaka 2009/2010 hadi dola za Kimarekani milioni 625.1 mwaka 2010/2011.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara pia imeendelea kushiriki kikamilifu kwenye mchakato wa kuanzishwa kwa Umoja wa Forodha wa SADC na mchakato wa kuanzishwa kwa Itifaki ya Biashara ya Huduma. Lengo la Itifaki hii ya Biashara ya Huduma ni kuwezesha nchi wanachama kufunguliana milango katika sekta hii na hivyo kupanua zaidi wigo wa fursa za masoko. Majadiliano yapo katika hatua za awali na Wizara ya Viwanda na Biashara inaratibu majadiliano
haya kwa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uimarishaji wa vituo vya biashara vya London na Dubai, Wizara inaendelea kuviimarisha kwa kuvipatia vitendea kazi kama vile samani za ofisi na kuimarisha mawasiliano. Vilevile kuviongezea uwezo kifedha kadri Wizara inavyopata fedha. Kituo cha Dubai kiliratibu ushiriki wa kampuni ya Classic Homecare Furniture kwenye maonesho ya mbao yaliyofanyika kuanzia tarehe 5 - 7 Aprili, 2011 Airport Expo Center -Dubai ambapo Kampuni ilifanikiwa kupata order za kuuza milango ya mbao na vilevile kupata machine na vifaa vya kuboresha utendaji wa kiwanda.

Aidha, Kampuni ilipata mashine ya kusindika vumbi la mbao kuwa mkaa wa kupikia ili kuondosha tatizo la uchafuzi wa mazingira. Kampuni ya MAM Foodstuff LLC ya Dubai ilikuja Tanzania ili kutatua matatizo yanayokwamisha uuzaji wa matunda hususan maparachichi kutoka Tanzania kwa kushirikiana na Technoserve na Frank Horticultural and Timber Crops. Sababu kubwa inayokwamisha uuzaji huo ni gharama kubwa ya usafiri wa ndege toka Tanzania. Technoserve wanafuatilia kupata punguzo la bei toka shirika la ndege la Emirates. Kituo pia kilitoa ushauri kwa Kampuni ya Arabian Resources ambayo watashirikiana na TCCIA kuandaa maonesho makubwa ya kilimo na kongamano la uwekezaji kwenye kilimo litakalofanyika mwezi Mei, 2012 Mlimani City, Dar es Salaam.

Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Wizara ya Fedha ipo katika mchakato wa kuanzisha vituo vya biashara nchini China na Marekani kwa lengo la kukuza mauzo nje na kuvutia wawekezaji. Tayari Serikali ya China pamoja na Benki ya Dunia wameonesha nia ya kusaidia kuanzisha kituo hicho nchini China na
tayari Serikali ya China imetenga eneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inashikiri kikamilifu kwenye mchakato wa kuanzishwa kwa
Eneo Huru la Biashara (Grand FTA) litakalojumuisha Kanda za COMESA, EAC na SADC. Hatua mbalimbali zimefikiwa ikiwa ni pamoja na kusainiwa kwa Hati ya Makubaliano (Memorandum of Understanding - MoU) na roadmap. Kukamilika kwa eneo huru kubwa la biashara la Kanda hizi tatu za COMESA, EAC na SADC kutasaidia kupanuka kwa soko la bidhaa zetu na pia litasaidia kupunguza tatizo la mwingiliano wa Kikanda (multiple membership) na hivyo kuwezesha biashara kufanyika bila vikwazo. Wakuu wa nchi za Kanda hizi wameshaidhinisha kuanzwa kwa majadiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia Mkakati Unganishi wa Biashara Tanzania (TTIS) imeunda Programu ya Uendelezaji wa Sekta ya Biashara (Trade Sector Development Programme- TSDP) kupitia mfuko maalumu (Multi Donor Basket Fund) ambao utashirikisha washirika wetu wa Maendeleo (Development Partners) katika kuchangia mfuko huo. Utekelezaji wa programu hiyo
unategemea kuanza rasmi katika mwaka wa fedha wa 2011/2012.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa, nchi ya Sweden kupitia Shirika lake la Maendeleo ya Kimataifa (SIDA) imeonesha nia ya kuchangia kwenye mfuko. Aidha, Mkakati wa Zanzibar wa Kuendeleza Mauzo Nje (Zanzibar Export Development Strategy-ZEDS) ambao umetayarishwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar umeonekana kuwa unakidhi mahitaji ya Diagnostic Trade Integration Study (DTIS) iliyotakiwa ifanyike Zanzibar chini ya Mkakati Unganishi wa Biashara Tanzania (TTIS) na hivyo hakuna haja ya kufanya DTIS tena kwa madhumuni ya kujumuisha
masuala ya Zanzibar katika programu ya TSDP.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa na ushirikiano mkubwa na wenzetu wa Zanzibar kupitia Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, pamoja na Zanzibar Chamber of Commerce and Agriculture (ZNCC). Wizara ilitayarisha mwelekeo (Road Map) kwa kupitia programu ya TTIS tuliweza kugharimia mafunzo juu ya Usimamizi wa Miradi (Project Life Cycle Management) kwa wadau wa TTIS Zanzibar kama sehemu ya maandalizi ya TSDP. Kamati za Taifa ya Uendeshaji (Trade Integration National Steering Committee) na Kamati ya Wataalamu (TTIS Technical Committee) ziliendelea kutekeleza majukumu yao katika mkakati huu wa TTIS kwa kufanya vikao na kutoa maelekezo kwa Wizara kwa ajili ya utekelezaji wa yale yaliyokubaliwa katika vikao hivyo. Pia wajumbe kutoka sekta za umma na binafsi kutoka Zanzibar waliingizwa katika Kamati hizo ili kuziimarisha katika kushughulikia biashara za nje kama moja ya
masuala ya Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi ilifanya zoezi la kufuatilia miradi ya majaribio (pilot projects) iliyotekelezwa na wavuvi katika Mikoa ya Dodoma na Iringa na pia wanenepeshaji wa mifugo kibiashara katika Mikoa ya Mwanza na Shinyanga. Miradi yote imeonesha mafaniko makubwa na kuleta matokeo chanya (positive impact) kwa wavuvi na wafugaji/wanenepeshaji mifugo walioshiriki katika miradi husika. Hali kadhalika, Wizara ilifuatilia mradi uliotekelezwa na TAHA, ambao pia ulionesha kuwa na matokeo chanya na mafanikio makubwa kwa wakulima wadogo wadogo wa mboga mboga na matunda
katika Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, kwa ujumla kumekuwa na unafuu wa bei ya mlaji kwa mazao makuu ya chakula. Wastani wa bei ya jumla ya mahindi kwa gunia la kilo 100 ilishuka kutoka shilingi 42,133 mwaka 2009/2010 na kufikia shilingi 34,247 mwaka 2010/2011 ikiwa ni punguzo la asilimia 18. Aidha, bei za mchele, ngano, ulezi na mtama zilishuka pia. Bei ya mlaji kwa maharage ilipanda kutoka shilingi 105,092 hadi shilingi 109,537 kwa gunia la kilo 100 sawa na ongezeko la asilimia nne. Kupanda na kushuka kwa bei ya mazao makuu ya chakula
kulitokana na hali halisi ya ugavi na mahitaji katika soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010, wastani wa bei ya mkulima kwa mazao ya kahawa, chai, pamba, mkonge na korosho uliongezeka. Aidha, bei ya kuuzia nje iliongezeka kwa mazao ya chai na kahawa aina ya Arabika ambapo wastani wa bei ya kahawa ya aina ya Arabika ilipanda kutoka dola za Kimarekani 2.98 kwa kilo mwaka 2009 hadi 3.45 mwaka 2010 na katika kipindi hicho wastani wa bei ya chai ilipanda kutoka dola za Kimarekani 2.40 hadi 2.91.

Hata hivyo, wastani wa bei ya kahawa aina ya Robusta ilishuka kutoka dola za Kimarekani 2.02
kwa kilo mwaka 2009 hadi dola 1.57 mwaka 2010, na wastani wa bei ya mkonge pia ilishuka kutoka dola za Kimarekani 1,209 kwa tani mwaka 2009 hadi dola za Kimarekani 908 kwa tani
mwaka 2010.

Aidha, mwenendo wa bei za bidhaa nyingi za viwandani unaonyesha kuwa bei zilipanda. Bei ya rejareja ya sukari ilipanda kutoka wastani wa shilingi 1,500 hapo mwaka 2009 hadi kufikia shilingi 1,600 mwaka 2010 kwa kilo. Bei hiyo ilipanda zaidi katika robo ya kwanza ya mwaka 2011 hadi kufikia shilingi 2,000 hapo Machi 2011. Hata hivyo, kufuatia jitihada mbalimbali za Serikali kwa kushirikiana na wadau husika, bei hiyo imeshuka na kuwa kati ya shilingi 1,600 na shilingi 1,800 kwa kilo moja katika maeneo mengi. Bei ya rejareja ya saruji ya mfuko wa kilo 50 katika masoko mbalimbali nchini ilikuwa kati ya shilingi.12,500 na shilingi 17,400 mwezi Desemba 2009 na kupanda na kuwa kati ya shilingi 13,046 na shilingi 19,000 Desemba, 2010. Vilevile bei ya bati la geji 30 ilishuka kutoka kati ya shilingi12,500 na shilingi 17,722 mwezi Desemba, 2009 hadi kufikia kati ya
shilingi 11,000 na shilingi 17,061 mwaka 2010.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, kumekuwa na ongezeko la bei ya mifugo (ng'ombe, mbuzi na kondoo). Wastani wa bei ya jumla ya ng'ombe daraja la pili iliongezeka kutoka shilingi 389,696 mwaka 2009 hadi shilingi 393,853 mwaka 2010 ambalo ni sawa na ongezeko la asilimia moja. Aidha, bei ya ng'ombe daraja la tatu ilishuka kutoka shilingi 285,470 mwaka 2009 hadi shilingi 285,359 mwaka 2010 sawa na anguko la asilimia 0.04. Bei ya mbuzi ilipanda kutoka shilingi 37,458 hadi shilingi 38,805 wakati bei ya kondoo ilipanda kutoka shilingi
32,677 hadi shilingi 34,333 katika kipindi hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa taarifa za masoko umeendelea kuboreshwa na kupanuliwa katika kukusanya, kuchambua, kuhifadhi na kusambaza taarifa za masoko ya mazao ya kilimo, mifugo na bidhaa za viwandani hususan za saruji, mabati na nondo. Taarifa za masoko ya mazao zinaonesha kuwa masoko yameongezeka kutoka masoko 93 katika mwaka wa fedha 2008/2009 hadi masoko 104 mwaka 2010/2011. Pia, minada ya mifugo imeongezeka kutoka minada 46 mwaka 2009 hadi minada 53. Taarifa hizo husambazwa kwa kushirikiana na sekta binafsi kwa njia ya magazeti, luninga, tovuti, mtandao wa internet na ujumbe wa simu za kiganjani. Taarifa za bei ya mazao makuu ya chakula husambazwa kwa wadau mara tatu kwa wiki na taarifa za bei ya mifugo hukusanywa na kusambazwa mara moja kwa wiki. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Benki ya Dunia pamoja na wadau wengine ipo katika hatua za mwisho kukamilisha Mkakati wa Kuanzisha Mfumo Mpana na Unganishi wa Taarifa za Masoko kwa masoko
ya ndani na nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imeshirikiana na taasisi binafsi ikiwemo Nuru Infocom Ltd., makampuni ya huduma za simu, vyombo vya habari na magazeti kuwahabarisha wananchi juu ya taarifa muhimu za biashara na masoko ili waweze kufanya maamuzi muafaka katika uzalishaji, usindikaji na uuzaji wa mazao na bidhaa zao. Taarifa hizo hujumuisha bei kwa kila aina ya zao,
madaraja, masoko na ugavi kwa upande wa mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tathmini ya matumizi ya taarifa za masoko imefanywa sanjari na jitihada za kuanzisha mkakati wa mfumo mpana na unganishi wa taarifa za masoko. Tathmini ilibaini umuhimu wa kuongeza jitihada za usambazaji wa taarifa hususan vijijini kwa njia za kisasa zaidi kama matangazo ya redio, ujumbe wa simu za kiganjani na mbao za matangazo. Aidha, Wizara imekamilisha ujenzi wa banda la kudumu katika viwanja vya Maonesho ya Wakulima Nzuguni Dodoma ili kufanikisha utangazaji wa majukumu ya Wizara, bidhaa/teknolojia zinazozalishwa na Taasisi zetu pamoja na huduma wanazotoa kwa wakulima na wananchi wengine wakati wa Maonesho ya Nanenane. Aidha, wajasiriamali pamoja na taasisi nyingine binafsi za wazalishaji wa bidhaa za kilimo na mifugo waliwezeshwa kushiriki katika maonesho ya
Sabasaba na ya wakulima Nanenane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuimarisha uwezo wa halmashauri na manispaa wa kukusanya na kusambaza taarifa za masoko, Wizara imeendelea kutoa mafunzo kwa wakusanya taarifa za masoko ya mazao ya kilimo na mifugo walioko katika Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji 114 kwa upande wa mazao makuu ya chakula na 52 ya mifugo. Aidha, vitendea kazi vimeendelea kutolewa kwa ajili ya kuwezesha na kufanikisha ukusanyaji wa taarifa hizo.
Uboreshaji zaidi unaofanywa ili taarifa hizo zitumwe na kusambazwa kwa njia ya ujumbe kwa njia ya kisasa zaidi ikiwemo ujumbe wa simu ya kinganjani (sms).

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia Bodi ya Leseni za Maghala Tanzania kwa kutumia mfumo wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani umewezesha ubora wa mazao yaliyohifadhiwa ghalani kuongezeka na kuwezesha wakulima kulipwa bei inayolingana na ubora. Kwa mfano, katika Mkoa wa Pwani zaidi ya asilimia 80 ya korosho ziliuzwa kama daraja A msimu wa 2010/2011, ikilinganishwa na hapo awali ambapo korosho zote kutoka mkoa wa Pwani na Tanga ziliuzwa kama daraja B. Mfumo huu pia ulionesha ongezeko la korosho zilizokusanywa katika maghala kutoka tani 72,492 mwaka 2009/2010 hadi tani 120,139 mwaka 2010/2011.

Aidha, Mfumo wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani umewezesha matumizi ya vipimo sahihi katika ununuzi wa mazao. Kwa upande wa bei ya wakulima, Mfumo wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani umewawezesha wakulima kupata bei nzuri ikilinganishwa na wale waliouza nje ya mfumo huo. Kwa mfano, wakulima waliotumia mfumo kwa zao la ufuta Mkoani Lindi msimu wa 2010/2011, walipata wastani wa shilingi 1,400 kwa kilo ikilinganishwa na shilingi 1,000 kwa kilo kwa wakulima waliouza nje ya mfumo. Aidha, Mfumo wa Stakabadhi Ghalani umewezesha bei ya korosho daraja la kwanza kuongezeka kutoka shilingi 800 kwa kilo bei dira hadi kufikia wastani wa shilingi 1,600 kwa kilo msimu wa 2010/2011, ikilinganishwa na shilingi 700 bei dira na bei ya wastani 1,428
kwa msimu wa 2009/2010 ikiwa ni ongezeko la asilimia 12.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ya Mfumo wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani imeendelea kutolewa kwa wakulima na viongozi mbalimbali katika mikoa ya Kilimanjaro, Lindi, Manyara, Mbeya, Morogoro, Mtwara, Mwanza, Pwani, Shinyanga na Singida kwa njia ya semina na mikutano. Bodi imeshiriki pia katika maonesho mbalimbali yakiwemo ya Nanenane, Sabasaba, Wiki ya Utumishi wa Umma na Wiki ya Ushirika. Aidha, matangazo ya kalenda na vipeperushi kwa
ajili ya kuhamasisha wadau na kutoa elimu yamefanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfumo wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani umeendelea kusisitiza ubora wa mazao ghalani kwa kuhakikisha vifaa vya kudhibiti ubora vinapatikana kwenye maghala ambapo ni njia mojawapo ya kuongeza thamani na kivutio tosha kwa wanaotaka kusindika mazao husika. Bodi imekuwa ikihimiza wajasiriamali kufungua viwanda vidogo vya
kuongeza thamani karibu na maghala hasa kwa mazao ya alizeti, mahindi na mpunga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kwa kushirikiana na Bodi ya Leseni za Maghala imehamasisha Halmashauri za Wilaya na sekta binafsi kushiriki katika uendelezaji wa miundombinu, mfano, maghala na barabara. Mabenki ya NMB, CRDB Bank na TIB yamekubali kushiriki katika kutoa mikopo ya ujenzi wa miundombinu iliyotajwa. Aidha, NMB na CRDB Bank wamekubali kutoa mikopo kwa vyama vya msingi kwa ajili ya ujenzi wa maghala katika mikoa ya Singida na Pwani. Pia mabenki haya yametoa mikopo kwa ajili ya ununuzi wa mazao. Mikopo iliyotolewa ni pamoja na shilingi bilioni 20.66 zilitolewa na NMB msimu wa 2009/2010 na kuongezeka hadi shilingi bilioni 42.9 msimu 2010/2011; CRDB Bank walitoa mikopo ya kiasi cha shilingi billioni 45.92 mwaka 2009/2010 na kuongezeka hadi shilingi bilioni 66.17 msimu 2010/2011. KCB msimu wa 2009/2010 ilitoa mikopo ya kiasi cha shilingi bilioni 2.96 na msimu wa 2010/2011 imetoa shilingi bilioni 2.16.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kwa kushirikiana na Bodi ya Leseni za Maghala, Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Mamlaka ya Soko la Mitaji na Hisa (Capital Markets and Securities Authority CMSA), Wizara ya Fedha, Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeanza kufanya matayarisho ya uanzishaji wa Soko la Bidhaa (Commodity Exchange) hapa nchini. Maandalizi ya concept paper yamekamilika. Aidha, timu ya maafisa wa Serikali iliyoundwa kuratibu maandalizi haya inashirikiana na taasisi za Kimataifa hususan UNCTAD na Benki ya Dunia kuandaa road map ya uanzishaji wa soko la bidhaa nchini. Jitihada zinafanyika ili kuwezesha kutembelea baadhi ya nchi zilizofanikiwa katika kuendesha soko la bidhaa ikiwa ni
pamoja na nchi za Afrika ya Kusini, Ethiopia na India.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia Bodi ya Leseni za Maghala inaendelea kuhimiza
ujenzi wa maghala mapya yatakayojengwa yawe na ujazo usiopungua tani 3,000 na kuongezea uwezo maghala yaliyopo pale inapowezekana ili yaweze kuwa na ujazo huo. Hii itasaidia hasa pindi kutakapokuwa na soko la bidhaa ambapo mnunuzi anaweza kupata mazao mengi kwenye kituo kimoja, pia kuwezesha maghala yawe na vifaa vyote vya kitaalamu ili iwe rahisi
kuyaunganisha na soko la bidhaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maghala yapatayo 27 yamepewa leseni msimu wa 2010/2011. Aidha, kulingana na Ssheria Nambs 10 ya mwaka 2005 ambayo inawataka waendesha maghala wote kusaini hati ya kinga (performance bond) na Bodi ya Leseni ya Maghala, akaunti imefunguliwa katika benki ya CRDB ambapo waendesha maghala wanaweka fedha za kinga kulingana na utaratibu wanaopewa. Kiasi cha shilingi 100,235,919 zimeshaingizwa katika akaunti hiyo na shilingi
55,098,418 zimeshalipwa kama fidia kwa wanaostahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya Leseni za Maghala kwa kushirikiana na taasisi nyingine zinazosaidia katika utekelezaji wa Mfumo wa Stakabadhi za Mazao Ghalani zimekusanya maoni kutoka kwa wadau kuhusu maeneo yenye utata au mgongano katika Sheria Namba 10 ya 2005 na Kanuni zake, pia kuangalia sheria nyingine zenye mahusiano ya kiutekelezaji na mfumo mzima. Kazi hiyo inafanyika kwa kutumia vikundi kazi (working groups) vilivyoundwa baada ya mkutano wa wadau. Aidha, Bodi imewasiliana na Chuo cha Ushirika Moshi kwa lengo la kuangalia namna ya kuanzisha mitaala mbalimbali kwa wadau. Kinachotakiwa kufanyika ni kuona jinsi walimu wa Chuo hicho watakavyopata elimu kuhusu mfumo huu ili waweze kuandaa mitaala na kufundisha. Wizara imejadiliana na Natural Resource Institute (NRI) ya Uingereza ambao wana utaalamu katika eneo la Mfumo wa Stakabadhi ili kuweza kuwafundisha walimu kutoka Chuo cha Ushirika
Moshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara nchini (TanTrade) iliandaa Maonesho ya 34 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam. Maonesho hayo yaliendelea kuwa kivutio kikubwa kwa washiriki wa ndani na nje ikilinganishwa na Maonesho ya nyuma. Idadi ya waoneshaji iliongezeka kutoka 2,103 mwaka 2009 hadi 2,150 mwaka 2010 sawa na ongezeko la asilimia 2.2. Kati ya hao, washiriki 1,800 walikuwa wa ndani ya nchi na washiriki 350 walitoka nje ya
nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yameendelea kutumiwa na nchi mbalimbali shiriki kama jukwaa la kutangazia biashara zao. Kumekuwapo na ongezeko la nchi shiriki kutoka 23 mwaka 2009 hadi 27 mwaka 2010. Katika Maonesho hayo, maulizo ya biashara kwa ajili ya soko la nje (export enquiries) yalikuwa dola za Kimarekani milioni 196.0 mwaka 2010 ikilinganishwa na dola za Kimarekani milioni 199.1 kwa mwaka 2009, huo ukiwa ni upungufu wa asilimia 1.56. Upungufu huo umetokana na mtikisiko wa kiuchumi wa dunia na uwepo wa upungufu wa makampuni yaliyotaka kuagiza bidhaa toka hapa nchini. Kadhalika, maulizo ya bidhaa kutoka nje ya nchi yalikuwa dola za Kimarekani milioni 197.0 mwaka 2010 ikilinganishwa na dola za Kimarekani milioni 132.7 mwaka 2009, hilo likiwa ni ongezeko
la asilimia 48.0.

Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu zinaonesha kupungua kwa mauzo ya papo kwa papo kutoka takribani shilingi bilioni 25.4 mwaka 2009 hadi takribani shilingi bilioni 25.0 mwaka 2010. Kupungua kwa mauzo haya kumetokana na mwamko wa washiriki kuyatumia maonesho haya kwa ajili ya kutafuta biashara endelevu badala ya kufanya mauzo ya papo kwa papo. Pamoja na hali hiyo, katika mikutano ya kibiashara ijulikanayo kama business to business meetings iliyofanyika wakati wa maonesho, makampuni 67 kutoka nje na ndani ya nchi yalishiriki. Katika mikutano hii kulikuwa na maongezi ya kibiashara ya thamani ya shilingi milioni 608.95 zikijumlisha uwekezaji
katika sekta ya kilimo, mahitaji ya bidhaa za nguo, ngozi na nyuzi za pamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TanTrade iliratibu ushiriki wa Tanzania katika Maonesho ya Expo 2010 Shanghai ambapo washiriki 23 wakiwemo TTB, TIC, TANAPA na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro walishiriki katika kunadi vivutio vya utalii, kutangaza maeneo ya uwekezaji na kuonesha bidhaa zao. Maonesho China yaliyodumu kwa muda wa miezi sita yaliyojulikana kama Expo 2010 Shanghai yaliyofanyika nchini China. Kaulimbiu ya maonesho hayo ilikuwa ni Mji Bora Maisha Bora (Better City Better Life) na Tanzania ilitumia fursa hiyo kutangaza miradi tisa iliyoendana na
kaulimbiu hiyo pamoja na vivutio vya utalii, utamaduni na uwekezaji. Banda la Tanzania lililojengwa kwa mandhari ya Kitanzania lilikuwa kivutio kwa watembeleaji pamoja na wageni na
viongozi mashuhuri kutoka Tanzania na nchi nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekit, TanTrade imeanza kutekeleza jukumu la uratibu wa biashara ya ndani i
kwa kufanya utafiti katika mikoa na wilaya zote za Kanda ya Ziwa na Kanda ya Magharibi pamoja na mipaka iliyopo katika Kanda hizo. Katika utafiti huo, TanTrade ilikutana na viongozi wa mikoa, wilaya, tarafa, kata, vijiji pamoja na wazalishaji mbalimbali katika Sekta za Kilimo, Mifugo, Madini na Maliasili ili kubaini bidhaa zinazozalishwa, wingi wake, ubora, mfumo wa masoko, bei na kutambua changamoto zinazowakabili wazalishaji. Utafiti huo ulibaini changamoto mbalimbali zikiwemo za kutokuwepo mfumo wa masoko, miundombinu hafifu hususan ya barabara kufika maeneo ya uzalishaji, bei ndogo za bidhaa zinazozalishwa, ubora hafifu wa baadhi ya bidhaa na vikwazo mbalimbali vikiwemo vya ushuru katika maeneo ya mipakani mwa Tanzania na nchi jirani. Mapendekezo ya mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo yamewasilishwa kwa mikoa husika kwa hatua zaidi na TanTrade inaendelea kufanya kazi na Uongozi wa Mikoa na Wilaya ili
kushirikiana katika kupata ufumbuzi wa kudumu wa changamoto hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS) iliendelea na majukumu ya uwekaji viwango vya ubora wa bidhaa na usimamiaji wa utekelezaji wa viwango hivyo. Pamoja na viwango vinavyohusu sekta mbalimbali, Shirika lilikamilisha viwango muhimu vya vigae, ubora wa huduma za nishati, uwezo wa vifaa au mifumo kufanya kazi bila mwingiliano na sumaku umeme katika mazingira, mafuta ya kula, maziwa, nguo, ubora wa maji, matairi ya magari, vifaa vya ujenzi, zana za kilimo kama vile matrekta, majembe, plau, matrekta ya kusukuma kwa mikono (power tillers) na mashine zinazotumika katika kilimo. Hadi kufikia mwezi Machi, 2011, Shirika lilikuwa limetayarisha viwango vya Taifa 1,427 katika sekta mbalimbali yaani
kilimo na chakula, nguo, kemikali, uhandisi, mazingira na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Viwango limeendelea na juhudi za kutoa mchango muhimu katika Sekta ya Ufungashaji wa Bidhaa kupitia Kituo cha Ufungashaji (Packaging Technology Centre) ambacho kwa sasa hivi kipo katika hatua ya majaribio ya awali. Aidha, Shirika liliendelea na utoaji wa mafunzo ya ufungashaji bora kwa wajasiriamali wadogo na kati (SMEs) wapatao 140 katika mikoa ya Iringa, Mtwara, Rukwa na Tanga. Kituo kitakapoanza kazi rasmi, kitatoa huduma za kupima sampuli za viwanda vya ufungashaji kwa lengo la kuongeza ubora wa bidhaa zinazozalishwa hapa nchini na kuhakiki vifungashio (packaging materials) kwa bidhaa
zinazotoka nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika linaendelea na juhudi za kuziwezesha maabara zake kupata umahiri na kufikia viwango vya upimaji vya Kimataifa (laboratory accreditation). Ninayo furaha kulitaarifu Bunge lako kuwa tarehe 4 Novemba 2010, Kamati ya pamoja ya SADCAS na SANAS iliipatia Maabara ya Shirika ya Ugezi Cheti cha Umahiri wa Utendaji wa Kazi zake
(laboratory accreditation) katika Nyanja ya upimaji wa ukubwa (dimensional).

Pia, Maabara ya Chakula (food microbiology) nayo ilipata Cheti cha Umahiri wa Utendaji kazi zake (laboratory accreditation) katika upimaji wa vijidudu kwenye vyakula na maji vinavyosababisha maradhi kama vile homa ya matumbo (typhoid), kipindupindu (cholera), kuumwa tumbo na kuhara (E.coli) na magonjwa yaambatanayo na majipu (staphylococci).

Aidha, maabara za Shirika za Uhandisi Umeme, Uhandisi Mitambo na Uhandisi Ujenzi zimekamilisha miongozo ya ubora kulingana na kiwango cha kimataifa ISO/IEC 17025 na tayari imekaguliwa na imeidhinishwa. Wakati wowote maabara hizo zitafanyiwa ukaguzi wa awali wa kuthibitisha umahiri wa upimaji wa nyaya za umeme, nondo na simenti. Kupata umahiri kwa maabara hizo, kutawahakikishia walaji ubora wa bidhaa zinazozalishwa na kuingizwa nchini. Pia watunga sera watakuwa na uhakika wa kutolea maamuzi ya majibu yaliyopatikana kutoka katika maabara zilizohakikiwa umahiri wake. Vilevile hatua hizo zitapanua masoko ya bidhaa zetu ndani na nje, kwani taarifa za upimaji na ugezi zitakazotolewa na Shirika zitatambulika Kimataifa na hivyo
kuongeza kukubalika kwa bidhaa za Tanzania duniani kote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TBS inashirikiana na mashirika mengine ya viwango Kikanda na
Kimataifa katika uwekaji wa viwango. Katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Shirika linaendelea kushirikiana na mashirika ya viwango ya Burundi, Kenya, Rwanda na Uganda kuweka viwango vya Afrika Mashariki. Nafurahi tena kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa hadi Machi 2011, jumla vya viwango vya Afrika Mashariki 1,222 vilikamilishwa katika nyanja za uhandisi, vyakula, nguo na
kemikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Viwango Tanzania kupitia programu ya MKUKUTA limesaidia kuinua ubora wa bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa na wajasiriamali wadogo na wa kati (SMEs). Hadi kufikia mwezi Machi 2011, jumla ya leseni 63 zilikuwa zimetolewa kwa viwanda vya wajasiriamali wadogo na wa kati (SMEs) baada ya kuthibitishwa kuwa vinazalisha kulingana na viwango vya Kitaifa ambavyo huwaruhusu kutumia alama ya ubora wa bidhaa TBS kwa bidhaa zifuatazo, mkate, mafuta ya kujipaka mwilini, siagi, chaki, spageti, asali, jibini, juisi, mvinyo,
vibamba (paving blocks), unga na achari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika liliendelea na utaratibu wa kufanya ukaguzi wa viwanda vyote hapa nchini kwa nia ya kuvisaidia viweze kuzalisha bidhaa zenye ubora. Hadi kufikia mwezi Machi 2011, Shirika limeweza kutembelea jumla ya viwanda 176 vya wajasiriamali wadogo kama ifuatavyo, Dodoma 18, Kilimanjaro 17, Lindi 4, Manyara 19, Mbeya 15, Morogoro 16, Mtwara 5,
Rukwa 32, Ruvuma 17 na Tabora 33.

Shirika limeendelea kuboresha miundombinu yake kwa kufungua ofisi ya kukagua ubora wa bidhaa zinazoingia Tanzania kupitia mpaka wa Namanga. Aidha, maandalizi yameanza kwa ajili ya ufunguzi wa ofisi ya Tunduma. Kwa sasa tathmini inafanyika kwa ajili ya kufungua ofisi katika mipaka ya Mtambaswala, Mtukula na Rusumo. Kwa upande wa vifaa vya kisasa vya maabara, katika mwaka 2010/2011 Shirika limenunua vifaa vya kupimia ubora wa saruji na upimaji wa
chumvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika pia liliendelea kusimamia utekelezaji wa viwango vya Taifa kwa kutumia mifumo iliyopo ya kuhakiki ubora (certification schemes). Aidha, Shirika lilitoa jumla ya leseni 1,199 za ubora wa bidhaa mbalimbali katika viwanda 762 vya humu nchini. Leseni za ubora wa bidhaa hutolewa na TBS kwa wazalishaji wanaotimiza masharti ya ubora wa bidhaa zikiwemo
zile zinazogusa afya na usalama wa walaji, mazingira na uchumi wa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, Shirika liliendelea kutekeleza Mkakati wa Kudhibiti Bidhaa Duni Kutoka Nje ya Nchi ambapo leseni 2,100 za ubora wa bidhaa zilitolewa ikilinganishwa na leseni 661 za mwaka 2009/2010. Vilevile Shirika linaendelea na jitihada za uanzishwaji wa utaratibu wa upimaji wa ubora wa bidhaa kabla ya kusafirishwa kuja Tanzania (Pre-shipment Verification of Conformity to Standards) na utekelezaji wake unatarajiwa kuanza mwanzoni wa mwaka wa fedha 2011/2012. Zabuni kwa ajili ya kuwapata wazabuni ilikwishatangazwa na kufunguliwa ambapo uchambuzi wa maombi hayo unafanywa. Katika kutekeleza mfumo huo, Shirika hushirikiana kwa karibu sana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2010/2011, Wizara kupitia Wakala wa Vipimo na Mizani imeendelea kukagua na kuhakiki vipimo vinavyotumika katika biashara ili kumlinda mlaji. Jumla ya vipimo 807,719 vinavyotumika katika biashara vilikaguliwa ikilinganishwa
na vipimo 739,842 vya mwaka 2009/2010. Hilo ni ongezeko la asilimia tisa.

Aidha, zaidi ya ukaguzi unaofuata ratiba, ukaguzi wa kushitukiza umefanyika mara nyingi zaidi katika mikoa yote. Jumla ya wafanyabiashara 4,738 walipatikana na makosa kwa kukiuka Sheria ya Vipimo. Hatua mbalimbali za kisheria zilichukuliwa dhidi yao ikiwa ni pamoja na kufilisiwa (compounding) na kushitakiwa mahakamani. Idadi ya watu waliofilisiwa kwa kukiuka matumizi ya
vipimo ni 7,028 na jumla ya kesi 12 zipo mahakamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutoa elimu kwa umma, Wakala wa Vipimo kwa mwaka 2010/2011 imeshiriki katika Maonesho ya Sabasaba, Nanenane, Wiki ya Utumishi wa Umma, pamoja na ya wajasiriamali yaliyotayarishwa na SIDO, Dar es Salaam. Katika maonesho hayo ilipata nafasi ya kuelimisha wazalishaji matumizi sahihi ya vipimo na namna nzuri ya ufungashaji wa
bidhaa wanazozalisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakala imepanua wigo wa kazi zake kutoka vipimo vilivyozoeleka kama mizani na pampu za mafuta kwa kuanzisha upimaji wa malori ya mchanga, kokoto na matenki yanayotumika kuhifadhi mafuta ya kuendeshea mitambo na nishati (storage tanks for petroleum products). Jumla ya malori ya mchanga na kokoto 1,246 yalipimwa katika kipindi cha
mwaka 2010/2011 lengo likiwa ni kupima malori 1,440.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imerekebisha Kanuni za Sheria ya Vipimo kupitia Tangazo la Serikali (Government Notice) Na.144 la tarehe 17 Novemba, 2010 ili kuiwezesha Serikali kufahamu kwa usahihi zaidi kiasi cha mafuta yanayoingizwa nchini kwa madhumuni ya kuondoa udanganyifu uliokuwa unafanywa na baadhi ya waagizaji wa mafuta na hivyo kuwezesha nchi kupata kodi stahiki. Baada ya marekebisho hayo, Wakala pia imeweza kupima matenki makubwa
177.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2010/2011, Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imesajili makampuni 7,058 kutoka makampuni 5,278 mwaka 2009/2010 sawa na ongezeko la asilimia 33.7, majina ya biashara 14,866 kutoka majina ya biashara 11,127 mwaka 2009/2010 sawa na ongezeko la asilimia 33.6, leseni za viwanda 105 kutoka leseni za viwanda 92 mwaka 2009/2010 sawa na ongezeko la asilimia 14.1 na alama za biashara na huduma 1,652 kutoka alama za biashara na huduma 1,724 mwaka 2009/2010.

Pia idadi sawa ya hataza 22 ilitolewa katika kipindi cha miaka miwili. Aidha, ili kuweza kutoa huduma kwa urahisi na kwa ubora zaidi, BRELA inaboresha mfumo wa utoaji wa huduma kwa mfumo wa kielektroniki. Tayari mfumo wa usajili kwa njia ya kisasa (Registration Information Management System - RIMS) umetengenezwa kwa kutumia wataalamu wa ndani na kuweza
kufanya kazi.


Aidha, taratibu za upekuzi wa majina (name search) umeboreshwa na kuwekwa kwenye tovuti ya BRELA ili kumwezesha mdau yeyote kupata huduma hiyo popote alipo (on-line). BRELA imeweka huduma mbalimbali ndani ya tovuti yake ya www.brela-tz.org ikiwa ni pamoja na kuweza kupata fomu zote za usajili popote, Katiba ya kampuni iliyorahisishwa (Simplified MEMART),
maelekezo juu ya majina yanayoruhusiwa na yasiyoruhusiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, BRELA imefanya mazungumzo na TCCIA ili kushirikiana nao katika kutoa huduma saidizi kwa wateja hadi katika ngazi ya Wilaya kwa kuwa tayari wana mfumo wa kitekinolojia unaowasiliana katika wilaya 95. TCCIA watatoa huduma za kuwasaidia waombaji wa kusajili majina ya biashara na makampuni ambazo siyo za kisheria. Rasimu ya makubaliano (MOU) ya kutekeleza azma hiyo imekwishaandaliwa. BRELA imeanza kutembelea baadhi ya vituo vya TCCIA kwa lengo la kujionea hali halisi ya zana za kufanyia kazi na pia kutoa elimu kwa wajasiriamali ili wafahamu uwepo wa huduma hizo katika ofisi za TCCIA zilizo karibu nao. Aidha, BRELA ipo kwenye mazungumzo na TRA ili iweze kutoa huduma ya TIN kwa wateja mara
wanaposajili makampuni na majina ya biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, BRELA imefanya semina na warsha mbalimbali mikoani na jijini Dar es Salaam, imeshiriki maonesho ya Wiki ya Utumishi, Sabasaba, Nanenane na Siku ya Miliki Ubunifu Duniani. Maonesho haya husaidia kuelimisha juu ya shughuli za Wakala kwa wadau wote. Aidha, Wakala umetoa vipeperushi, vitabu vidogo vidogo na makala mbalimbali kwenye vyombo vya habari. Pia iliitisha mkutano wa vyombo vyote vya habari mwezi Februari, 2011 kuelezea uboreshaji mbalimbali uliokwishafanyika katika kuwafikia wadau nchi nzima kwa kutumia mtandao. Wakala pia hufanya ukaguzi kwenye maeneo ya biashara kuangalia na kuelimisha juu ya utekelezaji wa sheria za biashara na kutembelea viwanda. Hilo limefanyika Arusha, Dodoma,
Kigoma, Manyara, Mbeya, Moshi, Mwanza, Songea na Tanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakala imefanya semina mbalimbali za wadau kwa kushirikiana na Shirika la Miliki Ubunifu Duniani (WIPO) ambapo branding strategy itasaidia kuwezesha mazao kama kahawa, chai, karafuu na mchele kuuzwa kwa bei nzuri kwenye masoko ya nje. Mkakati huu
humsaidia mzalishaji na/au muuzaji nje ya nchi wa bidhaa zenye utambuzi wa pekee kufuatilia thamani halisi ya bidhaa anayozalisha ama kuuza nje ya nchi ambayo watumiaji wa bidhaa hiyo watakuwa tayari kuilipa. Aidha mkakati huu hupunguza sana ama kuondoa kabisa wizi wa thamani za bidhaa unaofanywa na madalali katika magulio ya bidhaa hizo ndani ya nchi. Kwa mfano, nchi ya Ethiopia imeutumia kikamilifu mkakati huu katika kuboresha thamani ya bidhaa ya kahawa ya nchi hiyo. Hivi sasa kahawa ya Ethiopia ni miongoni mwa kahawa maarufu sana duniani na inajulikana hivyo kwa kutumia mkakati huo. Vilevile wavumbuzi na innovator katika taasisi za TIRDO, SIDO, COSTECH na Vyuo Vikuu wamehamasishwa kuhusu matumizi bora ya miliki ubunifu kwa kuanzisha na kutumia kituo kilichopo COSTECH (Tanzania Intellectual Property Advisory Service and Information Centre - TIPASIC).

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hatua za kuandaa Mkakati wa Miliki Ubunifu, ilionekana kuna haja kwanza kufanya tathmini ya miliki ubunifu (IP Audit). Kamati ya Kitaifa (National IP Audit Steering Committee) iliyojumuisha wadau wote muhimu iliundwa na Kamati imefanya tathmini ya namna IP Audit itakavyotekelezwa. Wizara kwa kushirikiana na BRELA inafanya maandalizi ya
kupata rasilimali watu na fedha kwa ajili ya kufanya tathmini hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mwanachama wa Mashirika ya Miliki Ubunifu Kikanda na Kimataifa ya African Regional Intellectual Property
Organization (ARIPO) na World Intellectual Property Organization (WIPO). Wizara hulipa
michango ya kila mwaka kwa mashirika yote mawili. Kwa ARIPO, BRELA inapata ada kwa kila hataza na alama ya biashara iliyosajiliwa ARIPO na mwombaji kuomba miliki ubunifu wake ulindwe hapa Tanzania. Katika mwaka huu, BRELA ilishiriki katika mikutano mbalimbali katika ngazi za Kikanda na Kimataifa ambayo inawezeshwa ama na WIPO, ARIPO na/au asasi nyingine za Kimataifa. Aidha, BRELA ilihudhuria Mkutano Mkuu wa Baraza la nchi Wanachama wa WIPO huko Geneva, Switzerland na mkutano uliofanyika Istambul, Uturuki ambapo Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara alihudhuria pamoja na Mwenyekiti na Mjumbe mmoja wa Kamati ya Bunge
ya Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, BRELA imekuwa inatafuta jengo au eneo la kujenga ofisi zake zitakazowezesha kuwahudumia wateja na zilizo na mazingira mazuri ya utendaji wa kazi. BRELA imetenga fedha takriban shilingi bilioni tatu za kuanza kujenga jengo lake. Hadi sasa bado eneo la kujenga jengo la ofisi halijapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka 2010/2011, COSOTA imeendelea kutoa huduma mbalimbali ikiwemo usajili wa wanachama na kazi zao. Jumla ya wanachama 2,215 walisajiliwa kati ya hao watunzi na wasanii wa kazi za muziki ni 1,142, wachapishaji na wazalishaji wa kazi za muziki ni 35, watunzi na waigizaji wa kazi za maigizo ni 309, wachapishaji na wazalishaji wa kazi za maigizo ni 18, watunzi wa kazi za maandishi ni 669 na wachapishaji wa kazi za maandishi ni 42. Aidha, jumla ya kazi 9,461 zilisajiliwa zikiwemo kazi za muziki 8,202, maigizo 423 na maandishi 836.

Mheshimiwa Mwenyekiti, COSOTA inaendesha zoezi la ukusanyaji wa mirabaha kutokana na matumizi ya kazi za muziki na filamu (maonyesho ya umma) katika mahoteli, baa, migahawa, kumbi za disko na majumba ya starehe. Katika mwaka 2010/2011 jumla ya shilingi 162,795,000.00 zimekusanywa, ambapo jumla ya leseni 746 zimetolewa kwa wamiliki wa maeneo husika. Makusanyo hayo yamegawanywa kama mirabaha na kunufaisha jumla ya watunzi na wasanii 1,142 wa fani ya musiki na filamu. Vilevile COSOTA imeanza zoezi la ukadiriaji wa mirabaha kutoka kwenye mabenki, makampuni ya simu na mashirika ya utangazaji. COSOTA inawasiliana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ili kupata
taarifa zitakazorahisisha zoezi hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kudhibiti uharamia nchini, kesi 27 dhidi ya wakiukaji wa Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki zilifunguliwa na kesi hizo zinaendelea katika Mahakama za Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Moshi na Singida. Kwa kushirikiana na Multichoice (DSTV) na polisi, kesi dhidi ya wanaokiuka taratibu za usambazaji wa matangazo zimefunguliwa katika mikoa ya Mara, Mwanza, Shinyanga, Singida na Tabora. Baadhi ya kesi hizo zimeishatolewa hukumu na watuhumiwa kulipa faini na kesi nyingine zinaendelea. Vilevile COSOTA imepokea migogoro 71 ya
hakimiliki kati ya hiyo migogoro 44 imesuluhishwa na usuluhishi wa migogoro iliyobaki bado
unaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kwa kushirikiana na COSOTA na wadau mbalimbali likiwemo Shirika la Rulu Arts Promoters kwa ufadhili wa BEST Advocacy Component na UNESCO inafanyia marekebisho Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki ya mwaka 1999. Aidha, maafisa wa COSOTA kwa kushirikiana na wataalamu wa sheria wanaendelea na zoezi la kurekebisha Kanuni za Utoaji Leseni kwa Matumizi ya Kazi za Muziki na Filamu za mwaka 2003 na kuandaa Kanuni za Ukusanyaji wa Mirabaha kutokana na uzalishaji na utoaji nakala za kazi za maandishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia Tume ya Ushindani imeendelea kusimamia ushindani kwa kudhibiti muungano wa makampuni (mergers and acquisitions) ambao unaathiri ushindani katika biashara. Kwa kipindi cha 2010/2011, Tume imepokea na kushughulikia maombi 19 ya muungano wa makampuni ikilinganishwa na maombi ya makampuni matano na yote kuridhiwa katika kipindi cha 2009/2010. Maeneo yaliyohusika ni pamoja na maduka makubwa (supermarkets), mawasiliano, mafuta ya petroli, utalii, kilimo na taasisi za fedha. Kati ya maombi 19 yaliyowasilishwa, Tume imeridhia muungano wa makampuni 13 bila masharti na makampuni mawili kwa masharti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha 2010/2011, Tume imeendelea kufanya tafiti katika sekta mbalimbali za kiuchumi kwa lengo la kubainisha masuala ya kiushindani. Kupitia utafiti, Tume huweza kubainisha masuala ya kisera, kanuni na taratibu zinazoweza kuathiri ushindani na hivyo kuiwezesha Tume kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa Sheria ya Ushindani Na. 8 ya mwaka 2003. Katika mwaka 2010/2011, Tume imekamilisha tafiti katika sekta ndogo za saruji na tumbaku na matokeo ya utafiti yanafanyiwa kazi. Aidha, Tume inaendelea kufanya tafiti katika Sekta za Ujenzi, Sukari, Kahawa, Pamba, Mbolea, Benki, Bima, Mabati, Madawa na Vinywaji Baridi.

Aidha, Tume imekamilisha utafiti katika Sekta ya Sukari. Tafiti hiyo pamoja na mambo mengine ililenga kubainisha mahusiano yaliyopo kati ya wahusika mbalimbali katika Sekta ya Sukari hususan mahusiano baina ya wazalishaji wa ndani na waingizaji wakuu wa sukari kutoka nje ya nchi ili Serikali iweza kuchukua hatua stahiki. Utafiti umebainisha kuwa makampuni yanayoingiza sukari toka nje ya nchi yanaruhusiwa pia kununua na kusambaza sukari inayozalishwa na viwanda vya ndani. Utafiti umependekeza ziwekwe taratibu za kutenganisha
wanunuzi na wasambazaji wa sukari inayozalishwa katika viwanda vya ndani na wale
wanaoagiza sukari toka nje ya nchi ili kuimarisha ushindani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2010/2011, Baraza la Ushindani (Fair Competition Tribunal - FCT) lilikuwa na kesi sita zilizokuwa zinaendelea kusikilizwa ambazo zilisajiliwa mwaka 2009/2010. Aidha, Baraza lilisajili kesi mpya kumi na moja na hivyo kufanya idadi ya kesi za kusikilizwa katika kipindi cha 2010/2011 kuwa 17. Hadi kufikia mwezi Aprili 2011, kesi 11 zilisikilizwa na kutolewa maamuzi na kesi sita zilikuwa katika hatua mbalimbali za usikilizwaji. Lengo la Baraza ni kesi kusikilizwa kwa miezi isiyozidi sita tangu tarehe ya kusajiliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Baraza la Ushindani limeweza kutekeleza malengo yake ya kujenga uwezo zaidi katika kushughulikia kesi kwa kupata mafunzo mbalimbali ndani na nje ya nchi. Mafunzo hayo yalihusisha wajumbe wote wa Baraza na Wafanyakazi watano ambapo walijifunza juu ya sekta zinazosimamiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na taratibu zinazofuatwa na Mamlaka hiyo katika kutatua migogoro. Aidha, Wajumbe wanne wa Baraza wamehudhuria mafunzo juu ya better regulation, energy, water, communications and transport kwenye taasisi ya Public Administration International (PAI) nchini Uingereza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Baraza la Ushindani limeweza kutoa elimu kwa umma juu ya kazi zake kwa njia mbalimbali kama vile kuandaa kipindi cha Lijue Baraza la Ushindani ambacho kinarushwa mara nne kwa wiki kwenye vituo vya luninga vya Shirika la Habari la Tanzania (TBC) na ITV. Katika vipindi hivyo, umma unaelimishwa pia juu ya taratibu za kufuata wakati wa kusajili na
kusikiliza kesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka 2010/2011, pamoja na kusikiliza kesi za rufaa, Wizara kupitia Baraza na Tume ya Ushindani iliweza kuchambua Sheria ya Ushindani ya mwaka 2003 na kubainisha mapungufu yanayosababisha taasisi hizo zisifanye kazi kwa ufanisi uliokusudiwa. Mapendekezo ya marekebisho ya Sheria hiyo yapo katika hatua za mwisho ili yafikishwe Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo furaha tena kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa katika kipindi cha mwaka 2010/2011, Wizara kupitia Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (CAMARTEC) ilikamilisha uundaji wa trekta dogo aina ya CFT 22 (CAMARTEC FASTRUCKTOR) lenye horse power 22 (HP22) linalofaa kwa matumizi mbalimbali (multi-purpose tractor). Tayari CAMARTEC imetengeneza matrekta sita ya awali katika karakana yake. Matrekta hayo yalifanyiwa majaribio huko Chanika, Dar es Salaam, Mlandizi Pwani, Dakawa na Gairo Morogoro na kuonesha mafanikio makubwa. Rasimu ya upembuzi yakinifu na Mpango wa Uwekezaji Kibiashara (Business Investment Plan) kwa ajili ya uzalishaji wa matrekta hayo na zana mbalimbali kibiashara vimeandaliwa. Makusudio ni kuanzisha Kampuni ya kuzalisha matrekta hayo na zana za
kilimo katika eneo la Kilimanjaro Machine Tools Complex, Moshi ifikapo Januari, 2012.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia CAMARTEC iliendelea kusimamia utekelezaji wa Programu ya Kueneza Matumizi ya Teknolojia ya Biogesi Ngazi ya Kaya (Tanzania Domestic Biogas Programme - TDBP) chini ya ufadhili wa Serikali ya Tanzania na Uholanzi. Hiyo ni Programu ya Kitaifa ya miaka mitano iliyoanza kutekelezwa mwaka 2009 kwa kushirikiana na sekta binafsi kwa madhumuni ya kuibua sekta endelevu ya Biogas kwa kujenga mitambo 12,000. Programu hii ilizinduliwa rasmi tarehe 26 Machi, 2011 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal. TDBP imeeneza mitambo 1,000 ya Biogas katika mikoa 11 ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Kilimanjaro, Manyara, Mbeya, Pwani, Ruvuma, Singida na Tanga. Aidha, waashi 490, wasimamizi 42 na watumiaji 367 wa teknolojia ya Biogas walipata mafunzo juu ya ujenzi wa mitambo, usimamizi na udhibiti wa ubora na matumizi mazuri ya teknolojia ya Biogas.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, Wizara kupitia Taasisi yake ya Uhandisi na Usanifu wa Mitambo (TEMDO) ilikamilisha ubunifu na uendelezaji wa mashine mbalimbali za kusindika kahawa, za kutengeneza bidhaa za ngozi na mtambo wa kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu ya maji. Aidha, Taasisi ya TEMDO imeendelea kuboresha mashine za kusindika matunda, asali, karanga, kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu ya upepo na kutengeneza mkaa unaotokana na taka za mbao, vumbi la mkaa na mabaki ya mimea (briquettes). Mashine hizo zilihaulishwa kupitia SIDO ambayo inazitengeneza na kuzisambaza kibiashara nchini. Vilevile mtambo wa kutengeneza briquettes ulihaulishwa kupitia Shirika la Mzinga. Mtambo wa kuzalisha
umeme kwa kutumia nguvu za upepo umefungwa Arusha kwa majaribio zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jitihada za kutoa mchango kwenye sekta ya afya na utunzaji wa mazingira, Taasisi ya TEMDO imeboresha kiteketezi cha taka ngumu zikiwemo za hospitali (solid/hospital waste incinerator). Kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), TEMDO imefunga kiteketezi hicho katika Chuo cha Mafunzo na Tiba Muhimbili, Hospitali za Mawenzi, Kibong'oto, Masama, Kisiki, Hai, Ngarenaro, Kisongo na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. Utumiaji wa viteketezi hivyo umepunguza uagizaji wa vifaa hivyo kutoka nje ya nchi na hivyo kuokoa fedha za kigeni. TEMDO itahaulisha teknolojia hiyo kupitia Shirika la Mzinga ili zitengenezwe na kusambazwa nchini kibiashara. Natoa wito kwa wazalishaji taka ngumu hususan za hatari kama za hospitali kutumia viteketezi vinavyotengenezwa na TEMDO ili kupunguza athari za uchomaji onyo wa taka hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Utafiti la Maendeleo ya Viwanda nchini (TIRDO) kwa kushirikiana na Kampuni ya Intermech ya Morogoro liliunda mashine ya kukamua na kusafisha mafuta ya mawese yenye ubora na viwango vinavyokubalika. Mashine hizo zitasaidia wazalishaji wa mafuta ya mawese kuondokana na njia zisizo na ubora katika kukamua mafuta kama vilen kutwanga, njia ambayo inapoteza muda na hutoa mafuta yasiyo na ubora. Majaribio
yaliyofanywa kwa mashine hiyo yalionesha ufanisi mzuri ambapo uwezo wa kukamua mafuta ni kilo 100 za mbegu za mchikichi kwa saa. Pia mafuta yaliyokamuliwa na kusafishwa na mashine hiyo yalipimwa na ubora wake ukabainika kuwa na viwango vya mafuta ya mawese ya kula vinavyosimamiwa na Shirika la Viwango la Tanzania (TBS).

Mheshimiwa Mwenyekiti, TIRDO imetengeneza mashine za kusindika vyakula na matunda (hammer mill, juice extractor), ambazo zimetumia malighafi zisizo na madhara kwa walaji na zinazokubalika Kimataifa kama vile chuma cha pua (stainless steel). Aidha, katika hatua ya awali Shirika limeendeleza ujenzi wa majengo ya viatamizi (incubators) vya teknohama na usindikaji wa mazao ya kilimo kwa ajili ya kuinua viwanda na wajasiriamali. Pia TIRDO imetengeneza makaushio yanayotumia teknolojia ya ukaushaji kwa kutumia jua ambapo makaushio 17 wamesambaza kwenye vijiji 17 vya mikoa ya Mtwara na Lindi chini ya ufadhili wa FAO. Vilevile Shirika limebuni kaushio kubwa linalotumia nishati ya jua lenye uwezo wa kukausha kilo 150 za muhogo kwa siku. Kaushio hilo litatumika kukaushia unga wa muhogo wenye ubora wa viwango vya Kimataifa. Majaribio yanaonesha kuwa unga unaokaushwa una kiwango cha unyevu kinachotakiwa cha asilimia 12.95 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 13 wa kiwango cha Kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la TIRDO limeendelea na shughuli za kuimarisha maabara ya mazingira ili kupata hadhi ya Kimataifa ya uhakiki (accreditation) pamoja na kuongeza vifaa vya kuboresha uwezo wa maabara wa kufanya kazi. Hiyo ni pamoja na kununua flue gas analyzer ya kisasa yenye uwezo wa kupima gesi zaidi ya kumi, kuvifanyia calibration vifaa vilivyopo na pia kurekebisha upungufu ambao umejitokeza wakati wa tathmini ya awali. Aidha, maabara imefanya ukaguzi wa ndani kabla ya tathmini kutoka kwa wakaguzi wa nje. Vilevile Shirika limechukua hatua za awali katika kuhakiki maabara ya vifaa vya kihandisi ili iweze kufikia viwango vya Kimataifa. Hatua hizo ziliwezesha utengenezaji wa machapisho ya ubora wa maabara na uboreshaji wa vifaa vya maabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la TIRDO limetoa mafunzo kwa wazalishaji bidhaa kuhusu Mfumo wa Ufuatiliaji (treaceability) kama njia ya kuhakikisha kuwa bidhaa zinazoingia katika masoko zinatimiza masharti na viwango vinavyohitajika katika masoko hayo hususan bidhaa za vyakula. Mfumo wa ufuatiliaji umeainishwa katika Sheria Na. 178/2002 ya Vyakula ya Nchi za Ulaya (EU Food Law No. 178/2002), ambayo inahitaji kila bidhaa ya chakula iweze kufuatiliwa tangu shambani hadi kwa mlaji. Hilo ni sharti kuu ambalo ni lazima litekelezwe. Katika kuwezesha bidhaa za Tanzania kuingia katika soko la Ulaya, TIRDO imetoa mafunzo kuhusu Mfumo wa Ufuatiliaji kwa wasindikaji 3,574 katika bidhaa za asali, chai, kahawa, korosho, mifugo na samaki na pia kwa viongozi wa Wizara za Kilimo, Chakula na Ushirika na Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi. Lengo ni kuimarisha na kuboresha uwezo wa wazalishaji kuweza kuzalisha bidhaa bora na salama. Pia Shirika lilisaidia wajasiriamali wa kahawa kuweza kutumia Teknolojia ya Kompyuta ya Mfumo wa Ufuatialiaji (Computerized Traceability System). Teknolojia hiyo inawasaidia wajasiriamali kuendeleza uuzaji nje mazao ya chakula na biashara kwa kufuata viwango vya
Kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kusaidia bidhaa za Tanzania kuingia katika masoko mbalimbali, Wizara kupitia TIRDO ilihamasisha sekta binafsi kuhusu umuhimu wa ufuatiliaji wa bidhaa (traceability) na matumizi ya mfumo wa utambuzi wa bidhaa wa GS1 unaotumia nembo za mistari (bar codes). Jumla ya makampuni 120 katika Kanda za Ziwa, Kusini, Kaskazini na Dar es Salaam yalihamasishwa na kufanyiwa mafunzo ya mfumo wa ufuatiliaji na mfumo wa Kimataifa wa utambuzi (GS1). TIRDO kwa kushirikiana na SIDO na sekta binafsi hususan TCCIA, TPSF, ZCCIA, ACT, CTI, TWCC na TAHA iliwezesha kukubalika kuanzishwa kwa shughuli na huduma za GS1 hapa nchini. Ninayo furaha kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa maombi hayo yamekubaliwa mwezi Mei, 2011 na maandalizi ya kuwezesha kuanza kutolewa kwa huduma hii nchini yamefikia hatua nzuri na inatarajiwa kuwa huduma hii itaanza kutolewa kabla ya kufika mwezi Septemba, 2011.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na juhudi zilizofanywa na TIRDO na wadau wengine kama ilivyoelezwa hapo awali, Tanzania imepata usajili wa GS 1 na kuruhusiwa kutumia mfumo wa utambuzi wa bidhaa (bar codes) ambao wajasiriamali wa hapa nchini wamekuwa wakiupata toka nchi za Kenya, Afrika Kusini na Denmark kwa gharama kubwa. Pia sekta binafsi watapatiwa mafunzo ya kuelewa na kutumia mifumo ya elektroniki ya biashara duniani kama vile Electronic
Product Coding (EPC) na e-commerce.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna faida nyingi za kuwa na Mfumo wa Utambuzi wa Bidhaa kwa kutumia bar codes kwani ni rahisi kujumuisha taarifa nyingi za kuwezesha kutambua bidhaa, nchi zilikozalishwa, mfumo wa uzalishaji, ubora na usalama wa bidhaa na ufuatiliaji wa bidhaa (traceability). Hivyo mfumo huo unafanya wanunuzi kuwa na uhakika wa usalama wa bidhaa wanazonunua na zinakotoka. Aidha, mfumo huo husaidia katika uboreshaji wa uthibiti wa mfumo wa usambazaji na kulinda thamani ya jina la bidhaa. Pia kiuchumi mfumo wa ufuatiliaji husaidia kuokoa biashara isiporomoke kwa kuwa na kumbukumbu bayana zilizohifadhiwa katika mlolongo wa ufuatiliaji. Mfumo huo utasaidia wazalishaji wadogo hadi wakubwa kuuza bidhaa zao kwenye maduka makubwa ya bidhaa (supermarkets) ya ndani na pia kurahisisha bidhaa zetu kupenya katika masoko ya nje ikiwa ni pamoja na yale ya kikanda (EAC na SADC) na masoko ya
kiupendeleo kama AGOA na EBA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011 TIRDO kwa kushirikiana na asasi isiyo ya Kiserikali ilihamasisha matumizi ya TEKNOHAMA na kuwasaidia wajasiriamali kupata masoko ya bidhaa za mazao ya kilimo yaliyosindikwa. Aidha, juhudi hizo zimeiwezesha TIRDO kuwafikia wajasiriamali 172 kutoka vikundi 79 katika mikoa ya Pwani, Tanga, Dar es Salaam, Mtwara na Lindi na pia kuwajengea tovuti ambazo zitatangaza bidhaa zao Kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TIRDO imetoa mafunzo yaliyolenga kuboresha bidhaa za uyeyushaji chuma kwa mafundi 13 kutoka viwanda nane. Mafunzo yalitolewa pia kwa viwanda vya kufua vyuma katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Ruvuma na Kilimanjaro na kutoa ushauri wa kitaalamu ili kuweza kuboresha bidhaa zao. Aidha, Shirika lilitoa mafunzo ya uchomeaji vyuma kwa mafundi na wajasiriamali 40 katika Manispaa ya Iringa. Vilevile Shirika katika mwaka 2010/2011 limeendelea kupima na kutoa ushauri kwa wenye viwanda kuhusu uchafuzi wa mazingira
utokanao na uzalishaji na njia za kuzuia uchafuzi huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, TIRDO imetengeneza makaushio 41 ya matunda, mboga na samaki na kusambazwa kwa njia ya kufundisha vikundi katika mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Mara, Mwanza, Mtwara na Pwani. Wajasiriamali wapatao 534 wa mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Kilimanjaro, Morogoro, Pwani na Ruvuma wamefundishwa uzalishaji wa uyoga na Shirika limetengeneza matembe 26 ya kukaushia tumbaku katika mkoa wa Ruvuma. Wajasiriamali 326 katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Iringa, Morogoro, Mtwara, Pwani, Ruvuma na Tanga wamepata mafunzo ya kusindika matunda, unga bora wa mihogo usio na sumu (cynanide) na nyanya. Mashine 25 za usindikaji zimesambazwa katika mikoa hiyo. Wazalishaji na wasindikaji katika viwanda 38 wamepewa mafunzo kuhusu Mfumo wa Ufuatiliaji (traceability) kama njia ya kuhakikisha kuwa bidhaa zinazouzwa ndani na nje ya nchi zinatimiza masharti ya viwango vya juu. Aidha, wajasiriamali 147 wa Kyela walifundishwa jinsi ya kutengeneza mafuta
bora ya mawese.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Viwanda Duniani (UNIDO) iliendelea kutekeleza majukumu yake ya kuendeleza sekta ya viwanda nchini. Moja ya maeneo yaliyofaidika ni pamoja na kujenga uwezo wa wataalamu katika masuala yanayohusu uchambuzi na maandalizi ya sera na mikakati ya maendeleo ya viwanda, kutekeleza programu ya kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya viwanda kwa kutumia mfumo wa mlolongo wa thamani, kutoa mafunzo ya teknolojia na uzalishaji wa bidhaa bora kwa wajasiriamali pamoja na teknolojia za kisasa zinazohusika na usindikaji wa mazao ya kilimo ili kuwawezesha wajasiriamali hao kukua kiteknolojia na kiuzalishaji na hivyo kuzalisha bidhaa bora zilizoongezwa thamani na zinazouzika ndani na nje ya nchi. Aidha, Shirika lilitekeleza programu mbalimbali zenye lengo la kusaidia upatikanaji wa nishati jadidifu (renewable energy) sambamba na kutoa mafunzo kwa wajasiriamali 130 na wenye viwanda juu ya uzalishaji unaozingatia uhifadhi wa mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka 2010/2011 jumla ya wajasiriamali wapatao 300 walipata mafunzo ya ubanguaji wa korosho sambamba na kupewa msaada wa mashine ndogo 240 kwa ajili ya kufanya ubanguaji wa awali wa korosho katika Wilaya za Masasi na Tandahimba mkoani Mtwara. Kupitia utaratibu wa One UN, unaotekelezwa na Mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa kutoa huduma pamoja, UNIDO ilitoa mashine za kisasa kwa ajili ya
kukamua ufuta katika Wilaya ya Ruangwa Mkoani Mtwara. Usimikaji wa mashine hizo umekamilika
na majaribio ya awali yamefanyika na kuonesha matokeo mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa uboreshaji wa nishati vijijini, programu za UNIDO ziliwezesha vijiji vinne vya mfano ambavyo ni Nyangao (Lindi), Ilagala (Kigoma), Tanga na Zanzibar kupata teknolojia na mafunzo ya utumiaji wa mitambo midogo ya uzalishaji nishati mbadala na jadidifu kwa matumizi ya uzalishaji. Aidha, mitambo midogo ya kuzalisha umeme kwa kutumia nishati ya jua, taka na mabaki ya mimea ilisimikwa katika mikoa ya Kigoma, Lindi na Tanga. Matumizi ya nishati mbadala yanawezesha uendeshaji wa miradi ya maendeleo, kusaidia kupunguza uharibifu wa mazingira pamoja na kupambana na mabadiliko ya tabia nchi (mitigate
climate change).

Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kimeongeza kiwango cha udahili kutoka jumla ya wanachuo 7,007 kwa mwaka 2009/2010 hadi kufikia wanachuo 10,704 katika mwaka 2010/2011 ambalo ni ongezeko la asilimia 53. Udahili kwa mwaka 2009/2010 kwa kila Kampasi ulikuwa ni 4,069 (Dar es Salaam), 2,108 (Dodoma) na 830 (Mwanza) ambapo kwa mwaka 2010/2011 udahili kwa kila kampasi ulikuwa ni 5,878 (Dar Es Salaam), 3,080 (Dodoma) na
1,746 (Mwanza).

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) imeendelea kuboresha Kampasi ya Dar es Salaam, ambapo ujenzi wa Jengo la Vipimo na Mizani upo katika hatua za mwisho ili kukiwezesha Chuo kudahili wanachuo wengi zaidi katika fani ya vipimo na
mizani na kuimarisha mafunzo katika fani hiyo muhimu nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuimarisha mafuzo ya vipimo na mizani kwa vitendo, Chuo kimenunua mashine na vifaa vingine kwa ajili ya maabara ya vipimo na mizani chuoni. Vifaa hivyo vimenunuliwa kupitia mradi wa Marching Grant uliokuwa ukisimamiwa na Mfuko wa Uendelezaji wa Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) ambapo jumla ya vifaa vyenye thamani ya dola za Kimarekani 197,727.04 vilinunuliwa. Aidha, Chuo kimepata vifaa mbalimbali vya kufundishia na kusomea kwa msaada wa TPSF. Vifaa hivyo ni pamoja na kompyuta 412, viti 412 na meza 206, laptop 35, projectors na projection screens 20 na viyoyozi 20. Jumla ya thamani ya vifaa hivyo ni dola za Kimarekani 865,717 sawa na shilingi 1,302,038,368.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia Shirika la TIRDO ilifanya tathmini katika viwanda vya kusindika ngozi kuhusu uchafuzi wa mazingira. Viwanda sita vya ngozi katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Kilimanjaro, Morogoro na Pwani vilitembelewa na sampuli za maji taka yanayotokana na shughuli za usindikaji wa ngozi yalifanyiwa uchunguzi katika maabara za TIRDO. Uchunguzi huo ulisaidia kubainisha viwango vya viini vya uchafuzi wa mazingira vinavyotokana na shughuli zao za uzalishaji. Ushauri ulitolewa kwa viwanda hivyo kuhusu matumizi ya teknolojia mbadala za uzalishaji zinazozingatia utunzaji wa mazingira. Vilevile kwa kupitia maonesho ya Kitaifa kama Wiki ya Viwanda Duniani, Sabasaba na Nanenane Wizara imeendelea kutoa elimu na mafunzo juu ya Sera ya Taifa ya Mazingira, Sheria ya Usimamizi wa Mazingira pamoja na Kanuni zake kwa wadau wa Sekta ya Viwanda kwa lengo la kuzijua na kuzitekeleza. Aidha, Wizara imeendelea kushiriki katika kufanya tathmini ya mazingira katika miradi mipya ya viwanda pamoja
na miradi iliyoanzishwa bila kufanya tathmini hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, Wizara iliendelea na jitihada za kutoa mafunzo kuhusu mbinu za kupambana na kuthibiti rushwa. Elimu hiyo ilitolewa kwa umma kupitia maonesho mbalimbali ya Kitaifa kama vile Sabasaba, Nanenane na Wiki ya Utumishi wa Umma. Pia mafunzo yalitolewa kupitia vikao vya idara, vitengo na taasisi zake ambayo hufanyika kwa wastani kila mwezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka 2010/2011, watumishi waliothirika na UKIMWI walipata mafunzo ya jinsi ya kutunza afya zao. Pia Wizara iliendelea kutoa huduma ya lishe, virutubisho (food supplements) na usafiri kwa waathirika waliojitokeza. Taasisi zote zilizo chini ya Wizara ziliendelea kukumbushwa umuhimu wa kujali afya za wafanyakazi likiwemo suala la elimu mahala pa kazi ya kupambana na maambukizi mapya ya UKIMWI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2010/2011, Wizara ilikuwa na jumla ya watumishi
213 waliokuwa kwenye orodha ya mishahara na iliajiri watumishi wapya watatu ambao walipangwa na Sekretarieti ya Ajira. Hata hivyo, kutokana na ufinyu wa Bajeti ya Serikali, Wizara haikufikia malengo yake iliyojiwekea ya kuajiri watumishi kumi na nane kulingana na ikama ya mwaka 2010/2011.

Aidha, kwa kipindi hicho Wizara iliwapandisha vyeo watumishi 11 ili kujaza nafasi mbalimbali kwa lengo la kukidhi Miundo ya Utumishi (Scheme of Service) na pia kuziba nafasi zilizoachwa wazi kutokana na kustaafu utumishi wa umma, kuacha kazi na kuhamishwa. Katika kipindi hicho hicho, Wizara iliweza kusomesha jumla ya wafanyakazi 25 kulingana na Mpango wa Mafunzo wa Wizara. Kati ya hao, 15 walikwenda mafunzo ya muda mrefu na kumi ya muda mfupi kwenye vyuo vya ndani na nje ya nchi. Vilevile Wizara ilitumia mfumo wa wazi wa mapitio na tathimini ya utendaji kazi kwa watumishi (Open Performance Appraisal System-OPRAS) wakati wa
kupandisha vyeo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa Mipango ya Sekta ya Viwanda, Biashara, Masoko na Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo, zipo changamoto za jumla zilizojitokeza wakati wa utekelezaji na uendeshaji wa sekta hii ambazo zinahitaji ushirikishwaji wa sekta mbalimbali ili kufikia malengo yaliyokusudiwa. Changamoto zinazoikabili Wizara hii ni Wizara na taasisi zake kutengewa na kupata fedha za kutosha kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yake, upatikanaji wa fedha za fidia kwa maeneo yaliyobainishwa kwa ajili ya uwekezaji chini ya EPZA, upatikanaji wa umeme wa uhakika na maji, kuwa na miundombinu imara kama vile barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege, mifumo ya taarifa, maghala na cold rooms kwa ajili ya usafirishaji wa malighafi, bidhaa na nyenzo yenye kuwezesha sekta shindani ya viwanda na biashara na kukabiliana na msukosuko wa soko la mitaji, soko la fedha na uchumi wa
dunia ambayo kwa kiasi kikubwa imesababisha upungufu wa uwekezaji na mauzo nje.

Pia kuwezesha upatikanaji wa mitaji na teknolojia sahihi kwa ajili ya kuongeza uzalishaji, usindikaji na kuongeza thamani na ubora wa mazao na bidhaa zitakazowezesha kuhimili ushindani katika soko la ndani na nje, kuwezesha upatikanaji wa wataalamu bingwa na wa kutosha katika nyanja za viwanda, biashara, masoko na viwanda vidogo na biashara ndogo, kuimarisha Taasisi za Utafiti na Maendeleo ya Viwanda, Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo, Biashara na Masoko, kuwezesha ushindani wa haki katika soko, utoaji wa elimu ya biashara na ujasiriamali kwa Watanzania walio wengi, upitiaji wa Sheria zilizopitwa na wakati na kusimamia utekelezaji wake na upatikanaji wa masoko ya uhakika na yenye masharti nafuu kwa bidhaa na huduma zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya uwekezaji na kufanya biashara.

Katika mwaka 2011/2012, malengo ya sekta ya viwanda, biashara, masoko na viwanda vidogo na biashara ndogo ni pamoja na kuweka kipaumbele katika utekelezaji na ukamilishaji wa
yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2011/2012, malengo ya sekta ya viwanda ni kuendeleza uhamasishaji wa uwekezaji na kutoa kipaumbele kwa viwanda vinavyoongeza thamani mazao ya kilimo, kuendeleza utekelezaji wa Mkakati Unganishi na Mpango Kamambe wa Kuendeleza Sekta ya Viwanda Nchini hususan kuandaa miradi na mikakati ya sekta ndogo za viwanda, kuhamasisha uanzishaji wa viwanda vipya vya kusindika ngozi na bidhaa za ngozi. Hii itakwenda na programu mahsusi inayolenga kujenga miundombinu (industrial villages/clusters) itakayowezesha viwanda vidogo na vya kati SME kuongeza uzalishaji wa bidhaa za ngozi nchini na kuendeleza utoaji wa mafunzo ya kuongeza tija, ufanisi na ubora wa bidhaa za viwanda ikiwa ni pamoja na uzalishaji unaozingatia hifadhi na kulinda mazingira katika shughuli za uzalishaji bidhaa viwandani.

Pia kuendelea na ushiriki katika ukamilishaji wa Sera na Mkakati wa Maendeleo ya Viwanda ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na nchi wanachama wa Jumuiya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), kuanza maandalizi ya awali ya kufanya sensa ya viwanda Tanzania. Sensa kama hiyo kwa mara ya kwanza ilifanyika mwaka 1989. Wizara kwa
kushirikiana na UNIDO, Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), sekta binafsi na wadau wa maendeleo itaendelea na majadiliano ya kuona namna ya kutekeleza kazi hiyo ifikapo mwaka 2013 na kuendelea na utekelezaji wa miradi ya kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe ya Mchuchuma na chuma ghafi na chuma cha pua kwa kutumia chuma cha Liganga ambapo uchorongaji na uandaaji wa upembuzi yakinifu utaanza mwaka huu wa fedha, ujenzi wa Mgodi wa Chuma, Mgodi wa Makaa ya Mawe na Kiwanda cha kuzalisha chuma ghafi (sponge iron) unatarajiwa kuanza mwaka 2012 na uzalishaji wa chuma ghafi unatarajiwa kuanza mwaka 2013.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuendelea na utekelezaji wa mradi wa kasi mpya, ikiwa ni pamoja na kukamilisha uchorongaji na upembuzi yakinifu ifikapo Desemba, 2011 na kuanza ujenzi wa Mgodi wa Chuma, Mgodi wa Makaa ya Mawe na Kiwanda cha kuzalisha chuma ghafi mwaka 2012, kuendelea na utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe wa Ngaka Kusini (Mbalawala na Mhukuru huko Mbinga) na kuendelea na ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza dawa za kibaiolojia za kuua viluwiluwi vya mbu wa Malaria (TAMCO - Kibaha).

Pia kuendelea na usindikaji mazao ya kilimo (agro-processing of rubber, sweet sorghum, meat processing), kupitia NDC ambayo imejipanga kutekeleza miradi hiyo kwa njia ya ubia kati yake, wawekezaji na wakulima wadogo, kuendelea na utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme kutokana na upepo huko Singida, kukamilisha zoezi la ubainishaji wa maeneo ya EPZ na SEZ katika Mikoa mitatu iliyobaki ya Dodoma, Rukwa na Tabora, kukamilisha taratibu za uanzishaji Mfumo wa Kituo cha Utoaji Huduma (One Stop Service Centre) kwa wawekezaji katika eneo la Benjamin William Mkapa Special Economic Zone, kukamilisha uandaaji Mfumo wa SEZ, ili usajili wa wawekezaji kupitia mfumo huo uanze kutumika na kukamilisha uandaaji wa Mpango Kamambe (Master Plan) katika eneo la kipaumbele la Bagamoyo SEZ na kuanza ujenzi wa miundombinu ya
msingi kwa kushirikiana na sekta binafsi.

Pia kuendelea na uhamasishaji wa wawekezaji wa kujenga miundombinu na wa kujenga viwanda vya kuzalisha bidhaa katika maeneo ya EPZ na SEZ na kwa kushirikiana na UNIDO kuendelea kusaidia maendeleo ya sekta ya viwanda kwa kutoa kipaumbele katika mafunzo yanayolenga kuongeza ujuzi kwa wazalishaji, kusaidia utambuzi wa teknolojia sahihi za uzalishaji, uhaulishaji wa teknolojia, uchambuzi wa sera, uendelezaji wa nishati jadidifu, biashara na
upatikanaji wa masoko, taarifa za viwanda na usimamizi wa Sera ya Viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2011/2012, malengo ya sekta ya viwanda vidogo na biashara ndogo ni kuendeleza zoezi la uperembaji na tathmini ya utekelezaji wa sera ya viwanda vidogo na biashara ndogo, kuongeza kasi ya upatikanaji na usambazaji taarifa zinazohusiana na sekta ya viwanda vidogo na biashara ndogo, kujenga uwezo wa kutoa huduma za ugani katika maeneo walioko wajasiriamali hasa vijijini, kutafuta utaratibu wa kuzalisha kwa wingi teknolojia zinazofaa na kuzisambaza kwa watumiaji, kutoa ujuzi maalumu wa kuzibadilisha rasilimali hasa mazao ya kilimo, misitu na mifugo kuwa bidhaa, kujenga miundombinu itakayowafanya wajasiriamali hasa wa vijijini kupata sehemu za kufanyia kazi na kujenga misingi
ya kusaidia utengenezaji wa bidhaa mpya kutokana na mawazo ya wajasiriamali.

Pia kutoa elimu ya ujasiriamali na usimamizi wa biashara, kuwawezesha wazalishaji wadogo kupata masoko ya bidhaa na huduma kwa kutengeneza miundombinu ya kupokea na kusambazia habari za kibiashara na kutengeneza sehemu za kuonesha bidhaa zao, kutoa huduma za kifedha ikiwa ni pamoja na ushauri na mikopo pale itakapodhihirika kuhitajika na
kujenga uwezo wa uzalishaji wa zana za kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2011/2012, malengo ya sekta ya biashara ni kuendelea kusimamia na kutekeleza Mikataba na Itifaki mbalimbali ambayo Tanzania imeridhia chini ya makubaliano kati ya nchi na nchi (bilateral), kikanda na ile ya Kimataifa, kutoa mafunzo kwa Maafisa Biashara wa Wilaya, Manispaa na Majiji kuhusu fursa za masoko ya nje ikiwa ni pamoja na sheria na kanuni za kuingia masoko hayo hususan yale ya upendeleo yanayotolewa chini ya mpango wa AGOA, EBA, nchi kama Canada, China, India na Japan na yale ya Kikanda na Kimataifa kwa mfano SADC na EAC, kusimamia taratibu na sheria za biashara chini ya
makubaliano ya WTO ikiwa ni pamoja na maadili ya ushindani katika uchumi ili kuliwezesha Taifa kuhimili changamoto za biashara ya Kimataifa na kuweka sera, sheria, kanuni na taratibu za kukuza na kuimarisha ulinzi na haki za uvumbuzi na ubunifu (intellectual property rights) na kuendelea kuimarisha mahusiano kati ya nchi na nchi (bilateral), kikanda na yale ya kimataifa kwa lengo la kuendelea kukuza fursa za masoko kwa bidhaa zetu.

Pia kutekeleza Mkakati Maalumu wa Kukuza Mauzo Nje (Export Development Strategy - EDS), kuongezea thamani mazao, bidhaa na huduma nje ya nchi ili kukuza uchumi na kupunguza umaskini, kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Biashara ili kuhakikisha inaendana na mfumo wa utandawazi katika nyanja za kibiashara, kuendelea kuimarisha vituo vya Biashara vya Tanzania vilivyopo London na Dubai na kupeleka Waambata wa Biashara nchini China na Marekani, kuendeleza majadiliano ya Ubia wa Uchumi kati ya EAC na EU na kuendelea kushiriki majadiliano ya kuanzishwa kwa Eneo Huru la Biashara la Kanda za COMESA, EAC na SADC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2011/2012, malengo ya sekta ya masoko ni kukamilisha mkakati wa mfumo mpana na unganishi wa taarifa za masoko unaolenga kukuza biashara ya ndani na mauzo nje, kukusanya, kuhifadhi, kuchambua na kusambaza taarifa za masoko kwa wadau kwa njia za kisasa zaidi ili kuwajengea uwezo wazalishaji na wafanyabiashara kuzalisha zaidi na kuuza katika masoko yenye bei shindani, kuendeleza vituo vya pamoja vya mipakani vya Tunduma/Nakonde na Kabanga/Kobero, kuendelea kuboresha miundombinu ya masoko hususan masoko, magulio, maghala na barabara za vijijini, kuendelea kuboresha
mazingira ya biashara nchini na kuanzisha soko la bidhaa.

Pia kukuza matumizi ya mfumo wa utambuzi wa bidhaa kwa kutumia nembo za mistari (bar codes) unaoratibiwa na Shirika la Kimataifa la GS1 lenye Ofisi zake huko Brussels Ubelgiji, kuendeleza matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za Mazao Ghalani, kutekeleza Sheria ya Usajili wa Shughuli za Biashara (BARA), kufanya tafiti za masoko ya mazao na bidhaa na kutangaza bidhaa
za Tanzania kupitia maonesho ya ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2011/2012, Mamlaka ya Biashara Tanzania
(TanTrade) itafanya yafuatayo:-

Kwanza kuendelea na utafiti wa mfumo wa biashara ya ndani katika Mikoa na Wilaya zote nchini ili kuandaa mapendekezo yatakayowezesha kuundwa kwa Mfumo wa Masoko wa Kitaifa utakaosaidia kuongeza uzalishaji na kuwa na masoko endelevu ya bidhaa hapa nchini. Pili, kuendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo Wajasiriamali katika vituo vya Zanzibar na Mwanza.

Tatu, kuratibu uandaaji wa Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, Maonesho ya Kisekta, Tamasha la miaka 50 ya Uhuru, pamoja na uratibu wa maonesho ya kimataifa na nchi za Kenya, Rwanda, Malawi na China na nne, kuimarisha Ofisi ya Zanzibar ili
iweze kusaidia juhudi za kukuza sekta ya biashara Visiwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2011/2012, Tume ya Ushindani
imepanga kutekeleza yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kutangaza shughuli za Tume kwa umma ili kuongeza compliance, pili, kumuelimisha na kumlinda mlaji, tatu, kuboresha elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari kama radio, luninga na magazeti kuhusiana na bidhaa bandia na madhara yake kwa binadamu na mali zake, nne, kupambana na kudhibiti makampuni yanayokula njama kwa pamoja kwa kupanga bei, na kwa kudhibiti kiasi cha bidhaa inayopelekwa kwenye soko (output restrictions between competitors) na nne, kufanya uchunguzi wa masoko na kusikiliza kesi
za ushindani.

Tano, kufuatilia na kuidhinisha muungano wa makampuni, sita kuongeza mafunzo kwa rasilimali watu wa Tume jinsi ya kutumia mifumo mbalimbali kama ASCUDA++(TRA) na IPM tool (WCO) ili kuwezesha Tume ya Ushindani kupambana na bidhaa bandia kwa ufanisi zaidi, saba, kuboresha mahusiano na Taasisi nyingine za Serikali kama TRA, TFDA, Polisi, TBS na Ofisi ya Mawanasheria Mkuu wa Serikali kupitia vikao vitakavyopangwa na Tume kwa mujibu wa Kanuni
ya Alama za Bidhaa ya mwaka 2008 na kukamilisha marekebisho ya Sheria ya Ushindani ya mwaka 2003.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka 2011/12, Baraza la Taifa la Utetezi wa
Mlaji litatekeleza yafuatayo:-

(i) Kusimamia maslahi ya mlaji kwa kupeleka maoni yake kwenye Tume ya Ushindani,
Mamlaka za Udhibiti na Serikali kwa ujumla;

(ii) Kuendelea kupokea na kusambaza habari na maoni yenye maslahi kwa mlaji;

(iii) Kuanzisha Kamati za Mlaji za Mikoa na Sekta na kushauriana na kamati hizo; na

(iv) Kushauriana na wenye viwanda, Serikali na jumuiya nyingine za walaji katika mambo
yenye maslahi kwa mlaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2011/2012, Baraza la Ushindani
litatekeleza yafuatayo:-

(i) Kusikiliza kesi za rufaa zinazotokana na mchakato wa Ushindani katika soko na Udhibiti
wa Bidhaa na Huduma;

(ii) Kujenga uwezo zaidi wa Baraza katika kushughulikia kesi hizo;

(iii) Kutoa elimu kwa umma juu ya kazi za Baraza katika Uchumi; na

(iv) Kwa kushirikiana na Tume ya Ushindani, kukamilisha marekebisho ya Sheria ya
Ushindani ya mwaka 2003.

Mheshimiwa Mwenyekiti, malengo ya Shirika la Viwango kwa mwaka 2011/2012 ni:-

(i) Kutoa mchango muhimu katika sekta ya ufungashaji wa bidhaa kupitia Kituo cha
Ufungashaji (Packaging Technology Centre) ambacho kwa sasa hivi kiko katika hatua ya majaribio ya awali. Kituo kitatoa mafunzo ya huduma za kupima sampuli za viwanda vya ufungashaji kwa lengo la kuongeza ubora wa bidhaa zinazozalishwa hapa nchini na kuhakiki
vifungashio (packaging materials) kwa bidhaa zile zinazotoka nje ya nchi;
(ii) Kuendelea na juhudi za kuhakikisha kwamba maabara zote za Shirika zinapata vyeti vya umahiri (laboratory accreditation) ili kuongeza kukubalika kwa bidhaa za Tanzania katika soko
la kimataifa;

(iii) Kuanza utekelezaji wa utaratibu wa kupima ubora wa bidhaa zote mahali zinapotoka kabla ya kuingia nchini (Preshipment Verification of Conformity to Standards - PVoC). Utaratibu
huo utasaidia Tanzania isiwe jalala la bidhaa hafifu kutoka nje ya nchi;

(iv) Kushirikiana kwa karibu na vyombo vingine vya Serikali vikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Mkemia Mkuu wa Serikali, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Tume ya Ushindani (FCC) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) ili kuhakikisha kuwa
bidhaa zinazoingia nchini ni zenye ubora unaokubalika;

(v) Kuongeza idadi ya utoaji wa leseni kutoka leseni 100 kwa mwaka hadi kufikia leseni 120
katika mwaka 2011/2012;

(vi) Kuendelea kutoa mafunzo kwa wajasiriamali nchini kote kuhusu viwango vya udhibiti wa ubora wa bidhaa na vyeti vya ubora wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje zinatarajiwa kuwa
2,800 kwa mwaka 2011/2012; na

(vii) Kuendelea na upimaji sampuli za bidhaa mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Malengo ya Wakala wa Vipimo kwa mwaka 2011/2012 ni:-

(i) Kuanza uhakiki wa vipimo vingine vinavyotumika kwa biashara kama vile mita za
umeme, mita za maji na mitungi ya gesi ya kupikia;

(ii) Kuimarisha Kitengo cha Vipimo Bandarini (WMA Ports Unit) ili kiweze kutoa huduma kwa
makampuni yanayoagiza mafuta kwa ufanisi zaidi;

(iii) Kuendelea kukagua usahihi wa bidhaa zilizofungashwa (quantities in pre-packed
goods) zinazozalishwa na viwanda vya hapa nchini na pia kutoka nje ya nchi;

(iv) Kufanya upembuzi yakinifu kwa mradi wa ujenzi wa Jengo la Wakala (Vipimo House) ambalo litakuwa na ofisi za Makao Makuu ya Wakala, maabara za kisasa, na pia litatumika kama
kitega uchumi;

(v) Kufanya upembuzi yakinifu kwa mradi wa ujenzi mpya na wa kisasa (eneo la kupimia
magari yanayosafirisha mafuta) katika eneo la Wakala huko Misugusugu, Pwani;

(vi) Kukamilisha taratibu za utungaji wa Sheria mpya ya Vipimo (Legal Metrology Act) ili kukidhi matakwa ya sasa ya biashara na pia kuzingatia maridhiano yaliyofikiwa na nchi kikanda
na kimataifa kuhusu masuala ya vipimo;

(vii) Kukamilisha taratibu za kusitisha matumizi ya mizani ya rula (steel yard) katika ununuzi
wa zao la pamba;

(viii) Kuendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa kuongeza vitendea kazi ikiwa ni pamoja na ununuzi wa vifaa vya kitaalam na vyombo vya usafiri imara na vya kutosha kwa ofisi zote ili kuhakikisha huduma za Wakala zinawafikia walaji/wadau wengi zaidi, kwa haraka na ufanisi zaidi;
na

(ix) Kutekeleza programu ya elimu kwa umma ili kuongeza uelewa wa matumizi ya vipimo sahihi kwa wananchi wengi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Malengo ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni kwa mwaka
2011/12 ni kama ifuatavyo:-

(i) Kukamilisha uingizaji wa taarifa zote za makampuni na majina ya biashara kwenye mfumo wa kompyuta ili kurahisisha na kuboresha taratibu za utoaji wa huduma kwa kutumia
mifumo ya kiteknolojia;

(ii) Kupanua wigo wa watumiaji wa huduma na kupeleka huduma hizo karibu na wateja. BRELA kwa kushirikiana na TCCIA itatekeleza mpango wa kutoa baadhi ya huduma zake wilayani;

(iii) Kuhamasisha na kuelimisha watumishi na watumiaji wa huduma za Wakala, ili
kuharakisha urasimishaji wa biashara;

(iv) Kuendeleza elimu juu ya umuhimu wa matumizi bora ya Miliki Ubunifu ili kuwawezesha wananchi kutumia fursa zilizopo katika rasilimali hizo kukuza uchumi wao na kupambana na
umaskini;
(v) Kukamilisha upitiaji wa sheria za Miliki Ubunifu, Majina ya Biashara, Leseni za Viwanda na kuendelea na utekelezaji wa Sheria ya Makampuni ya mwaka 2002, ili iweze kwenda na
mabadiliko yanayoendelea sasa hivi duniani;

(vi) Kuendelea na mpango wa kuandaa Mfumo Mkakati wa Miliki Ubunifu Tanzania
(Intellectual Property Strategy Framework);

(vii) Kuimarisha ushirikiano uliopo katika eneo la miliki ubunifu na mashirika ya nje kama
vile Shirika la Miliki Ubunifu la Kanda ya Afrika (African Regional Intellectual Property Organization - ARIPO), Shirika la Miliki Ubunifu la Dunia (The World Intellectual Property Organization - WIPO) na
Shirika la Biashara Duniani (World Trade Organization - WTO);

(viii) Kuimarisha ushirikiano baina ya nchi na nchi (bilateral arrangements) katika maeneo
ya Miliki Ubunifu na maeneo mengine ambayo BRELA inayasimamia;

(ix) Kutekeleza Sheria ya Usajili wa Shughuli za Biashara (BARA) kwa kushirikiana na
Mamlaka za Serikali za Mitaa (Local Government Authority); na

(x) Kupata kiwanja au jengo kwa ajili ya Ofisi za Wakala kwa ajili ya utoaji huduma na kuiwezesha Wakala kutumia teknolojia ya kisasa katika kutoa huduma zake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Katika Kipindi cha mwaka 2011/2012, COSOTA imejipanga
kutekeleza yafuatayo:-

(i) Kuhamasisha masuala ya Hakimiliki, na kutumia kila nafasi ya kushirikiana na vyombo
vya habari katika uhamasishaji;

(ii) Kuanzisha matumizi ya stika zenye namba, zijulikanazo kama HAKIGRAM, katika usambazaji wa kanda na CD za kazi za muziki na Filamu, ili kuwawezesha wanunuzi wa kazi hizo
kutofautisha kati ya kazi halali na bandia;

(iii) Kutoa elimu kwa wauzaji wa kanda na wanunuzi kuhusu CD na mikanda bandia;

(iv) Kusajili makampuni ya uzalishaji na usambazaji wa kanda na CD, uchapishaji na
mashirika ya utangazaji yaliyopo ili kutoa miongozo ya kufanya kazi kwa mujibu wa Sheria ya
Hakimiliki;

(v) Kukusanya mirabaha na kutoa leseni kwa mashirika ya utangazaji, mabenki na
makampuni ya simu;

(vi) Kuandaa marekebisho ya Sheria ya Haki Miliki na Haki Shirikishi ya mwaka 1999;

(vii) Kuendelea kusuluhisha migogoro na kufungua kesi dhidi ya wakiukaji wa Sheria na
wanaogoma kulipia mirabaha;

(viii) Kurekebisha viwango vya mirabaha ili viweze kulipika na kuendana na wakati; na

(ix) Kufanya mikutano na vyama vya wafanyabiashara mikoani juu ya utekelezaji wa
Sheria ya Hakimiliki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2011/2012, Bodi ya Leseni za Maghala
itatekeleza yafuatayo:-

(i) Kusimamia na kuratibu utekelezaji wa Mfumo wa Stakabadhi za Maghala katika
maeneo yote yanayotekeleza mfumo hapa nchini;

(ii) Kukuza matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi katika maeneo na mazao mengine;

(iii) Kuimarisha mfumo ili utumike kikamilifu katika soko la bidhaa (commodity exchange);

(iv) Kutoa elimu ya Mfumo wa Stakabadhi za Leseni Ghalani kwa wakulima na wadau
wengine;

(v) Kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuendeleza ujenzi wa maghala ya kuhifadhia
mazao; na

(vi) Kuhamasisha taasisi za fedha kutoa mikopo ya ununuzi wa mazao kupitia Mfumo wa
Stakabadhi za Mazao Ghalani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka 2011/2012, taasisi za utafiti zilizo chini
ya Wizara (CAMARTEC, TIRDO na TEMDO) zimejipanga kutekeleza yafuatayo:-

(i) Kuendeleza uboreshaji, uundaji na uanzishwaji wa uzalishaji kibiashara wa matrekta madogo aina ya CFT 22 na zana zake; kuendesha mafunzo kwa mafundi, waendesha matrekta
na wasimamizi wao;

(ii) Kuendeleza utafiti wa ufuaji umeme kwa kutumia teknolojia ya biogas;

(iii) Kuendeleza uundaji wa mashine za kusindika mazao ya kilimo;

(iv) Kuendelea na uhaulishaji wa teknolojia mbalimbali zilizobuniwa na taasisi za utafiti. Hii
itatekelezwa sambamba na kutoa huduma katika viatamizi vilivyopo kwenye taasisi za utafiti;

(v) Kutoa mafunzo na kuhamasisha wajasiriamali kwa kutumia viatamizi vya teknolojia
mbalimbali;

(vi) Kubuni na kuendeleza machinjio ya kisasa yenye gharama nafuu pamoja na
teknolojia za kuongeza thamani ya bidhaa zitokanazo na mabaki ya mifugo;

(vii) Kubuni na kuendeleza teknolojia za kurejesha taka za mijini (municipal solid waste
recycling technologies);

(viii) Kuendeleza utoaji huduma za kihandisi viwandani kwa lengo la kuongeza uzalishaji,
ubora wa bidhaa, kuhifadhi mazingira na matumizi bora ya nishati;

(ix) Kuendelea kuhamasisha matumizi ya teknolojia ya kisasa ili viwanda vya ngozi nchini
vipunguze uchafuzi wa mazingira;

(x) Kukamilisha mchakato wa kuhakiki na kuboresha maabara ya mazingira na ya vifaa vya kihandisi ili viweze kufikia viwango vya kimataifa na kuweza kutoa huduma bora kwa
wazalishaji viwandani;

(xi) Kutekeleza mfumo wa ufuatiliaji wa mazao (traceability);

(xii) Kuendelea kusaidia utendaji wa Kampuni ya GS 1 kama mshauri wa kiufundi chini ya
uendeshaji wa sekta binafsi; na
(xiii) Kuendelea kutoa huduma viwandani zinazolenga matumizi ya TEKNOHAMA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2011/2012, Chuo cha Elimu ya Biashara kinalenga
kutekeleza yafuatayo:-

(i) Kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa wajasiriamali wadogo wadogo ili kuwasaidia
kufanya biashara zao kisasa zaidi;

(ii) Kuaandaa mpango wa kuendesha mafunzo kwa wajasiriamali katika Kampasi zake za
Dodoma na Mwanza ili kuwafikia wajasiliamali wengi;

(iii) Kuandaa mitaala ya kozi ya ujasiriamali katika ngazi ya Astashahada, Stashahada na
Shahada; na

(iv) Kuandaa michoro katika kiwanja cha Nzunguni (Dodoma) na Kiseke (Mwanza).

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2011/2012 Wizara itaendelea kutekeleza mikakati
inayohusu masuala ya utunzaji wa mazingira pamoja na programu ya utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi na Utunzaji wa Mazingira viwandani na taasisi za Sekta ya Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka 2011/2012, Wizara itaendelea kupambana na kudhibiti rushwa kwa kutoa elimu kwa umma na kubaini mianya ya rushwa kwa lengo la kuiziba. Elimu hiyo itatolewa kupitia vikao mbalimbali vya Wizara na Taasisi zake na maonesho mbalimbali ya kitaifa kama vile Wiki ya Utumishi wa Umma, Sabasaba na Nanenane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2011/2012 tutaendelea kutoa mafunzo juu ya kujikinga na maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI na kuhamasisha upimaji wa afya za wafanyakazi kwa hiari. Pia, tutaendelea na jitihada za kuwawezesha wafanyakazi waishio na virusi
vya UKIMWI kupata huduma ya virutubisho (food suplements) lishe na usafiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha ujao wa 2011/2012, Wizara inatarajia kuajiri watumishi 80 kwa kada mbalimbali ili kuziwezesha idara na vitengo vyote kutoa huduma nzuri na kwa ukamilifu. Pia Wizara inatarajia kuwathibitisha kazini watumishi watatu na kuwapandisha vyeo jumla ya watumishi 67 baada ya kupima utendaji kazi wao kupitia OPRAS na kuzingatia muundo wa Utumishi wa Umma (scheme of service).

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzishukuru nchi rafiki na Mashirika ya Kimataifa ambao wametoa misaada mbalimbali kusaidia Wizara yangu. Misaada na michango yao imechangia kwa kiasi kikubwa Wizara yangu kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na tija. Nchi hizo ni pamoja na Austria, Canada, China, Denmark, Finland, India, Ireland, Japan, Korea ya Kusini, Marekani, Norway, Sweden, Uholanzi, Uingereza, Ujerumani na Uswisi. Aidha, Mashirika ya Kimataifa ni pamoja na ARIPO, Benki ya Dunia, CFC, DANIDA, DFID, EU, FAO, IFAD, JICA, Jumuiya
ya Madola, KOICA, SIDA, UNCTAD, UNDP, UNIDO, USAID, WIPO na WTO.

Maombi ya fedha katika mwaka 2011/2012, Matumizi ya Kawaida katika mwaka 2011/2012 Wizara na Taasisi zilizo chini yake inaomba kutengewa jumla ya shilingi 30,052,589,000 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida ili iweze kutekeleza majukumu niliyoelezea ya kuendeleza sekta ya viwanda, viwanda vidogo na biashara ndogo, biashara na masoko. Kati ya fedha hizo, shilingi 21,503,769,000 ni kwa matumizi ya mishahara na shilingi 8,548,820,000 kwa ajili ya Matumizi ya
Kawaida ya Wizara na Taasisi zake.

Katika mwaka 2011/2012 Wizara inaomba jumla ya shilingi 27,676,129,000 kwa ajili ya shughuli za Miradi ya Maendeleo katika Wizara na Taasisi zake. Kati ya fedha hizo shilingi 16,387,859,000 ni fedha za ndani ambazo zitatumika katika shughuli za maendeleo katika taasisi zilizo chini ya Wizara na shilingi 11,288,270,000 ni fedha za nje kutoka kwa Washirika wa Maendeleo.


Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.
Hon. Samuel John Sitta Contribution
WAZIRI WA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHIRIKI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.
Hon. George Boniface Taguluvala Simbachawene Contribution
MWENYEKITI:
Ahsante sana Waziri wa Viwanda na Biashara Mheshimiwa Dkt. Cyrill Chami kwa hotuba yako. Sasa nitamwita Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda na Biashara. Mheshimiwa
Mahmoud Mgimwa.
Hon. Mahmoud Hassan Mgimwa Contribution
MWENYEKITI WA KAMATI YA VIWANDA NA BIASHARA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kusoma maoni ya Kamati naomba Bunge lako Tukufu
kuongeza dakika 30 zilizotumika kwenye Miongozo.

Naomba utumike kwa wajumbe kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Kanuni Na. 99 (7) na 114 (11) Toleo la mwaka 2007, naomba kuwasilisha maoni na ushauri wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda na Biashara kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2010/2011, pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa
mwaka wa fedha 2011/2012.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uzima, afya na kuniwezesha kuwasilisha maoni haya mbele ya Bunge lako Tukufu. Kabla sijawasilisha maoni ya Kamati, naomba nichukue fursa hii kukushukuru wewe binafsi kwa kunipa fursa hii ili
niweze kuwasilisha maoni ya Kamati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mkosefu wa fadhila kama sitawashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Mufindi Kaskazini kwa kunichagua kwa kauli moja kuwa Mbunge wao na kwa ushirikiano mkubwa wanaonipatia katika kutekeleza majukumu yangu kama Mbunge, nawaahidi
kuwa nitajitahidi kwa kadri ya uwezo wangu wote kuwatumikia na wala sitawaangusha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee nitoe shukrani zangu za dhati kwa wanakamati kwa kunichagua kuwa Mwenyekiti wao kwa sauti moja na kwa ushirikiano mkubwa wanaonipatia bila kujali itikadi za vyama vyetu, pia namshukuru Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Engineer Stella Manyanya, kwa ushirikiano anaonipa na kwa namna ya kipekee namshukuru sana Waziri Kivuli Mheshimiwa Lucy Owenya, kwa ushirikiano wake mkubwa katika Kamati yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni na ushauri wa Kamati uliotolewa kwa Wizara kwa mwaka 2010/2011. Katika mwaka wa fedha uliopita Kamati ya Viwanda na Biashara ilitoa maoni, ushauri na mapendekezo 11. Nasikitika kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba kwa kiasi kikubwa Serikali haijatekeleza maagizo ya Kamati. Hivyo Kamati yangu inaendelea kusisitiza na kuagiza Serikali
kutekeleza maagizo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka wa fedha 2010/2011 Wizara iliidhinishiwa na Bunge, kiasi cha shilingi 64,260,505,500/=, kati ya fedha hizo fhilingi 31,542,839,000/= ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na shilingi 32,717,666,500/= ni kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo. Hata hivyo mpaka kufikia mwezi Aprili 2011, Wizara ilipokea shilingi 13,303,713,331/= tu kwa ajili ya Maendelao, ambayo ni sawa na asilimia 41% tu ya fedha yote ya Maendeleo ambayo iliidhinishwa na Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni mapungufu makubwa sana na athari zake kiuchumi ni kubwa, Kamati yangu inaiagiza Serikali kuipa Wizara ya Viwanda na Biashara fedha yote
inayoidhinishwa na Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yangu ilipokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na taasisi zilizo chini yake kwa mwaka wa fedha 2010/2011 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2011/2012, tarehe 31/5 hadi 2/6/2011 Jijini Dar es Salaam, iliyowasilishwa na Mheshimiwa
Dkt. Cyril Chami, Waziri wa Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika taarifa hiyo Waziri alieleza kuhusu mambo yafuatayo:-

(i) Dira, dhima na majukumu ya Wizara;

(ii) Utekelezaji wa maagizo ya Kamati yaliyotolewa wakati wa kujadili Bajeti ya mwaka
2010/2011;

(iii) Utekelezaji wa malengo ya Wizara kwa kipindi cha mwaka 2010/2011;

(iv) Changamoto zinazoikabili Wizara; na

(v) Maombi ya fedha kwa kazi zilizopangwa kufanyika katika mwaka wa fedha 2011/2012.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Makadirio hayo, Kamati ilielezwa kuwa Wizara ya Viwanda
na Biashara inaomba jumla ya shilingi 57,728,718,000/= kati ya hizo shilingi 30,052,589,000/= ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na shilingi 27,676,129,000/= ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yangu haikuweza kukamilisha na kupitisha Bajeti ya Wizara katika vikao hivyo kutokana na Bajeti hiyo kuwa ndogo sana ukilinganisha na majukumu ambayo Waziri aliyaainisha mbele ya Kamati kwamba Wizara yake imepanga kuyatekeleza na hivyo Kamati kupanga kuonana na Waziri Mkuu ili kuona uwezekano wa Wizara kuongezewa Bajeti, Kamati ilimwona Waziri Mkuu na kuahidiwa kuwa Bajeti hiyo itaongezwa, lakini hadi tarehe 30/07/2011, Kamati ilipokutana Dodoma na Wizara ili kupitisha Bajeti hiyo hapakuwa na
mabadiliko yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yangu imesikitishwa sana na Bajeti iliyopangiwa Wizara hii. Pamoja na ushauri wa Kamati uliotolewa mwaka jana kuhusu umuhimu wa Wizara hii na kutaka iingizwe kwenye Wizara za vipaumbele ikiwa ni pamoja na kuongezewa fedha bado Bajeti ya Wizara hii ni ndogo sana. Cha kusikitisha zaidi ni kwamba badala ya Bajeti ya fedha za Miradi ya Maendeleo kuongezeka mwaka huu imepungua zaidi kutoka shilingi 32,717,666,500/= kwa mwaka wa fedha 2010/2011 hadi shilingi 27,676,129,000/= kwa mwaka wa fedha 2011/2012. Wakati Wizara hii ina jukumu kubwa la kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 inayolenga kuifanya Tanzania kufikia kiwango cha kati cha Maendeleo ya Uchumi wa Viwanda (Semi Industrialized Economy) ifikapo mwaka 2025, hii ni pamoja na kutekeleza na kusimamia Sera ya Maendeleo
Endelevu ya Viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yangu inajiuliza hivi Serikali ina dhamira ya kweli ya kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya kuisaidia Wizara hii kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 na kuifanya isimamie kikamilifu Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda na kuifikisha Tanzania kiwango cha kati cha maendeleo ya uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025. Kamati inashauri Serikali kuongeza Bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara ili iweze kutekeleza azma hii. Aidha, Kamati inaitaka Serikali kuhakikisha kuwa fedha zote zilizoidhinishwa na Bunge
zinatolewa kama zilivyoidhinishwa kwa wakati muafaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na kodi za Serikali kuwa nyingi na kutozwa kwa kiwango kikubwa sana na kwa makundi machache ya watu na hivyo kodi kugeuka kuwa mzigo kwa wawekezaji na wajasiriamali wadogo kwa ujumla na kufanya wafanyabiashara wengi kukwepa kulipa kodi na Serikali kukosa mapato. Kamati yangu inaishauri Serikali kuwa ili kulinda maslahi ya nchi na kuwahamasisha wafanyabiashara wote kulipa kodi bila kukwepa, ni vyema mfumo wa kodi uangaliwe upya kwa lengo la kuboresha na kuongeza ukusanyaji wa mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania imejikita kwenye kaulimbiu ya Kilimo Kwanza ikiamini kuwa ndicho kitakachowakomboa Watanzania zaidi ya asilimia 80% wanaotegemea kilimo na kwamba kitawatoa kwenye hali ya umaskini na kuwawezesha kuwa na maisha bora, Kamati yangu inaamini kuwa bila kuweka mkazo na nia ya makusudi kwenye viwanda, azma hii ya Kilimo Kwanza haiwezi kufanikiwa kwa kiwango cha juu kwa sababu kilimo kinategemeana sana na viwanda, Kamati yangu inaishauri Serikali kuwa ili kufanikisha azma hii ya Kilimo Kwanza bado kuna umuhimu mkubwa wa sekta hii ya viwanda kupewa kipaumbele. Aidha, Kamati yangu inaamini kuwa Serikali inatakiwa kuhamasisha wananchi wawekeze katika viwanda vya kusindika mazao, ili kuongeza thamani ambayo kwa hakika itaongeza bei ya bidhaa zetu na kuongeza Pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Wizara ina taasisi 17 zenye miradi mbalimbali na kwa kuwa Bajeti ya Wizara haitoshi kutekeleza mipango yote kwa wakati mmoja, Kamati yangu inashauri Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara kuweka vipaumbele ndani ya Wizara kwa kuanza na Taasisi nne tu kwa mwaka huu ambazo zikiwezeshwa zitaleta ufanisi wa hali ya juu na kuepukana na utegemezi wa Bajeti unaojitokeza kila mwaka. Aidha, utekelezaji wa miradi husika utaiwezesha Tanzania kukua kiuchumi na hatimaye kuondokana kabisa na umaskini. Kwa mwaka
huu, Kamati yangu inapendekeza Mashirika yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC). Shirika hili katika mipango yake limekusudia kutekeleza Miradi ya Makaa ya Mawe ya Mchuchuma na Ngaka, Chuma cha Liganga, Mradi wa kuangamiza Mazalia ya Mbu na mradi wa Magadi Soda. Endapo miradi hii itatekelezwa nchi itaweza kutekeleza miradi mikubwa ambayo ni chachu ya uanzishwaji wa viwanda vikubwa, kati na vidogo kutokana na upatikanaji wa mali ghafi muhimu ya chuma na upatikanaji wa umeme wa uhakika. Miradi hii ya makaa ya mawe inatarajiwa kuwa na uwezo wa kuzalisha umeme wa Mw 1,000 ifikapo mwaka 2014 na kutengeneza chuma tani 1,000,000 kwa
mwaka.

Kamati yangu kwa msisitizo inaamini kabisa kuwa, kama Serikali ina nia ya kweli ya kutatua tatizo sugu la umeme ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa kuzorota kwa uchumi katika nchi yetu, Shirika la NDC kupitia Miradi ya Makaa ya Mawe Mchuchuma na Ngaka, Kiwira na mradi wa umeme wa upepo Singida ndio suluhisho la uhakika na la haraka. Kamati yangu imesikitishwa sana na taarifa za urasimu ilizozipata juu ya uanzishwaji wa mradi wa umeme uliopo Mkoani Singida, Kamati yangu inakusudia kumwita Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO ili atupe
sababu za msingi kwa nini mpaka leo hajasaini mkataba wa mradi huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi imejifunza kwa njia ngumu kuelewa kwamba sasa hatuwezi kuweka mategemeo yetu yote katika umeme unaotokana na maji. Duniani kote mitambo ya umeme inayotumia makaa ya mawe inachangia 41% ya umeme, wakati mitambo ya maji inachangia 16%, gesi 20%, nguvu za nukilia 15% na mafuta 6% tu. Katika nchi ya Afrika ya Kusini mitambo ya makaa ya mawe huchangia umeme kwa 93%, India 69% na Moroco 55%. Tanzania tuna maeneo kumi yenye makaa ya mawe na yanapatikana Kusini Magharibi mwa nchi yetu. Maeneo haya yanakadiriwa kuwa na makaa ya mawe zaidi ya tani bilioni 1.2. Kati ya maeneo haya yaliyokwishafanyiwa uchunguzi ni Mchuchuma - Katewaka, Songwe - Kiwira na Ngaka -
Mbinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, NDC kwa kushirikiana na Kampuni ya Intra Energy ya Australia wameunda Kampuni inayoitwa TANCOAL ENERGY LTD. inayoendesha Mradi wa Ngaka Wilayani Mbinga. Lengo ni kujenga mitambo ya kufufua umeme wa MW 400 kwa kutumia makaa ya mawe. Kwa kuwa kwa sasa Mkoa wa Ruvuma haujaunganishwa na Gridi ya Taifa na kwa vile Serikali ya Sweden inafadhili mradi huo toka Makambako hadi Songea kwa kujenga njia ya
umeme ya 132 kV. Kamati yangu inaishauri Serikali kufanya yafuatayo:-

(i) Kuzungumza na Wahisani hawa ili kuharakisha ujenzi wa mradi huu ili umeme
utakaozalishwa Ngaka uingizwe kwenye grid ya Taifa; na

(ii) Serikali kwa kushirikiana na Wadau wake ijenge njia ya umeme kutoka Ngaka mpaka
Songea. Mradi unakadiriwa kugharimu Dola za Kimarekani 46 milioni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, NDC inahusika sana pia kuendeleza miradi ya chuma cha Liganga na makaa ya mawe Mchuchuma kwa kushirikiana na wawekezaji kutoka china. Kwa kuwa miradi hii ni yenye faida na maslahi makubwa kwa Taifa na imezungumzwa kwa muda
mrefu. Kamati yangu inaishauri Serikali kufanya yafuatayo:-

(i) Kuipa fedha zaidi NDC ili iweze kuwa na nguvu ya kimaamuzi na utekelezaji;

(ii) Kuhakikisha miradi hii inaanza vizuri kwa kuangalia maslahi ya wananchi pale
wanapotakiwa kupisha uchimbaji wa madini hayo kwa kuwalipa vizuri, lakini pia kuwapimia na kuwaandalia makazi ya kisasa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa kiwanda cha kutengeneza dawa za kuangamiza mazalia ya mbu. Mradi wa kiwanda cha kutengeneza dawa za kuangamiza mazalia ya mbu chenye uwezo wa kuzalisha lita milioni sita kwa mwaka. Utekelezaji wa kiwanda hiki utaleta suluhisho la kudumu la ugojwa sugu wa malaria kwa Watanzania na kuondoa tatizo la kupoteza nguvu kazi inayopotea kila mwaka kutokana na vifo vya malaria. Aidha, mradi huu utaweza kuiondolea Serikali adha ya kuendelea kupata msaada wa vyandarua ambavyo hata hivyo siyo suluhisho la kudumu la tatizo la malaria, kwani tumeendelea kuona na kushuhudia watanzania wakiendelea kupoteza maisha kutokana na ugojwa wa malaria pamoja na juhudi za Serikali za
kugawa vyandarua kila kaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO). Mataifa mengi duniani yamekuwa na uchumi mzuri na kuondokana na umaskini kwa kuwawezesha wajasiriamali wadogo kupitia Viwanda Vidogo vidogo (SIDO). Endapo SIDO itawezeshwa na kutumiwa vizuri itasaidia sana kuondoa tatizo la ajira kwa vijana na Pato la Taifa kukua kwa kiwango kikubwa na
hivyo kuondoa tatizo la umaskini na kuboresha maisha ya kila Mtanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili SIDO iweze kutekeleza mipango yake kwa mwaka wa fedha 2011/2012 itahitaji shilingi 11,232,000,000/=. Katika Bajeti hii imetengewa shilingi 1,759,322,360/= tu, fedha ambayo haiwezi kutekeleza hata mradi mmoja. Suluhisho la kudumu la ajira kwa vijana linapatikana hapa. Tatizo la ajira ni bomu linasubiri muda, linaweza kulipuka wakati wowote. SIDO imedhamiria kujenga mitaa ya viwanda kila Wilaya kwa kuandaa maeneo kwa ajili ya wazalishaji wadogo na wa kati. SIDO isaidiwe kwa kupewa mtaji wa kutosha ili kutengeneza ajira za kutosha nchi nzima. Maisha bora kwa kila Mtanzania yatawezekana kama Taifa litaamua kwa dhati kuwekeza SIDO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wengi wameshindwa kujiajiri kutokana na ukosefu wa maeneo ya kufanyia kazi na mitaji. Wakopeshaji wanakuwa na hofu kutokana na vijana hao kutofikika kirahisi na kutojulikana kwa shughuli zao. Matokeo yake wengi wa vijana wahitimu wa vyuo wamejikuta wakianzisha biashara zisizo na tija au kuishia kuwa vibarua wa wageni. Kamati yangu inaishauri Serikali kutumia fursa za mitaa ya SIDO na maeneo huru ya uwekezaji (EPZA) kutenga maeneo maalum kwa ajili ya vijana hususan wanaomaliza Vyuo Vikuu na VETA, ili kuwajengea mazingira mazuri ya kujiajiri. Aidha, tunashauri vijana waanzishiwe benki yao maalum kama ilivyo kwa wanawake ili kuwawezesha kupata mitaji ya biashara rasmi inayofanana na elimu yao. Hali kadhalika vijana hao wakijiajiri wanaweza kulipa mikopo yao ya benki na ya elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wengi wameshindwa kujiajiri kutokana na ukosefu wa maeneo ya kufanyia kazi na mitaji. Wakopeshaji wanakuwa na hofu kutokana na vijana hao kutofikika kirahisi na kutojulikana kwa shughuli zao. Matokeo yake wengi wa vijana wahitimu wa vyuo wamejikuta wakianzisha biashara zisizo na tija au kuishia kuwa vibarua wa wageni. Kamati yangu inaishauri Serikali kutumia fursa za mitaa ya SIDO na maeneo huru ya uwekezaji (EPZA) kutenga maeneo maalum kwa ajili ya vijana hususan wanaomaliza Vyuo Vikuu na VETA, ili kuwajengea mazingira mazuri ya kujiajiri. Aidha, tunashauri vijana waanzishiwe benki yao maalum kama ilivyo kwa wanawake ili kuwawezesha kupata mitaji ya biashara rasmi inayofanana na elimu yao. Hali kadhalika vijana hao wakijiajiri wanaweza kulipa mikopo yao ya benki na ya elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mamlaka ya Maeneo Huru ya Kukuza Uchumi (EPZA), Mkutano uliopita wa Bunge tulipitisha marekebisho ya Sheria ya EPZA ili kuipa mamlaka hiyo nguzu zaidi ya usimamizi wa Maeneo Huru ya Uwekezaji, ikiwa ni pamoja na kupata wawekezaji kwa maeneo yaliyokwishaainishwa likiwemo eneo la Bagamoyo ambalo wawekezaji wako tayari kuwekeza wakati wowote likikamilika. Ili uwekezaji uweze kuendelea katika maeneo yaliyoainishwa, EPZA
inatakiwa kulipa fidia ya shilingi 65,000,000,000 kwenye maeneo yafuatayo:-

Bagamoyo shilingi 55,000,000,000/0, Songea shilingi 3,100,000,000/=, Tanga shilingi
4,200,000,000/=, Kigoma shilingi 1,500,000,000/= na Mara shilingi 1,200,000,000/=. Aidha EPZA inatakiwa kukamilisha ujenzi wa miundombinu katika eneo la Bagamoyo na Benjamin Mkapa. Kwa mwaka wa fedha 2011/2012 Mamlaka imetengewa kiasi cha shilingi 4,106,164,640/= tu, kiasi hiki cha fedha hakiwezi kulipa fidia wala kukamilisha ujenzi wa miundombinu katika eneo moja. Endapo EPZA itawezeshwa na kukamilisha ujenzi wa miundombinu katika eneo la Benjamin Mkapa na Bagamoyo tu, litaweza kupata wawekezaji, hivyo kuliongezea Taifa fedha za kigeni, kuongeza ajira kwa wananchi wengi pamoja na kuongeza kipato chao na hivyo maisha bora kwa kila Matanzania yatawezekana. Aidha, kukamilika kwa mradi wa Bagamoyo kutasaidia kuondoa
msongamano wa kibiashara uliopo Dar es Salaam ikwemo Bandari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, EPZA imetenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji katika Mikoa yote ya Tanzania isipokuwa Tabora na Dodoma na maeneo hayo yalikuwa yanamilikiwa na wananchi hivyo inatakiwa kulipwa fidia. Wananchi wamekuwa wakisubiri kwa muda mrefu ili kulipwa fidia yao na thamani ya fedha inashuka kila kukicha je, wananchi hao watalipwa fidia yao pamoja na riba? Ni vyema Serikali iipatie EPZA fedha ya kutosha ili wananchi husika waweze kulipwa fedha zao la sivyo Serikali iache maeneo ya wananchi ili wafanyie shughuli zao za maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na nyumba nyingi za wananchi wanaohamishwa kuwa duni hivyo kusababisha walipwe fidia ndogo ambayo haiwezi kwenda kujenga nyumba nyingine, Kamati yangu inashauri Serikali kuona utaratibu mzuri wa kuwasidia wananchi hawa kwa
kuwajengea nyumba nyingine mahali pengine (settlement).

Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (CARMATEC) kina kazi kubwa ya kubuni, kuunda na kueneza teknolojia za zana za kilimo vijijini. Endapo CAMARTEC itawezeshwa kifedha itaweza kuinua hali ya maisha ya wananchi wa vijijini kwa kutengeneza na kueneza teknolojia ya zana bora za kilimo. Kwa sasa CAMARTEC imejikita katika utengenezaji wa trekta. Kamati imebaini kuwa trekta hizo ni bora na zina uwezo mkubwa kuliko power tillers ambazo kwa sasa nchi yetu
inazieneza kwa kasi.

Kwa kuwa Serikali inahamasisha kaulimbiu ya Kilimo Kwanza, Kamati yangu inashauri Serikali kupitia Halmashauri za Wilaya kununua trekta kutoka CAMARTEC ili kuiwezesha kukuza mtaji wake, kusambaza teknolojia yao na kujiendesha yenyewe hivyo kuipunguzia Serikali mzigo (Commercialization of Tractor Project). Aidha, wananchi watakuwa wamefaidika na teknolojia iliyogunduliwa hapa nchini na Watanzania wenyewe na hivyo kuharakisha mapinduzi ya viwanda. Ili kukamilisha mipango yake kwa mwaka wa fedha 2011/2012 CAMARTEC inahitaji shilingi 4,406,691,795/=; kwa sasa imetengewa shilingi 850,000,000/= tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na umuhimu wa maeneo ya vipaumbele yaliyoainishwa hapo juu, Kamati yangu inaendelea kusisitiza Wizara iongezewe Bajeti na kupatiwa angalau shilingi 50,000,000,000/= kwa matumizi ya maendeleo ili Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), Mamlaka ya Maeneo Huru ya Uwekezaji (EPZA) na Kituo cha Zana za Kilimo na Ufundi Vijijini (CAMERTEC) ziongezewe fedha kwa lengo la kutekeleza angalau sehemu ya miradi iliyopangwa kutekelezwa na Taasisi hizi kwa maslahi ya uchumi wa nchi yetu. Aidha, Kamati yangu iliahidiwa kuwa Bajeti hii itaongezwa wakati wa kufanya mapitio ya Bajeti (Mid Year Budget Review). Kamati yangu inaamini kwamba kwa umakini wa Serikali yetu ahadi hii itatekelezwa kwa muda muafaka kama ilivyoahidi na hivyo kupitia Bajeti
hii Kamati inaomba kauli ya Serikali kuhusu commitment yake juu ya jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia utekelezaji wa mfumo wa soko huru, Tanzania imekuwa jalala la bidhaa zote zisizo na ubora na bandia, Serikali bado haijadhibiti mianya yote inayotumiwa kuingiza bidhaa zisizo na ubora na bandia ambazo zimekuwa na athari kubwa kwa Taifa na watu wake. Kwa mfano uingizaji wa tairi na tube za pikipiki aina ya Vee Rubber Thailand ambazo huuzwa kwa bei ndogo na kusababisha ushindani usio wa haki katika biashara kwa viwanda vyetu vya hapa nchini. Mipira hii bandia imetapakaa sana Dar es Salaam na maeneo mengi ya mipakani kama Kilimanjaro, Mbeya, Mwanza, Bukoba na Musoma. Athari za bidhaa hizi
bandia ni kubwa sana kwa Taifa letu ikiwemo:-

(i) Ajali za mara kwa mara zinazosababishwa na kupasuka kwa tairi na kusababisha
vilema vya kudumu au kupoteza maisha kwa waendesha pikipiki na watembea kwa miguu, hivyo kupoteza nguvu kazi ya Taifa.

(ii) Wananchi kudanganywa kulipia bidhaa bandia kwa bei kubwa sawa na bidhaa halisi kutokana na kukosa uelewa wa kutofautisha kati ya bidhaa bandia na halisi kwani bidhaa hizi kwa kawaida zinakuwa zinafanana sana na siyo rahisi kutofautisha.

(iii) Kutokana na udanganyifu unaofanywa na baadhi ya Maofisa wa TRA kwa kushirikiana na wafanyabiashara wadanganyifu wanaoingiza bidhaa hizi bandia kutoka nje, Serikali inakosa mapato mengi ya haki. Aidha, hali hii inawavunja moyo na kuwakatisha tamaa wafanyabiashara waaminifu ambao wanaingiza bidhaa halisi na kulipia kodi kama wanavyotakiwa kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yangu inakusudia kuunda Kamati ndogo ili kulifanyia
uchunguzi jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yangu ina shangazwa sana na Serikali kwa nini mpaka leo Sheria ya Viwango Na. 2 ya mwaka 2009 ambayo pamoja na mambo mengine inahusu ukaguzi wa bidhaa kabla hazijaingia nchini (Pre-shipment Verification of Conformity to Standard - PVoC) haijaanza kutumika, sheria hii ingeweza kudhibiti uingizaji wa bidhaa zisizo na ubora na bandia na kusaidia udhibiti dhidi ya wafanyabiashara na baadhi ya Maofisa wa TRA wasiowaaminifu kwa kufanya ukaguzi wa bidhaa zote zinazoingia nchini huko huko nje zinakotoka. Suala la kufanya ukaguzi wa bidhaa hizi zikiwa tayari zimeingia nchini linaleta hasara na machungu mengi kwa wahusika kwani zinapothibitika hazina kiwango au ni bandia, Sheria ya TBS
inataka bidhaa hizo ziteketezwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yangu inashauri utaratibu wa Pre-shipment Verification of Conformity (PVoC) uanze kutumika haraka kwa kuwa Sheria hiyo ilishapitishwa na Bunge lako Tukufu tangu mwaka 2009. Aidha, inapotokea bidhaa zimekamatwa ambazo hazifai, wahusika waamriwe kuzirudisha kule walikozitoa badala ya utaratibu wa sasa wa kuziteketeza kwa moto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia kauli ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na tamko la Waziri wa Fedha lililotolewa wakati akiwasilisha Bajeti kwa mwaka wa fedha 2011/2012 kuhusu Serikali na Taasisi zake kuacha kununua bidhaa ikiwemo samani kutoka nje na kutoa agizo kuwa samani zote zinunuliwe kwa wenye viwanda hapa nchini, Kamati inaipongeza Serikali kwa tamko hili ambalo wananchi wamekuwa wakisubiri kusikia kwa muda mrefu sasa. Kwa vile bado tunashuhudia kununuliwa kwa samani za nje, Kamati yangu inashauri kuwa ni wakati muafaka sasa Serikali ilete Muswada wa Sheria hapa Bungeni ili kurahisisha utekelezaji wa azma hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria na Sera ya uvunaji malighafi za viwandani ya mwaka 2006, iliwekwa kwa nia nzuri ya kuzuia watu wa nje wasiendelee kuvuna magogo na mbao na kuzisafirisha nje ya nchi, lakini kwa bahati mbaya Sheria hii haikuangalia wawekezaji na watumiaji wa malighafi hii katika viwanda vyetu vya ndani ambapo imesabababisha urasimu na usumbufu katika kupata vibali vya uvunaji wa malighafi pamoja na usumbufu katika usafirishaji kutokana na vizuizi vya barabarani na usumbufu wa polisi. Kutokana na sheria hii viwanda vingi vya samani vinalazimika kununua malighafi (magogo) nje, kutoka Msumbiji, Congo, Gabon na Afrika ya Magharibi ambako bei yake ni ndogo kuliko bei ya hapa nchini. Mfano cubic metre ya mbao kutoka nje hadi kufika Dar es Salaam ni dola za Kimarekani 500 hadi 600 wakati hapa nchini ni 900 hadi 1,000 na kupoteza fedha nyingi za kigeni ambazo zingetumika kwa matumizi mengine
kuendeleza uchumi wa nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vyote vilivyokuwa vya Serikali (Tanzania Wood Industry Corporation - TWICO) vilivyonunuliwa na wawekezaji kama Mang'ula Sawmill Morogoro, Mkata Sawmill Co. Ltd. na Sick Sawmill (T) Tanga, Kill Timber Moshi, Mingoyo Sawmill Co. Ltd. Lindi na Tabora Misitu vimekufa. Kamati inashauri Serikali kupitia Wizara husika kupunguza gharama ya malighafi hii ya magogo na mbao ili kunusuru viwanda vya samani ambayo bado vinaendelea, ikiwemo kufufua viwanda nilivyovitaja hapo juu. Aidha, Sheria ya Uvunaji Malighafi za Viwandani ya mwaka 2006 ifanyiwe marekebisho haraka. Kuchelewa kufanya marekebisho kwa sheria hii
kutasababisha viwanda vingi kufungwa na hivyo kuathiri ajira ya wafanyakazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na juhudi za makusudi zinazotakiwa kufanywa na Serikali kwa lengo la kuvilinda viwanda vya ndani, Kamati yangu inatoa angalizo katika maeneo
yafuatayo:-

(i) Kulinda viwanda vya ndani kusisababishe kuwaumiza wakulima wadogo, kwa wenye viwanda kupanga bei ndogo ya mali ghafi ambayo itaweza kuwathiri.

(ii) Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo kubwa sana linalojitokeza katika uagizaji wa sukari nje ya nchi. Lengo la Serikali ni zuri lakini, inatakiwa iruhusu uagizaji wa sukari mwaka mzima baada ya kufanya tathmini ya kweli na kujua mapungufu ambayo yatakuwepo katika mwaka huo husika. Hii itasaidia sana kufanya bei ya sukari kutobadilika badilika badala ya kutoa leseni na vibali vya kuingiza sukari pale inapogundulika kuwa kuna mapungufu, kwani wafanyabiashara ambao sio waaminifu hutumia mwanya huo kuwaumiza wananchi walio wengi kwa kupandisha bei ya sukari
bila mpangilio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yangu inaipongeza Serikali kwa juhudi za makusudi za kuhamasisha na kuchochea uwekezaji wa viwanda vya kutengeneza bidhaa za ngozi ndani ya nchi vinavyotumia ngozi zilizosindikwa na viwanda vya usindikaji vilivyopo hapa nchini, hii ni pamoja na kazi nzuri ya uanzishaji na uzinduzi wa kituo cha mafunzo kwa wajasiriamali wa ngozi kilichozinduliwa hapa Dodoma tarehe 18 Juni, 2011 na Waziri wa Viwanda na Biashara. Hatua hii ya Serikali ni muhimu sana na inaonyesha kwamba inajali watu wake pamoja na rasilimali zilizopo
nchini.

Hata hivyo kituo hiki hakitakuwa na maana endapo Serikali itaendelea kuruhusu ngozi ghafi kuendelea kusafirishwa nje ya nchi. Tanzania ina uwezo wa kuzalisha ngozi ghafi zenye futi za mraba milioni 92 kwa mwaka, lakini wastani wa makusanyo ya ngozi ghafi nchini ni futi za mraba milioni 51.2 kwa mwaka. Uwezo uliosimikwa kwa mwaka kwa viwanda vyote kama vingekuwa vinafanya kazi ni futi za mraba milioni 74.0 lakini kwa tathmini ya mwaka 2010, uwezo uliotumika ulikuwa futi za mraba milioni 34.3, hata hivyo kumekuwa na ongezeko kubwa kwani mwaka 2005
uwezo uliotumika ulikuwa futi za mraba takribani milioni 6.0 tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu mojawapo ya viwanda vya usindikaji wa ngozi nchini kutotumia uwezo wao wote kama takwimu zinavyoonyesha ni kukosekana kwa mali ghafi ambapo sehemu kubwa inaendelea kuuzwa nje ya nchi, hii inaonyesha kwamba endapo ngozi zote zingekusanywa kikamilifu (potential production) na endapo viwanda vyote vya usindikaji vitafanya kazi kwa uwezo uliosimikwa, ngozi zinazokusanywa hazitatosheleza mahitaji ya ngozi
ghafi, kutakuwa na upungufu wa ngozi ghafi wa futi mraba takribani milioni 23.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyabiashara watiwe moyo kuongeza thamani ya zao la ngozi hata kwa kusindika kwa kiwango cha awali tu (Semi processed leather) na kuuza nje bila ushuru kwa lengo la kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wanabadilisha mfumo wa sasa wa kuuza ngozi ghafi badala yake wauze ngozi iliyosindikwa hapa hapa nchini na hii italeta faida kubwa
kwa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kulinda na kuimarisha sekta hii ya ngozi, Kamati yangu
inashauri mambo yafuatayo:-

(i) Serikali kuongeza ushuru wa ngozi ghafi zinazouzwa nje (Export Levy) kutoka 40% inayotozwa sasa hadi 90%. Hii itasaidia ngozi ghafi kutosafirishwa nje kwa wingi na hivyo viwanda vyetu vya ndani kupata mali ghafi ya kutosha kwani kwa sasa ngozi ghafi nyingi inauzwa nje kwa sababu bei ya nje ni kubwa. Aidha, Serikali itaongeza mapato zaidi na fedha hizo zitarudi kusaidia sekta ya ngozi.

(ii) Kamati yangu imegundua udanganyifu mkubwa katika biashara ya ngozi ghafi zinazouzwa nje hasa kwa Maofisa wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi wanaotoa vibali vya usafirishaji wa ngozi ghafi nje ya nchi kwa kushirikiana na baadhi ya wafanyabiashara wasiowaaminifu.
Udanganyifu huo upo katika vipimo na uzito na bei ya kuuzia ambapo wafanyabiashara huwasilisha nyaraka zao Wizara ya Mifugo na Uvuvi zikiwa tayari zina udanganyifu na kwa bahati mbaya maafisa wanaohusika hupitisha na kutoa vibali, hii inawezekana ni kutokana na kukosa umakini kwa maafisa hao au ni kwa kusudi maalum.

Kamati yangu inaishauri Serikali iunde Kamati maalum itakayohusika na uchambuzi wa nyaraka za wafanyabiashara na kutoa mapendekezo kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili waweze kutoa vibali kwa kuzingatia mapendekezo na ushauri wa Kamati hiyo. Hii iatasaidia kunusuru mapato ya Serikali yanayopotea kutokana na ubadhilifu huu.

(iii) Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na ongezeko la uingizwaji wa viatu kutoka nje, mwaka 2005 ziliingia jozi za viatu vya plastiki 18,042,000 na viatu vya ngozi 140,000 tu, mwaka 2009 viliingizwa viatu vya plastiki 33,999,000 hivi vyote vinaongeza ushindani usio wa haki kwa viatu vya ngozi vinavyotengenezwa hapa nchini. Ili kupunguza ushindani usio wa haki, Serikali itoze ushuru maalumu (specific import duty) kwa bidhaa za plastiki kama mabegi na viatu zinazoingizwa nchini kutoka nje ambazo zinafananana na ngozi halisi. Hii itasaidia sio tu kupunguza ushindani usio wa haki bali kuvilinda viwanda vya ndani na Serikali kupata mapato.

(iv) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iweke mkakati wa makusudi wa kusimamia na kudhibiti ngozi ghafi zinazosafirishwa nje kupitia mipaka yetu kwa njia za panya. Aidha, Serikali ishirikiane na wadau wa ngozi kwa maana ya Chama cha Wadau wa ngozi (Leather Association of Tanzania - LAT) na Chama cha Wasindikaji wa Ngozi Tanzania (Tanzania Tanner's Association- TTA) kuhamasisha wenye viwanda vya usindikaji wa ngozi kuandaa na kutekeleza mipango thabiti ya kuongeza utumiaji wa uwezo wa viwanda vyao na kufanya upanuzi zaidi kwa lengo la kusindika ngozi zote zinazozalishwa hapa nchini.

(v) Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na nchi yetu kutokuweka utaratibu unaoeleweka kwa wafanyabiashara kumekuwepo na maduka kila mahali na yasiyo na mpangilio na wakati mwingine kuonekana kama uchafu. Kamati yangu inaishauri Serikali kuweka utaratibu wa maduka ya aina moja kuwa katika mtaa mmoja. Hii itasidia sana kudhibiti bidhaa bandia na zisizo na ubora pia itakuwa rahisi kwa Serikali kukusanya kodi. Aidha, Kamati inashauri maduka ya magari yatengewe eneo moja nje ya mji kuliko utaratibu wa sasa wa kila mahali katikati ya mji kuna
maduka ya magari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yangu na Wabunge wote kwa ujumula wamekuwa wakizungumzia kwa uchungu kuhusu ufufuaji wa kiwanda cha matairi cha General Tyre East Africa Ltd. Kamati yangu inampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuonesha nia ya dhati ya kuhakikisha kuwa kiwanda hiki kinafufuliwa na kuanza kufanya kazi kwa kuiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara kuanza mchakato huo. Kamati yangu inaiagiza Wizara kufanya kazi hiyo kwa haraka na kwa kuzingatia maoni ya Kamati ndogo ya Bunge iliyoundwa kuchunguza Kampuni ya General Tyre East Africa Ltd., taarifa ya Kamati ndogo itawasilishwa na Kamati husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia mwanzo huu mzuri wa kukifufua Kiwanda cha Matairi cha General Tyre, Kamati yangu inaiagiza Serikali kuchukua hatua thabiti juu ya viwanda vilivyobinafsishwa lakini havifanyi kazi au matumizi/malengo yake yamebadilishwa bila kibali cha
Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yangu ilipata fursa ya kutembelea Maonesho ya 35 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam ambapo ilifarijika sana na kazi nzuri inayofanywa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzanaia (TanTrade) ambayo ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge ya mwaka 2009 iliyopitishwa na Bunge lako kwa lengo la kuratibu na kusimamia biashara ya ndani na nje, shughuli ambazo zilikuwa zinafanywa na Halmashauri ya Biashara ya Nje (BET) na Bodi ya Biashara ya Ndani (BIT). Ikiwa katika viwanja vya Mwalimu Nyerere Kamati yangu iliweza kushiriki uzinduzi wa Mamlaka ya TanTrade uliofanywa na Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt. Gharib Bilal. Kuzinduliwa kwa Mamlaka hii kutaiwezesha kuendeleza na kukuza biashara ya ndani na nje, kutoa ushauri wa kitaalam kwa wazalishaji ili waweze kuzalisha kwa kuzingatia mwenendo
na mahitaji ya soko na hatimaye kuwaunganisha na masoko ya nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua fursa hii kumpongeza Mkurugenzi wa TanTrade Mheshimiwa Ramadhan Khalfan pamoja na watendaji wote walio chini yake kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuendelea kuyaboresha maonesho hayo mwaka hadi mwaka na hata kuyafanya kuwa kivutio kikubwa kwa washiriki wa ndani na nje. Aidha, kumekuwa na ongezeko
kubwa la washiriki. Jumla ya nchi 17 zilishiriki katika maonesho ya mwaka huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ubora wa bidhaa nao umeongezeka, mazingira yameboreshwa hakuna vumbi, milango ya kuingilia iliongezeka, mapato nayo yameongezeka kwa kipindi cha 2000 hadi 2010 mauzo ya papo kwa papo yaliyofanywa na makampuni na taasisi zilizoshiriki yamefikia shilingi 141,000,000,000, maulizo ya mauzo ya nje ya nchi (export orders) yalikuwa dola za Marekani milioni 1,176.5 na maulizo ya manunuzi toka nje (import orders) yalikuwa na thamani
ya dola za Marekani milioni 1,064. Hata hivyo Kamati inashauri yafuatayo:-

(i) Kuwepo mitaa maalum ili kuweza kupata kirahisi bidhaa ambazo wananchi waliziona wakati wa maonyesho na wanataka kuzinunua.

(ii) Kuwepo utaratibu wa kuwa na vifungashio vizuri ambavyo kwa bidhaa zinazofanana vinafanana ili kuwavutia wanunuzi.

(iii) Kutokana na urasimu na usumbufu uliopo mipakani na bandarini na hivyo kuchelewesha mizigo ya wafanyabiashara wanaokuja kwenye maonesho Serikali iangalie utaratibu mzuri wa kuondoa kero hizi kwani kuna wafanyabiashara wanasumbuliwa na kucheleweshewa mizigo yao na kujikuta wamechelewa kwenye maonyesho hivyo kuwakatisha tamaa.

(iv) Kuwepo na maonesha ya Kanda ya wajasiriamali wa ndani, wadogo na wa kati kabla ya Maonesho ya Kitaifa na wale watakaoonekana wanafanya vizuri wawe wanateuliwa kwa kusaidiwa kwenda kwenye Maonesho ya Kitaifa kwani tutakuwa na uwezo wa kupata washiriki wengi wa ndani.

(v) Kamati inaipongeza Wizara kwa kutenga eneo maalum kwa ajili ya wafanyabiashara wenye ulemavu, hata hivyo mazingira ya kufika maeneo hayo hayakuwa wezeshi kwa watu wenye ulemavu. Hivyo tunashauri kipindi kijacho Wizara iangalie namna ya kuweka mazingira rafiki
kwa watu wenye ulemavu ili nao wapate kufaidika na maonyesho kama watu wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yangu pia ilishiriki katika uzinduzi wa GS1. GS1 ni Asasi isiyo ya Kiserikali inayohusika na utoaji wa mfumo wa utambuzi wa bidhaa (bar codes). Nchi yetu imekuwa ikipata huduma hizi kutoka nchi za Kenya na Afrika Kusini na hivyo kufanya bidhaa zetu kuonekana zinazalishwa nchi hizo, kwa sababu hiyo, Kamati yangu inaipoingeza Serikali na
wajasiriamali wote waliofanikisha zoezi hili muhimu kwa uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio haya mazuri, Kamati imepata taarifa kuwa wapo wadau wengine hawajaridhika na namna mchakato wa kuipata Kampuni itakayoshughulikia na utambuzi wa wa bidhaa (bar codes) na kwa vile taarifa hizi zimewafikia Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla kupitia vyombo vya habari kama magazeti. Kamati yangu inaitaka Serikali itoe maelezo ya kina ili wananchi waweze kuelewa nini kinaendelea kuhusu suala hili. Aidha, wananchi waelimishwe vya kutosha juu ya matumizi ya mfumo huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza hapo awali kuhusu majukumu ya yanayofanywa na Taasisi/Mashirika yaliyo chini ya Wizara hii, Kamati yangu inaendelea kusisitiza juu ya umuhimu wa kuweka vipaumbele ndani ya taasisi chini ya Wizara ili kuziwezesha kwa mwaka huu Taasisi za SIDO, NDC, EPZA na CAMARTEC ziweze kutekeleza vema majukumu yake na
baadaye kuweza kujitegemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nikushukuru tena wewe binafsi, Spika Mheshimiwa
Anne Makinda, Naibu Spika Mheshimiwa Job Ndugai, pamoja na Wenyeviti wa Bunge, Mheshimiwa George Simbachawene, Mheshimiwa Jenista Mhagama na Mheshimiwa Sylvester Massele Mabumba kwa kuendesha vikao vya Bunge lenye machachari mengi vizuri na kwa
kufuata Kanuni zilizowekwa na Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuchukua nafasi hii kumshukuru Waziri wa Viwanda na Biashara Mheshimiwa Dkt. Cyril Chami, Naibu Waziri Mheshimiwa Lazaro Nyalandu, Katibu Mkuu Bibi Joyce Mapunjo, Naibu Katibu Mkuu Dkt. Shabani Mwinjaka, pamoja na wataalam wote wa Wizara ya Viwanda na Biashara na taasisi zake kwa maelezo na ufafanuzi walioutoa mbele ya
Kamati wakati wa kuchambua Bajeti ya Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee napenda niwashukuru Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Viwanda na Biashara kwa ushirikiano wao katika kuchambua Bajeti ya Wizara
na kutoa maoni haya ya Kamati.

Kwa heshima kubwa naomba niwatambue kwa kuwataja majina kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Mahmoud Mgimwa, Mwenyekiti, Mheshimiwa Engineer Stella Manyanya, Makamu Mwenyekiti, Mheshimiwa Hussein Nassor Amar, Mheshimiwa Shawana Bukheti Hassan, Mheshimiwa Riziki Omar Juma, Mheshimiwa Haji Khatib Kai, Mheshimiwa Gaudence Kayombo, Mheshimiwa Chiku Abwao, Mheshimiwa Conchesta Rwamlaza, Mheshimiwa Esther Midimu, Mheshimiwa Margareth Agnes Mkanga, Mheshimiwa Said Mussa Zubeir, Mheshimiwa Ahmed Juma Ngwali, Mheshimiwa Haji Juma Sereweji, Mheshimiwa Ezekia Wenje, Mheshimiwa Abuu Jumaa, Mheshimiwa Bahati Ali Abeid, Mheshimiwa Deo Sanga, Mheshimiwa Ahmed Ali Salum, Mheshimiwa Naomi Kaihula, Mheshimiwa Khatib Said Haji, Mheshimiwa Godbless Lema,
Mheshimiwa Salim Hassan Abdallah Turky na Mheshimiwa Mohamed Dewji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia nichukue fursa hii kumshukuru Katibu wa Bunge Dkt. Thomas Kashilillah na wafanyakazi wote wa Ofisi ya Bunge kwa ushirikiano wao katika kuisaidia Kamati kutekeleza majukumu yake bila kukwama. Aidha, namshukuru Katibu wetu wa Kamati Bibi Angelina Sanga kwa kazi nzuri ya kuihudumia Kamati wakati wote ikiwa ni pamoja na kuandaa
maoni haya ya Kamati kwa wakati muafaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee naomba nichukue fursa hii kuwatakia kila la heri Waislamu kokote duniani ambao wako katika mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Mwenyezi Mungu awabariki sana na awatakabalie swaumu zao. Amin.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa naomba Bunge lako Tukufu liyapokee maoni
haya na kuyajadili. Baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.
Hon. Lucy Philemon Owenya Contribution
MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI KWA WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hotuba yangu ni ndefu sana na sitaweza kuimaliza, naomba inukuliwe kwenye Hansard kama ilivyowasilishwa leo asubuhi hapa
Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wajibu wangu kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama hapa mbele ya Bunge lako Tukufu leo na kutoa maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu hotuba ya Bajeti ya Viwanda na Biashara mwaka wa fedha 2011/2012 kwa mujibu wa Kanuni za
Bunge Kifungu cha 99(7), Toleo la 2007.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni Mheshimiwa Freeman Mbowe, kwa kuniteua kuwa Waziri Kivuli wa Wizara ya Viwanda na Biashara. Namshukuru kwa miongozo yake na uongozi thabiti akishirikiana na Naibu wake Mheshimiwa Kabwe Zitto pamoja na Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Mheshimiwa Tundu Lissu, kwa kuendelea kuonyesha imani kwangu. Naahidi nitaendelea kuifanya kazi niliyotumwa na chama changu kwa moyo mmoja na uaminifu mkubwa. Sina budi sasa kuwashukuru sana wapiga kura wa Tanzania kwa kuongeza sana imani yao kwa chama changu cha CHADEMA na kukipa kura nyingi ambazo bado sura ya kukubalika kwa chama
imeendelea kung'aa sana siku hadi siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishukuru familia yangu hasa wanangu Caroline, Yahone na mume wangu mpenzi Dkt. Fidelis Owenya kwa kuendelea kunivumilia kwa kunipa ushauri, upendo na mwongozo visivyokoma hasa kipindi kigumu cha kuuguzwa baada ya kupata kipigo cha polisi huko Jjijini Arusha Januari mwaka huu. Ninakiri kuwa donda la unyama niliofanyiwa na askari wa polisi nikiwa kama mama, Mbunge na raia mwema wa nchi hii lingenitesa zaidi kama nisingepata ushirikiano mkubwa kutoka kwa familia yangu hasa wazazi wangu, Mama Ndehorio Makomu na Mzee Philemon Ndesamburo pamoja na marafiki. Ninachoweza kusema, nawapenda, Mungu
azidi kuwalinda na kuwatimizia yote mnayoyatarajia kutoka kwake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kutoa masikitiko makubwa wakati tunajiandaa kutimiza miaka 50 ya Uhuru wa nchi yetu, sekta ya viwanda na biashara imeathirika sana na hasa viwanda kushindwa kuzalisha au kuzalisha chini ya uwezo wake kutokana na matatizo ya nishati ya umeme na hivyo kupelekea wafanyakazi kuachishwa kazi kutokana na kukosa kazi za kufanya. Hii ni aibu kwa Taifa letu ambalo viongozi wake wakuu ambao mara zote wanatafuta wawekezaji katika sekta ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi zetu kwa Serikali kwa kupunguza bei ya mafuta kama ilivyoahidi, Kambi ya Upinzani ilisikitishwa na tabia ya kiburi, dharua iliyoonyeshwa na wafanyabiashara wa nishati hii ya mafuta. Aidha, tunaishauri Serikali isimamie kikamilifu na kutekeleza agizo la Bunge lako Tukufu lililoitaka Serikali kuwa na akiba kubwa ya mafuta ili kudhibiti
soko la nishati hii ikiwa ni pamoja na kufufua kiwanda cha kusafishia mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema Serikali ikawachukulia hatua wote waliohusika katika mgomo wa kuuza mafuta. Haya ndiyo matatizo ya soko huria ambalo Serikali haisimamii kwa makini na hatimaye kuwa soko holela. Aidha, Kambi ya Upinzani inapendekeza biashara ya
mafuta inabidi iangaliwe kwa jicho pana zaidi kwani inaweza kutishia usalama wa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhima ya Wizara hii ni kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya maendeleo endelevu ya sekta za viwanda, biashara na masoko kwa njia ya kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika uwekezaji na biashara, kujenga na kuimarisha ujuzi katika biashara na kuweka msukumo zaidi kutumia fursa za masoko na kujenga mifumo imara ya viwanda, biashara na masoko yenye kuendeleza na kukuza mauzo nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutimiza dhima hii Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kuwa kuna changamoto kubwa ambayo inatokana na mfumo wetu wa Viwanda na Biashara ambao ulikuwa umejengeka katika dhana nzima ya kukabiliana na bidhaa na huduma toka nje ya nchi. Viwanda vinajitahidi kuzuia bidhaa za nje kwenye soko la ndani badala ya kujitahidi kufungua milango kwenye masoko ya nje sambamba na kuongeza ubora wa bidha hizo. Hili ni tatizo kubwa na jambo hili limechangia kwa kiasi kikubwa sekta ya Viwanda na Biashara kutokuwa shindani katika sura ya Kimataifa na hivyo kutokutoa tija inayohitajika ya kuleta uchumi ulioendelevu kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha Kambi ya Upinzani inaona kuwa ili kuwa na sekta endelevu ya viwanda inatakiwa kurekebisha mfumo mzima wa sekta ya fedha na sekta ya nishati
kama vichocheo muhimu ili kufanya sekta ya viwanda kuwa shindani Kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema kubadlisha mfumo wa sekta ya fedha kwa dhana kuwa mikopo inayotolewa kwa wawekezaji wa viwanda uwe tofauti na ule unaotumiwa na
wafanyabiashara wa kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni kumekuwa na malalamiko mengi kupitia vyombo vya habari pamoja na baadhi ya watu binafsi kuhusiana na usajili wa kampuni ya kutoa huduma ya kutambua bidhaa (bar codes). Kadhia hii inatokana na kusajiliwa kwa kampuni mbili tofauti lakini zenye maudhui sawa na Katiba za kampuni hizo zikiwa zinafanana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mvutano wa kampuni hizi umezua mashaka makubwa kwa
kuwa umeihusisha Serikali ikiwemo Ikulu pamoja na watendaji wake chini ya Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mvutano huo Kambi ya Upinzani inamtaka Waziri alieleze Bunge lako Tukufu kuhusu barua yake yenye Kumb. Na. BC.407/533/01 ya tarehe 16 Machi, 2011 aliyomuandikia Mkurugenzi Mkuu wa BRELA akimtuhumu kuhusika na sakata hili huku ikionyesha wazi kuwa kuna mashaka juu ya taratibu zilizotumika kuanzisha kampuni hizo mbili. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa ufafanuzi, je, taratibu za sheria na utawala bora zilifuatwa
katika usajili wa kampuni hizi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya changamoto kubwa zinazoikabili Wizara kwa ujumla ni kutokutengewa Bajeti ya kutosha ili kuendesha taasisi zilizo chini yake. Jumla Wizara imetengewa jumla ya shilingi bilioni 39.97 wakati mahitaji halisi kulingana na shughuli zinazotakiwa kutekelezwa
na Wizara pamoja na mashirika yake iliomba jumla ya shilingi bilioni 114.1.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tofauti kati ya fedha zilizotolewa na zile zilizoombwa na Wizara ni shilingi bilioni 74.13 ambayo ni sawa na asilimia 64.96. Lazima ifahamike kwamba duniani kote viwanda mama ni jukumu la Serikali kuvianzisha, ni ukweli uliowazi hakuna mwekezaji hata mmoja
aliyekuja na kujenga kiwanda hata kimoja bali wamerithi vile vilivyokuwepo.

Kwa Bajeti hii ni kweli Serikali ina nia ya dhati ya kufanya mapinduzi ya viwanda? Japokuwa Bajeti ya Wizara imekuwa finyu mno kwa kulinganisha na mahitaji halisi bado Wizara imetenga jumla ya shilingi milioni 175.9 kama posho za vikao. Kambi ya Upinzani inauliza umakini
uko wapi katika kupanga na kusimamia vipaumbele vyetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ana mamlaka ya usajili wa biashara na leseni kama jina lenyewe linavyosadifu lakini cha kushangaza mpaka sasa Wakala huyu hajihusishi na usajili wa leseni. Kambi ya Upinzani tunapenda kutoa ushauri kwa Serikali kuwa wakala huyu apewe jukumu la kusajili leseni kwa kuwa watakuwa katika nafasi kubwa ya kujua vizuri taarifa mbalimbali za wafanyabiashara kuliko ilivyo sasa ili kupunguza
urasimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge lako tukufu lilitunga Sheria ya Usajili wa Biashara namba 14 ya mwaka 2007 na kuridhiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 30 Machi, 2007. Hata hivyo pamoja na sheria hiyo kuwepo muda mrefu bado haijaanza kutumika mpaka
sasa, Kambi ya Upinzani inataka kuelewa sheria hiyo itaanza kutumika lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria hiyo inatoa mwanya wa kuanzisha kanda za usajili ambapo itasaidia wananchi wanaoishi mbali na Msajili Mkuu lakini mpaka sasa Kanda hizo hazijaanzishwa na hivyo kuleta usumbufu kwa wananchi wanaotoka maeneo ya pembezoni. Pia Sheria hiyo inamtaja Msajili Mkuu wa Biashara (Chief Registrar) ambapo wadhifa huo mpaka sasa
haupo na badala yake bado wadhifa wa Mkurugenzi Mkuu bado unaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi ya Upinzani inataka kujua ni kwa nini sheria hiyo haijaanza kufanya kazi na kuleta tija kwa wafanyabiashara na wajasiriamali ambao wamekuwa wakihangaika kupata usajili wa majina ya biashara kutokana na urasimu uliopo BRELA kwa sasa, jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo ya kiuchumi ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya viwanda ina changamoto nyingi zinazosababisha sekta hii ishindwe kuwa kiongozi katika kuchangia kwenye Pato la Taifa na pia kutoa ajira nyingi na za uhakika. Moja ya sababu kubwa ni ughali katika uzalishaji kwa kulinganisha na uzalishaji viwandani kwa nchi za nje. Ughali huu kwa kiasi kikubwa unatokana na nishati umeme na maji. Sababu ya pili na ya msingi kutokuwepo kwa taasisi za fedha zinazotoa mikopo maalum kwa ajili ya uwekezaji kwenye sekta ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali ya changamoto hizo kuna tatizo la uingizwaji wa bidhaa zenye ubora hafifu kwenye soko letu na kusababisha ushindani mkubwa wa bei na bidhaa zinazozalishwa na viwanda vyetu, Kambi ya Upinzani inamtaka Waziri alieleze Bunge lako Tukufu bidhaa hizi zinaingiaje nchini mpaka zinamfikia mlaji kupitia bandarini mpakani na viwanja vya
ndege wakati maeneo hayo yana wakaguzi? Kwa nini wahusika wasichukuliwe hatua ikiwa ni
pamoja na kufukuzwa kazi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi ya Upinzani inaona changamoto zote tulizoeleza hapo juu sio za lazima bali zimetokana na mfumo mbaya wa Serikali uliojaa ukiritimba katika mipango inayoweka mazingira wezeshi kwa viwanda. Udhaifu uliopo katika kutekeleza sheria au sheria kutengenezwa kwa lengo la kuangalia baadhi ya watu na kwa muda fulani. Aidha, ni kwa Serikali kutunga sheria kutokana na msukumo toka nje bila ya kuwepo kwa sera na hivyo kusababisha wajanja kunufaika na sheria hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi ya Upinzani inasisitiza kuwa viwanda vyetu sisi ndio wenye jukumu la kuvilinda na sio nchi za nje ambazo nazo zinawajibu wa kulinda raia wake na viwanda vyao. Udhaifu wetu kushindwa kupanga matumizi bora ya rasilimali zetu pamoja na kutunga sheria bora na kuzisimamia itaendelea kuitesa nchi na kupelekea miaka yote sekta ya viwanda kushindwa kutoa matunda tarajiwa. Jibu la tatizo hili ni kubadilisha mfumo wa utawala tulionao kwani toka Uhuru hadi sasa imedhihirika wazi kuwa umeshindwa kuleta tija kwa Watanzania
kutokana na kuwa viongozi wabovu wanalindwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na mfumo mbovu nilioutaja hapo juu Kambi ya Upinzani inaamini kwamba marekebisho yanayotaka kufanywa na Serikali kwenye Sheria ya Manunuzi (Public Procurement Act), yanalenga kuruhusu ufisadi kuendelea kwenye ununuzi wa mali za Serikali, hivyo tunaishauri Serikali kuangalia upya sheria hiyo na kuachana na kununua mali
zilizotumika ili kulinda viwanda vyetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi ya Upinzani haiamini kabisa kama nchi nyingine inaweza kutoa fedha ili tutengeneze sheria, ni dhahiri kuwa sheria itakayotungwa haiwezi kuwa na maslahi ya wananchi wetu, kwa vyovyote vile kutakuwa na mwanya kwa ajili ya wale waliotoa fedha za utungaji wa sheria hiyo. Mfano mzuri ni Muswada uliorudishwa wa Sheria ya Manunuzi ya Umma (Public Procurement Bill), IMF wanadai ni kwa nini Muswada uliletwa Bungeni bila ya wao kutoa
ridhaa. Swali la msingi ni kwa nini wao wakubali na sio sisi wenye nchi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Kiwanda cha General Tyre, kutokana na kaulimbiu ya Kilimo Kwanza kiwanda hiki cha General Tyre kimetegemewa kutoa mchango mkubwa katika sekta ya usafirishaji hasa vijijini kwa kutengeneza mpira unaohimili barabara zetu. Mipira inayoagizwa toka nje imeshindwa kukidhi mahitaji ya barabara zetu kutokana na hali ya hewa na pia bei zake kuwa za hali ya juu kupita kiasi. Kambi ya Upinzani inapendekeza kuwa Kiwanda cha East African General Tyre cha Arusha kifufuliwe ili kikidhi mahitaji ya nchi ikiwa na pamoja na
kupunguza ajali za barabarani zitokanazo na matairi yasiyokidhi viwango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko yaliyofuatiwa na matamko ya Serikali kuhusu Kiwanda cha Matairi cha General Tyre East Africa Ltd. hivi sasa Kiwanda hiki kimefungwa na hakifanyi kazi yoyote. Tatizo mojawapo ambalo limechangia kufilisika kwa kiwanda ni ubadhirifu wa kuuza mali za kiwanda zikiwemo nyumba na viwanja kadhaa viliuzwa na uongozi wa Kiwanda katika mazingira tata. Vilevile takwimu zinaonyesha kuwa hadi mwaka 2009 kampuni ilikuwa ina madeni yanayofikia shilingi bilioni 38.3. Kambi ya Upinzani inataka kuelewa ni sababu zipi zilizosababisha mbia mtarajiwa (Continental AG) kubadilisha mawazo na
kuamua kutotoa mtaji kwa mujibu wa makubaliano?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na mkopo ambao Kampuni ilipewa na Taasisi ya NSSF Kambi ya Upinzani inapenda kupata maelezo kadhaa. Kiwanda cha General Tyre kinamilikiwa na Serikali kwa asilimia 74 na NSSF ni taasisi inayomilikiwa na Serikali kwa asilimia 100, NSSF ndiyo iliyotoa mkopo kwa General Tyre.

Kambi ya Upinzani inataka kujua ni katika mazingira gani yalipelekea kuwepo kwa dalali toka Marekani aitwaye Debt Advisory International - DAI kushughulikia mkopo huo? Baadaye dalali huyo kulipwa dola milioni moja sawa na asilimia 10 ya mkopo wote wa dola za Kimarekani milioni 10. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kufanya uchunguzi wa kina kuhusu Kampuni hiyo ya
DAI na hatua za kisheria zichukuliwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi ya Upinzani inapendekeza kuwa kiwanda cha East African General Tyre cha Arusha kifufuliwe haraka iwezekanavyo na kisifilisiwe kama ambavyo Serikali na wadai wa Kiwanda wakifikiria la kufanya. Kwa kuwa Taasisi ya NSSF ni ya umma na kuna mahusiano chanya kati ya kufufuka kwa kiwanda na kufaidika kwa taasisi hii (wafanyakazi kuwa wanachama wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii na hivyo kuongeza michango na faida kwa uchumi mpana kwa ujumla), Serikali iiombe Taasisi hii kubadili deni lake kuwa mtaji katika Kampuni ya GTEAL na kisha kutafuta mbia (Strategic Investor) kukifufua kiwanda. Katika kukifufua kuwe na mkakati makini wa kuhakikisha kuwa mashine zilizokuwa zinatumika kabla ya kufungwa kwa kiwanda hicho zimerejeshwa na kupatiwa uwezo wake wa kuzalisha na kufungwa katika kiwanda
hicho ili uzalishaji uanze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi ya Upinzani inatoa pendekezo hili baada ya kujiridhisha kuwa nchi yetu imekuwa soko la magurudumu yasiyokidhi kiwango. Watengenezaji wengi wa magurudumu kutoka katika nchi za Asia na Ulaya wamekuwa wakizalisha magurudumu ambayo
hayawezi kuhimili barabara zetu na hali ya joto katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushahidi kwamba magurudumu haya hayamudu changamoto za barabara zetu na hali ya hewa huku kwetu ni kutokea kwa ajali nyingi ambazo zinagharimu maisha ya Watanzania wengi na kuwaacha wengi wakiwa na ulemavu wa kudumu mara kwa mara, baada ya tairi hizo kupasuka ovyo au kuyeyuka barabarani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni matumaini ya Kambi ya Upinzani kwamba Kamati ndogo iliyoundwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC) itakuwa imemaliza kazi yake, hivyo Kambi ya Upinzani inataka taarifa yake iwasilishwe Bungeni haraka na hatua za
utekelezaji zichukuliwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Kiwanda cha Nguo Mwanza (Mwatex), kiwanda hiki ni mojawapo ya viwanda vilivyofunguliwa na Muasisi wa Taifa letu kwa lengo la kutoa ajira na kupata soko la wakulima wa pamba. Mwaka 1999 wafanyakazi zaidi ya 1500 waliachishwa kazi ghafla kwa kisingizio kuwa kiwanda hakina uwezo wa kujiendesha. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuwaeleza wafanyakazi hatma ya maslahi yao, ina mkakati gani wa makusudi wa kukirejesha kiwanda hicho katika hali yake ya awali ya uzalishaji ili kuepuka kuuza pamba ghafi nje
ya nchi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika miaka ya 1980 viwanda vya magunia vilikuwa vikifanya kazi kwa asilimia 100 na kupata tija kubwa sana. Ajira ilipatikana viwandani humo kwani Watanzania wengi waliajiriwa katika mashamba ya mkonge na viwanda husika. Serikali ilipata fedha nyingi za kigeni kutokana na biashara ya magunia na kamba za katani katika soko la dunia.

Kambi ya Upinzani inasikitishwa na namna sera ya uwekezaji inavyotekelezwa kwa kuua kabisa zao hili muhimu. Mathalani kiwanda cha magunia cha Mjini Moshi kilikabidhiwa kwa mwekezaji ambaye sasa amekifanya kiwanda hicho kuwa godown. Mashine zote zimeng'olewa katika kiwanda hicho na kuliacha jengo lile kuwa ghala tu la kuhifadhia mali. Mwekezaji analalamikia Serikali kuweka ugumu kwake kupata soko baada ya kufungua soko la magunia kuingia nchini kwa bei rahisi sana. Kambi ya Upinzani inaishauri Serikali kutoa waraka wa kuyataka mashirika yote yanayofungasha mazao ya chakula kama vile mahindi, mchele, kahawa, korosho, mbaazi, maharage na kadhalika kuwa yafungashwe mazao hayo katika magunia ya katani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, faida ya kuhifadhi nafaka kwa kutumia magunia yatokanayo na mkonge na viwanda vya hapa nchini ni nyingi. Nitaelezea chache tu, kwanza tutaendeleza kaulimbiu ya Kilimo Kwanza kwa vitendo kwa kuwaendeleza wakulima wetu kwa kupata ajira katika mashamba ya mkonge, pili, wananchi watapata ajira katika viwanda vinavyozalisha magunia na Serikali itapata fedha kutokana na kodi na viwanda hivi na kulioongezea Taifa
mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi ya Upinzani inapenda kutoa angalizo kwa wenye
viwanda vya magunia hapa nchini kwa kupata fursa ya kuuza magunia ya kuhifadhi nafaka wasichukulie ndio njia ya kuuza magunia kwa bei wanayoamua. Lazima bei iweze kulingana na bei ya soko. Kwa upande mwingine Serikali ichukue jukumu la kutoza kodi kubwa kwenye magunia
yanayotoka nje ili kulinda masoko ya ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wajibu wetu kama watunga sheria na wawakilishi wa wananchi kuhakikisha tunaweka Utaifa wetu mbele na mengine yafuate baadae. Kama nchi hii tunaweza kuagiza magunia kutoka nje ya nchi kwa nini sisi tusiwe ndio tunapeleka magunia hayo
nje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Kiwanda cha Nguo cha Urafiki, Serikali ya Tanzania inamiliki hisa asilimia 49% na Serikali ya watu wa China wanamiliki hisa 51%. Kiwanda cha ubia kilianza kazi rasmi tarehe 01/04/1997. Asilimia 49 ni nyingi mno hivyo kukosekana kwa ufuatiliaji wa mara kwa mara katika masuala mbalimbali yanayohusu uendeshaji ni kosa ambalo limesababisha Serikali kupata hasara kubwa. Katika hatua ya kukiimarisha kiwanda Serikali ya China ilitoa mkopo
wa USD 27,000,000 kwa ajili ya ununuzi wa mitambo mipya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichotokea ni kwamba fedha hizo zilitumika kununua mitambo mikuu kuu. Aidha, wafanyakazi waliendelea kupunguzwa badala ya kuongezwa kutokana na kufufuliwa kwa mitambo, jambo ambalo kama kweli mitambo ingelikuwa ni mipya ajira
zingeongezeka na siyo kupungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali inafahamu kuwa baadhi ya mitambo imekuwa ikiuzwa kama vyuma chakavu? Aidha, Waziri alieleze Bunge lako Tukufu ukaribu wa Serikali kwa ujumla na uendeshaji wa Kiwanda chetu ukoje? Kwani Serikali ndiyo iliingia ubia na Serikali ya watu wa
China.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, msuguano mwingine unatokana na ukweli kwamba wakati Bodi ya Pamba ilivitaka viwanda vyote vinavyotumia bidhaa ya Pamba kama malighafi muhimu katika uzalishaji wa bidhaa zake kuipelekea mahitaji yao ya pamba kutokana na kupanda kwa mahitaji ya pamba kwenye soko la dunia, menejimenti haikupeleka mahitaji ya kiwanda kwenye Bodi hiyo na matokeo yake, Bodi hiyo ikauza pamba nyingi kwenye soko la dunia. Matokeo yake ni kiwanda hicho kukosa malighafi ya kutosha na hivyo kupunguza
wafanyakazi kwa kisingizio cha kutokuwa na malighafi (pamba) ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa nchi yetu inakabiliwa na wimbi kubwa la ukosefu wa ajira, hivyo basi ninaiomba Serikali kupitia kwenye Bodi ya Mamlaka ya Pamba kuweka kipaumbele katika mauzo ya pamba kiwe ni viwanda vya ndani kwanza kabla ya kuuza nje ya
nchi, hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa mtafaruku wa bei ya pamba ulioko hivi sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiwanda cha Viberiti cha Mjini Moshi (Kibo Match) ni kati ya viwanda vyenye kuzalisha ajira zisizopungua 600. Hali ya kiwanda hiki kwa sasa iko taabani, punde kitafungwa kutokana na kukosa uwezo wa kujiendesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ugonjwa mkubwa uliokikumba kiwanda hiki ni ushindani usiodhibitiwa. Viberiti vingi kutoka nje vimevamia soko letu na kutokana na kutokuwepo kwa kodi maalum kwa waagizaji ikiwa ni pamoja na tatizo la kutokuwa na umeme wa uhakika. Kwa lengo la kukinusuru kiwanda basi kiwanda kimejikuta kikishindwa kabisa kumudu ushindani katika soko hili holela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi ya Upinzani tunaitaka Serikali kutoa njia mbadala za kuokoa kiwanda hiki ambacho kimeajiri mamia ya Watanzania ambao ajira zao zinakuwa si za uhakika mara kwa mara kutokana na kusuasua kwa soko la viberiti ambapo hali hiyo husababisha kiwanda kushindwa kujiendesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Kiwanda cha Sukari cha Mtibwa, Kiwanda hiki kilibinafsishwa mwishoni mwaka 1998 katikati ya mabishano na upinzani wa wafanyakazi wa kiwanda, wakulima na Serikali; hoja za wafanyakazi na wakulima wa miwa ilikuwa kwamba
kiwanda hakina matatizo yoyote ya kujiendesha na hivyo hakihitaji ubinafsishaji. Hata hivyo kiwanda kilibinafsishwa kwa nguvu ya Serikali na siyo kuwa kilikuwa na matatizo ya kiutendaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu kubinafsishwa kiwanda hiki kumekuwa na migogoro ya
mara kwa mara na endelevu hadi sasa:-

(i) Migogoro kati ya Kiwanda na Wakulima wa miwa;

(ii) Migogoro kati ya kiwanda na wafanyakazi wake;

(iii) Migogoro kati ya kiwanda na wafanyakazi wastaafu; na

(iv) Migogoro kati ya Kiwanda na vijiji majirani zake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuwaeleza wananchi wa
Mtibwa matatizo haya yataisha lini? Hadi sasa kiwanda hiki kinadaiwa jumla ya shilingi milioni 421 ikiwa kodi stahiki ya 0.3% kwa Halmashauri ya Mvomero kutokana na mauzo ya sukari, je, fedha hizi
zitalipwa lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Maonesho ya Sabasaba ya 34 ya mwaka 2011; Kambi ya Upinzani inapenda kuwapongeza TanTrade kwa maonesho ya mwaka huu 2011 ambayo yalikuwa yameandaliwa vizuri sana. Utaratibu wa kuingia katika maonyesho ulikuwa mzuri ikiwa ni pamoja
na suala zima la ulinzi na usalama wa raia na usafi kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo Kambi ya Upinzani bado tunatoa ushauri ili kuweza kuongeza kipato katika viwanja vya Sabasaba kuwe na maonesho endelevu tofauti, kila baada ya miezi mitatu. Kwa mfano maonesho ya vyakula pekee, maonyesho ya
magari na mwisho yaje yale ya jumla ya Sabasaba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi ya Upinzani inapendekeza pia kuwa maonesho kama yale ya Sabasaba yafanyike Kikanda kwa lengo la kuwakutanisha wazalishaji mbalimbali na wadau pamoja na kuwapatia masoko kwa wale wasioweza kufika Dar es Salaam kwenye
maonesho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaishauri Serikali iweke mkakati wa kuwaorodhesha wazalishaji wote wa viwanda vidogo vidogo ili iwezekane kuwashirikisha katika maonesho hayo mbalimbali ndani na nje ya nchi kama vile maonyesho ya Jua Kali Afrika Mashariki. Lengo la maonesho haya pia liwe kutoa mafunzo ya kuongeza tija katika uzalishaji wa bidhaa zao za
viwandani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bandari za Tanzania zinalalamikiwa sana kutokana na ucheleweshaji katika kutoa mizigo iliyoko forodhani. Mathalani inachukua si chini ya siku sita
kutembeza karatasi za kutoa mizigo bandarini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hakika tatizo la kucheleweshwa kwa utoaji wa bidhaa bandarini halitokani na ubovu au uduni wa miundombinu bali ni ukiritimba unaotokana na
mlolongo wa madawati yanayotakiwa kupitiwa hadi kufikia hatua ya kutoa mzigo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi ya Upinzani tunaitaka Serikali kuweka utaratibu mzuri wa kutoa mizigo bandarini na kuondoa kabisa mianya yote ya ukiritimba bandarini hapo ili
kuwawezesha wafanyabiashara kutovunjika moyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, malalamiko mengi yalikuwepo kipindi cha Sabasaba kwa waonyeshaji (exhibitor) kushindwa kukomboa mizigo yao bandarini hadi maonesho kukaribia kufungwa, hili siyo jambo zuri kwa nchi yetu. Nchi inayoyatangaza maonesho nchi za nje zije wakifika wanakutana na kero tele za kukomboa mizigo yao. Hii ni aibu kwa Serikali na hivyo
tunaitaka kuchukua hatua za kurekebisha kero hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila kitu ni biashara. Uendelezaji wowote ni biashara, kufanya kitu kiwepo ni biashara, uhai wa watu ni biashara, kuulinda huo uhai pia ni biashara. Kambi ya Upinzani imejiridhisha kuwa Serikali haina mpango wa kuwawezesha wafanyabiashara wa Tanzania
kufanikiwa kufanya biashara kwa mafanikio na tija kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na ukweli kwamba Serikali haijawa tayari kubeba mzigo wa kuwawezesha kiujuzi wajasiriamali pamoja na kuweka sera zitakazozilazimu taasisi za mikopo na benki zilizoko nchini kutoa mikopo rafiki kwa wajasiriamali wetu, ni wajibu wa Serikali kuweka mazingira mazuri kwa wazawa kumudu biashara na ushindani katika biashara husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali ikiwawezesha wananchi wake kufanya biashara zenye tija, uchumi utainuka kwa kasi kubwa. Tatizo la ajira litapungua sana kama si kutoweka kabisa na soko letu la ndani litakuwa na bidhaa zenye uhakika wa ubora kwa usalama wa walaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi ya Upinzani inaona kuwa hili linawezekana kabisa. Imekuwa ikionekana bayana kwamba wawekezaji kutoka nje ya nchi wanaingia nchini na briefcase tu yaani wanakuja bila mtaji hata kidogo ama wanakuja na mtaji kidogo sana lakini kama vile tumerogwa, mabenki yote yanafungua milango na Serikali inawapa wawekezaji hao fursa za kukopa na kuendesha biashara zao kwa mafanikio makubwa. Hatimaye wanaondoka
nchini wakiwa wamepata faida nono mno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi ya Upinzani inashindwa kuelewa kwa nini milango inayofunguka mbele ya wawekezaji wa kigeni haifunguki kwa wajasiriamali wazawa? Aidha, Kambi ya Upinzani inashauri masharti ya uwekezaji yawe ya usawa baina ya wageni na wazawa, kwani ilivyo wazawa wanaumia zaidi. Mfano mzuri ni katika ulipiaji wa ankara za umeme na maji wote wanalipa sawa lakini wageni wanapata unafuu wa kulipa kodi, jambo linalopelekea
kutokuwepo kwa mazingira sawa katika ufanyaji wa biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaonekana kuwa Taifa lisilojali watu wake kwa kuwapendelea sana wageni na kuwatelekeza wazawa. Maandiko matakatifu yanatanabaisha kuwa nchi yenu itakuwa imelaaniwa mtakapowapa wageni heri na kuwafanya wana na mabinti wenu kuwa
watumwa katika nchi yenu wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi Rasmi ya Upinzani inaacha changamoto hii kwa kuitaka Serikali kuonyesha kwamba ina nia ya kweli ya kuondoa umaskini kwa Watanzania na kwa Taifa
kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mawasiliano ndiyo nguvu ya biashara, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali itambue kuwa mawasiliano ya simu, posta, internet, fax na kadhalika ni nyenzo muhimu sana katika kufanikisha biashara. Kambi ya Upinzani inashauri Serikali sasa ione umuhimu wa kusaidia upatikanaji wa mawasiliano ya simu posta, benki, internet kwa wingi hadi vijijini. Ijulikane kuwa internet si anasa bali ni zana za kazi katika kuwezesha biashara kufanyika kwa ufanisi. Kambi ya Upinzani inapenda kuipongeza Serikali kwa kuendelea na juhudi za kufunga
mkongo wa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sekta ya viwanda vidogo na biashara ndogo, nchi zilizopiga hatua kubwa katika uchumi kama vile Malaysia, Indonesia, Trinidad na Tobago zilichukua hatua za makusudi kuwawezesha wazalendo kuanzisha viwanda vidogo vidogo vyenye tija, kuanzisha ama kwa ushirikiano au kibinafsi (individually) viwanda vya kati na vile vikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vidogo, vya kati na vikubwa havitokani tu na bidii ya wananchi na au wawekezaji. Ni sharti Serikali itengeneze sera nzuri na kuweka miundombinu rafiki
kwa ajili ya kuwezesha uanzishaji, uendeshaji, ukuaji na usalama wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tija katika sera ya Kilimo Kwanza haiwezi kuonekana hadi pale
ambapo tutakuwa tunawawezesha wananchi wetu kuzalisha na kuuza mazao ambayo yameongezewa thamani katika viwanda. Kama kilo moja ya pamba inayouzwa shilingi 800 - 1,100 inatengeneza mashati manne na kila shati likauzwa shilingi 10,000 tu, basi tukiwezesha Watanzania kutumia pamba yote nchini kwa kuwawezesha kujenga na kuendesha kwa tija viwanda vya nguo
pamba kilo moja ingepanda thamani hadi kufikia shilingi 20,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni mfano ambao Waheshimiwa Wabunge wote hapa Bungeni wanaujua na wana uchungu nao na dhana ya Mheshimiwa Rais ya maisha bora kwa kila
Mtanzania yatafanikiwa kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO); naipongeza SIDO kwa jitihada inayofanya kuwawezesha wajasiriamali lakini SIDO ingeweza kufanya vizuri zaidi kama Serikali ingeamua kuchukua hatua za makusudi kuwawezesha kifedha zaidi ili waweze kutengeneza viwanda vidogo/vya kati katika kila vijiji ili wakulima waweze kusindika na kuongezea
mazao thamani kulekule kijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uboreshaji huu kwa kiasi kikubwa utaondoa tamaa ya vijana kukimbilia mijini ambako wakifika huko badala ya kupata ajira wanaishia kupigwa mabomu ya
machozi na kupigwa kwa kuambiwa wamevamia maeneo yasiyoruhusiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi ya Upinzani inahoji kwa kiasi hiki cha shilingi bilioni 1.6 walichopewa SIDO, kweli Serikali ina nia thabiti ya kuwakomboa wajasiriamali au ni fedha za kulipa wafanyakazi mishahara? Ukizingatia kuwa walikuwa wameomba kupatiwa jumla ya shilingi bilioni
11.23?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) pamoja na kuwa na umuhimu mkubwa katika ukuaji wa uchumi kwa shirika hili, imekuwa kawaida kuona kuwa NDC inaendeshwa kama shirika linalogharamiwa na Serikali kwa miradi yake yote. Ni pendekezo la Kambi ya Upinzani kwamba kuanzia sasa NDC iendeshwe kibiashara, ikifanya miradi yake kibiashara na kwa utaalamu zaidi ili kupata faida na kuweza kujiendesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkataba wa ubia baina ya Shirika la NDC na Kampuni Sichuan Hongda toka China ili kuendeleza Mradi wa Mchuchuma - Liganga ni muhimu usainiwe sasa kwa haraka na Serikali ishauriwe kutimiza wajibu wake kwa hatua ambayo NDC imefikia ikizingatiwa faida za kiuchumi za mradi huu. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa taarifa ya utekelezaji kuhusiana na mradi huo. Mazingira ya sasa ya uchumi wa dunia na mahitaji ya Taifa ni muafaka kwa miradi ya makaa na chuma. Kuchelewa kuanza kwa miradi hii kunaweza kusababisha miradi isifanyike kabisa kwani uchumi wa dunia kwenye bidhaa za chuma huwa unayumbayumba sana
(fluctuations).

Mradi huu ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi yetu, ni vema tukaweka utaratibu wa kupata taarifa kila Mkutano wa Bunge juu ya utekelezaji wa mradi huu kama Kauli za Mawaziri
kuhusu utekelezaji wa mradi wa Mchuchuma na Liganga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kampuni tanzu itakayoundwa ili kuendesha miradi hii ifuate taratibu zote za uchimbaji ikiwemo kusainiwa kwa Mkataba wa Uendelezaji Migodi (Mineral Development Agreements-MDA) kwa madhumuni ya kulinda maslahi ya Serikali, watu wa Ludewa na kampuni yenyewe. Hapa tunasisitiza, faida kwa wananchi wa Wilaya ya Ludewa na badala ya kuwa na kinachoitwa win-win situation katika ya Serikali na mwekezaji, tuite win-win-win situation
na hii win ya mwisho ni wananchi wa Ludewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa suala la ubia limeishaamuliwa, ni bora kuangalia namna ya kufanya marekebisho ili ubia uzingatie kanuni ya faida (profitability and pay back period) au baada ya mwekezaji kurejesha mtaji wake basi hisa za Serikali zipande. Kwa mfano, NDC waanze kuwa na hisa 20% lakini mara baada ya mradi kulipa (payback period) umiliki wa hisa uwe ni sawa kwa sawa. Pendekezo hili pia lizingatiwe kwa mradi wa Ngaka ambapo NDC wanahisa 30% kwenye Kampuni tanzu ya TANCOAL Energy. Miradi mingine yote inayohusu
rasilimali madini ya Taifa iwekewe utaratibu wa aina hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bajeti iliyotengewa NDC ya shilingi bilioni 7.06 wakati wao waliomba jumla ya shilingi bilioni 24.35, kwa utekelezaji wa miradi minne mikubwa ambayo ni Liganga, Magadi Soda, Mradi wa kuangamiza mazalio ya mbu Wilayani Kibaha, ili kuingia kwenye ubia wenye faida ni lazima uweke mchango wako. Hivyo basi katika miradi ambayo NDC inaingia ushirika na makampuni toka nje mchango wa shirika hilo kwenye ubia ni muhimu zaidi, vinginevyo nchi yetu itaendelea kuwa wasindikizaji na kuwatengeneza faida wabia wetu na sisi tukibakia
masikini bila kupata faida yeyote kwenye ubia huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa Magadi Soda ni mradi mkubwa na muhimu kiuchumi (ukitekelezwa Taifa letu litapanda chati duniani kwa kuwa wazalishaji wakubwa wa Magadi - Soda duniani, watu watapata ajira, Bandari ya Tanga itapata biashara kubwa na uchumi wa Taifa utakua). Lakini kulitokea kutokuelewana baina ya Serikali na wanaharakati wa mazingira. Kambi ya Upinzani inataka Serikali kutoa kauli kuhusiana na je, mradi huo unaendelea au umesimama?

Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme na viwanda; viwanda ni moja ya sekta zinazoathiriwa sana na janga la ukosefu wa umeme linaloikumba nchi yetu kwa sasa. Tayari Umoja wa Wamiliki wa Viwanda umeshatangaza athari mbalimbali wanazozipa kutokana na janga hili ambalo mwisho wake ni kuathirika kwa uchumi wa nchi kwa wenye viwanda kushindwa kulipa kodi kwa
Serikali kama inavyotarajiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi ya Upinzani inashindwa kuona ni jinsi gani Serikali itawezesha kuendeshwa kwa sekta ya viwanda bila kuwepo kwa umeme wa uhakika. Tunaishauri Serikali kuona kwamba sasa umefika wakati suala la umeme lipatiwe suluhisho la kudumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi ya Upinzani inaamini kwamba vipo vyanzo vingi vya umeme ambavyo vinaweza kabisa kutumiwa na kupata umeme wa uhakika na pengine kuwa na ziada ya kuuza nje. Lakini inaonekana kwamba Serikali haipo makini katika suala hili na tunawashauri wazingatie mapendekezo kama yalivyowasilishwa na Waziri Kivuli wa Nishati na
Madini Mheshimiwa John Mnyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, EPZA ni mpango mzuri wa kuwavutia wawekezaji. Lakini ni lazima izingatie maslahi ya wazawa kwenye haki zao kama malipo ya fidia pindi wanapowapisha
wawekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna malalamiko mengi ya kulipwa fedha kidogo kwa wananchi wale ambao maeneo yao yamechukuliwa kwa ajili ya uwekezaji huu, mathalani Wilaya ya Bunda mradi wa EPZA ulifanyiwa tathmini tarehe 17/10/2007 ukihusisha vitongoji vinne katika kijiji cha Tairo ambavyo ni Kitongoji ch Kirumi waliofanyiwa tathmini ni 404; Kitongoji cha Mabatini "A" waliofanyiwa tathmini ni 220 na Kitongoji cha Bushigwamara waliofanyiwa tathmini ni 203.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya tathmini hii kufanyika mnamo mwaka 2008 baadhi ya vitongoji ambavyo viligundulika kuwa havimo kwenye mradi vilipewa ahadi ya kulipwa fedha za usumbufu kutokana na kuacha kuendeleza maeneo yao navyo ni Kitongoji cha Mabatini "A" na
kitongoji cha Bushigwamara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa vitongoji tajwa hapo juu wahusika 220 kutoka Kitongoji cha Mabatini na wakazi 203 kutoka Bushigwamara hawajalipwa chochote. EPZA iliamua kuchukua Kitongoji cha Kirumi ili kitumike kwenye mradi na kuhamisha wakazi 404 kutokana na tathmini, lakini malipo ambayo hayalingani na tathmini ya maeneo yaliyochukuliwa yalifanyika kwa wakazi 116 tu, aidha, wakazi waliolipwa fedha kiduchu wanasubiri kupewa maeneo mapya
jambo ambalo hadi sasa halijafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuonesha mambo tatanishi katika zoezi hilo, eneo la Ndugu Kichele Nyasawanga lenye ekari 32, tathmini ilifanywa kwa ekari 25, tarehe 28/10/2011 alipokea hundi kupitia NMB ya shilingi 8,012,792 PV No. 9000458 kama fidia ya ekari 32 pamoja na
mali zilizokuwemo wakati wa tathmini, suala ni kwa vipi walilipa ekari 32 wakati tathmini ilikuwa kwa ekari 25? Sambamba na hilo kuna wakazi halali wa kitongoji hicho majina yao hayakuonekana
katika wale wanatakiwa kupewa fidia na kupatiwa maeneo mbadala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, toka tathmini ifanyike hadi sasa ni muda wa miaka mitatu, ambapo ekari moja ilitathminiwa kwa shilingi 300,000 lakini hali halisi ni kwamba thamani ya ardhi imepanda. Kambi ya Upinzani inataka kuelewa ni kwa nini wananchi wasilipwe fidia kwa bei ya
soko ambayo ni tofauti na wakati wa kufanya tathmini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kuna madai kama hayo Wilayani Bagamoyo ambapo wananchi walichukuliwa mashamba na makazi yao kwa ajili ya kupisha mradi wa EPZA lakini hadi sasa mwaka umepita tangu kufanyika kwa tathmini lakini hawajapewa fidia na kupewa maeneo mbadala. Wananchi hao walizuiwa kufanya shughuli yoyote ya maendeleo katika eneo hilo, jambo linalowaletea umaskini na kuwa ombaomba. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa kauli katika suala hili na kama wakilipwa walipwe kwa kuzingatia thamani ya sasa na sababu zipi zimepelekea kutolipwa kwa mrefu kiasi hicho tangu mwaka 2007.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu wa fedha EPZA imetengewa fedha za ndani kwa ajili ya kuendeleza maeneo maalumu ya EPZ na SEZ, lakini haionyeshi fedha za kulipa fidia kwa wananchi wanaohamishwa kupisha mradi huo. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali inapoingia mikataba na wawekezaji maslahi ya wananchi yawekwe mbele, Kambi ya Upinzani inataka
kuelewa kipaumbele cha Serikali ni kwa wananchi wake au kwa uwekezaji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Udhibiti wa Ushindani, Ubora wa Bidhaa za Huduma (TBS); Kambi ya Upinzani inapokea kwa mikono miwili hatua ya Tanzania kuingia katika bar code system. Hii itawawezesha wazalishaji wa Tanzania kuuza bidhaa nje ya nchi kwa halisi ya bidhaa zao bila kuonekana kuwa bidhaa zetu zinazalishwa nchi jirani. Mfano mzuri ni Tanzanite katika soko la Kimataifa Tanzania haijulikani kama ni mzalishaji mkubwa na pekee duniani wa madini hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TBS inahitaji kuharakisha uanzishaji wa kituo cha ufungashaji (Packaging Technology Center) ili iwezeshe kuwepo kwa ushindani mzuri hasa katika nyakati hizi za utandawazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, izingatiwe pia kuwa Tanzania inaingia katika Soko la Afrika Mashariki hivyo ni lazima tuzalishe bidhaa zenye uwezo wa kushindana katika soko kwa mafanikio. Kambi ya Upinzani inapendekeza kuwa kasma ya shilingi milioni 80 iliyotengwa kwa ajili ya TBS iongezwe ili kuipa uwezo wa kufanya kazi zake kwa tija, kwani kasma hiyo ni kwa ajili ya kuendeleza teknolojia ya vifungashio bidhaa tu, Kambi ya Upinzani inaamini kabisa kuwa TBS inatakiwa kufanyakazi nyingi zaidi za maendeleo zaidi ya hii ya vifungashio, mfano mazao ya kilimo hasa matunda na mboga mboga kwa minajili ya soko la nje ya nchi yawe katika viwango
vipi na yazalishwe kwa utaalam upi? Hii yote ni changamoto inayoikabili TBS

Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti, mafunzo na maendeleo ya teknolojia, moja ya jukumu la msingi la Wizara hii ni kusimamia taasisi zinazofanya utafiti na maendeleo ya teknolojia katika sekta za kilimo na maendeleo vijijini (CAMARTEC), taasisi nyingine ya TEMDO inaonyesha kuwa msisitizo wa utendaji kazi wake umewekwa katika kubuni mitambo na vifaa vya kusindika na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na mifugo, mitambo na vifaa kwa ajili ya nishati mbadala pamoja na mitambo na vifaa kwa ajili ya sekta ya madini. Uanzishwaji wa Taasisi hii ilikuwa ni maalum kwa ajili
ya utafiti na maendeleo ya uandisi kwa ajili ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia maudhui mazima ya utendaji kazi wa taasisi hizi mbili ni dhahiri kuwa zinafanya kazi zinazofanana, japokuwa uanzishwaji wa TEMDO ulikuwa maalum kwa ajili ya utafiti wa teknolojia kwa ajili ya viwanda ambavyo Muasisi wa nchi hii alifanya juhudi kubwa sana kuvianzisha. Kambi ya Upinzani kwa kuliona hili la muingiliano wa shughuli baada ya taasisi moja kujitoa katika kazi zake za msingi jambo ambalo kwa kiasi kikubwa viwanda vyetu vimeishia kubinafsishwa kutokana na teknolojia iliyokuwa inatumika viwandani kupitwa na wakati.

Ni vyema taasisi hizi zikaunganisha nguvu zake badala ya kuendelea kufanya kazi za kurudufiana,
mfano, taasisi zote zinatengeneza mashine za usindikaji wa mazao kama kupukuchua mahindi,
kukamua mafuta na matunda na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfumo wa Stakabadhi Maghalani, mfumo huu umekumbana na changamoto nyingi hasa kwa mazao ambayo ni mazao ya chakula kutokana na wakulima kutokupatiwa elimu ya kutosha juu ya utendaji kazi wa mfumo huu. Hivyo basi Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuweka Bajeti ya kutosha kwa Bodi ya Leseni za Maghala Tanzania ili watoe elimu
ya kutosha Tanzania nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuhitimisha hotuba yangu hii kwa kutoa tena shukrani zangu kwa Watanzania kwa kuendelea kuwa wavumilivu wakati huu mgumu ambao maisha yamezidi kuwa magumu na hatuoni hatua za haraka za makusudi zinazofaywa na Serikali ili kuwaondolea mzigo huu. Hata hivyo sisi tutaendelea kuwatetea Bungeni kwa kutoa hoja zenye nguvu na zinazokusudiwa kuishauri na kuitaka Serikali kutekeleza vyema wajibu wake kwa wananchi. Kazi hii tutaifanya kwa upole, uhakika, umakini, bidii kubwa na hakuna kulala mpaka
kieleweke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia napenda kuishukuru Wizara na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda na Biashara kwa ushirikiano ambao wamekuwa wakinipa pindi
yanapotokea majadiliano yahusuyo Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo Waheshimiwa Wabunge wenzangu, wadau wote wa maendeleo na wananchi kwa ujumla nashukuru sana kwa kunisikiliza Mungu
awabariki wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.